Tuesday, May 01, 2007

Tucta: Serikali acheni kufanya anasa

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nestory Ngulla, ameitaka serikali kupunguza matumizi ili iweze kuwalipa wafanyakazi wake mishahara minono itakayokidhi mahitaji yao.

Akihutubia katika sherehe za siku ya wafanyakazi katika uwanja wa Kirumba jijini Mwanza jana, Ngulla aliishauri serikali kupunguza safari za nje na za mikoani na kuacha kununua magari ya kifahari ili iongeze maslahi ya wafanyakazi.

Ngulla aliyasema hayo mbele ya Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa mgeni rasmi katika kuadhimisha sherehe hizo.

Alisema kwa kufanya hivyo, serikali itaweza kuongeza mshahara ya wafanyakazi kutoka kima cha chini cha Sh75,000 za sasa hadi Sh315,000 kwa mwezi.

Alisema serikali itafanikiwa kuongeza mshahara kwa wafanyakazi wake endapo pia itaacha kununua vitu vya samani, kupunguza semina na kuacha mpango wa misamaha ya kodi katika sekta mbalimbali na kuboresha hospitali ili watu waweze kutibiwa katika hospitali zetu na si kupelekwa nje.

Ngulla alisema endapo Serikali itafanya hivyo, itamudu mpango wa kuongeza mishahara ambayo itawawezesha wafanyakazi kumudu mahitaji yao ya kila siku. Pichani baadhi ya wafanyakazi wakiandamana kuadhimisha kilele cha sikukuu hiyo.


No comments: