
Bibi Kikongwe Asha Msawila wa Kijiji cha Mkamba, Morogoro akitoka nje ya kasri lake, hebu fikiria haya ndo maisha.
Picha hii imepigwa na Kaanaeli Kaale.
KWETU Tanzania, kidesturi unapoamka hakuna siku utaamka ukamsalimu jirani au ndugu yako wa karibu akakujibu kuwa mambo ni safi sana, ikitokea hivyo huwa ni nadra mno.
Unapotoa salamu, moja kwa moja tegemea majibu kama:
Habari mbaya, Tunaumwa umwa, Alhamdulillahi, Tunaendelea hivyo hivyo na mengine mengi. Ndugu zangu kina
Makene,
Ndesanjo,
Mwaipopo,
Jeff, na
Tungaraza nadhani bado wanaikumbuka hii hali.
Inawezekana tukajibu hivyo kwa vile huwa tunakabiliwa na matatizo. Wala sina maana kwamba tunapokuwa na matatizo, basi tusiseme hivyo, lakini sijui ni asili yetu kujisikia wanyonge au ni hali ya maisha ndiyoinayotupeleka hivyo, au ni walalamishi!
Wenzetu wa ughaibuni hapa niseme kabisa
weupe ni wawazi wanapokuwa na unafuu wa maisha husema kabisa mambo ni safi, mambo ni
barabara , murua na kila kitu cha namna hiyo, ni safi sana. Pengine ni kwa sababu walishatunyonya katika mfumo usio wa haki.
Lakini, hili la unyonge si la kulipuuzia hata kidogo, hebu tujiulize unyonge wetu huu unatokana na nini je ni uvivu wetu tu, na au ni uzembe?
Kama wanaojituma wanafanya kazi kwa bidii, damu au hata jasho, kwa machozi na mabavu wanafanya hivyo, lakini kila kukicha wanabakia pale pale hawasongi mbele, tujiulize, hivi tatizo ni nini hasa.
Zipo taarifa kwamba wananchi wengi sasa wamefuta baadhi ya milo ya siku, utakuta au wanakula chakula cha mchana pekee, halafu ndiyo basi tena.
Au wanakula chakula cha usiku pekee halafu ndiyo siku inakwisha au chakula kinasogezwa mpaka jioni halafu siku imekwenda hivyo.
Watafanyaje wakati bei ya mchele imepanda mara dufu hivi sasa inakimbilia Sh1,300 au zaidi wakati muda mfupi uliopita ilikuwa Sh600, mkaa ambao ndiyo kimbilio la wengi umefikia Sh22,000 kwa gunia wakati ulikuwa chini ya 10,000, maharage ya soya nayo hayashikiki wakati kipato kimebakia pale pale au kushuka.
Kwa mahesabu ya kawaida tu uchukulie mwananchi anayeishi mjini na kisha anafanya pengine kazi na mara nyingi ni kibarua analipwa Sh 60,000, kwa maisha ya sasa atafanya nini ili aweze kujimudu wakati kila kitu kimepaa.
Nauli ya daladala inazidi kupaa ilikuwa sh. 150 sasa inakimbilia 250 hadi 400, hii ina maana kwamba ikiwa ni kwa kwenda na kurudi ni kati ya Sh 500 na 1,000 hiyo kama mhusika ana usafiri wa moja kwa moja.
Hii ikijumlishwa kwa mwezi inamaanisha kuwa nusu ya kipato itaondoka kwa usafiri tu, bado chakula, bado watoto hawajaenda shule, bado hawajaugua na bado mlolongo mrefu wa vitu vinavyohitajika kwa maisha ya kila siku.
Yote hii inafanyika kwa kivuli kwamba bei ya mafuta imepanda, ukosefu wa mvua na umeme, ingawa sasa tatizo la ukosefu wa mvua limeondoka na limeingia jingine la maafa ya mafuriko.
Haya yote yanatoa kitu kinachoitwa,
Mshtuko wa moyo kwa wakazi siyo wa mijini tu bali hata wale wa vijijini sasa, ule wakati wa kuishi bila senti kwa muda hata wa miezi sita unakwisha na sasa kila kitu pesa tena pesa nyingi.
Mfumuko huu wa bei umefanya watu wengi wawe na mawazo kama ya rafiki yangu mmoja aliyeibuka na aina yake ya kaulimbiu, yeye ameigeuza kauli mbiu akisema :
Ari Mpya, Kasi mpya, maisha magumu kwa kila Mtanzania.
Kwa ufupi, maisha ya Mtanzania halisi maisha yake yamekuwa taabu tupu wakati hakuna dalili zozote za kuleta matumaini kesho itakuwa vipi! Yaani, inakuwa afadhali jana kuliko leo.
Kuna watu miongoni mwetu wameshakata tamaa ya kaulimbiu au maneno matamu matamu, kwa kuwa wanaona kila mtu amepotea, kila mtu anajali maisha yake binafsi na hakuna anayewatetea.
Watu kama hawa ni wengi siyo wa kuhesabu wanalalamika chini chini kwani hawana pa kusemea wanaishia kunong’ona na siku zinatokomea bila huruma.
Wakati kuna wajanja wanabugia au kula raha kwa fujo, wanawanyonya damu hawa hawa wenye kipato cha chini, wanaopata kipato kwa kutukanwa na kunyanyaswa.
Hata kama ni wachache, hao hawana budi wadhibitiwe ili wapunguze unyonyaji huo, wanatumaliza wenzao taratibu, kwa mfano kuna haja gani ya kupanga njama kuuza vitu kwa bei ya juu wakati mnaouza mnanunua shambani kwa bei ya chini.
Mbona mahindi yapo mengi. Mbona mchele upo mwingi. Mbona mafuta mnanunua kwa bei ya chini kwanini muuze kwa bei ya juu. Hata kama ni soko huria hii itakuwa ni
soko hulia. Lile la kihuni, ambalo halina huruma.