Ujambazi Ubungo ulipangwa ndani ya NMB

INAWEZEKANA kipindi kifupi kijacho tukawa tunavuna matunda adimu ya uhuru wa taifa letu ambalo wazee wetu wamelisotea kwa kutaabika, kuunguzwa, kuumizwa na kunyanyasika.

Nasema inawezekana hivyo kwa dalili moja au mbili zinazojionyesha katika serikali yetu ya awamu ya nne. Kwanza ni kwa sababu ya ujasiri wa viongozi wa sasa, lakini pili kwa sababu ya kuthubutu kwao kutenda mambo.

Wameingia madarakani katika kipindi ambacho baadhi ya polisi wamekuwa majambazi, madaktari kadhaa wamekuwa wauaji, walimu wengi wamekuwa wafelishaji, wahandisi lukuki wamekuwa wabomoaji, wazuia rushwa kuwa walaji, walinzi wa amani kuwa wachafuzi na mambo mengi.

Kipindi ambacho mwizi anasifiwa kwa ujemedari, muadilifu anadharauliwa kwa moyo wake, mhalifu anasujudiwa anaonekana shujaa asiye mhalifu anaonekana mbumbumbu asiyefaa kabisa.

Wengi wetu tumekuwa tukivuna machungu ya uhuru, pengine kutokana na utamaduni huu wa ulafi, hofu, kulindana na kuogopana kulikokuwapo na au kuliopo katika mikono ya watawala.

Tumekuwa mabawabu na washuhudiaji tu wa utajiri wa wenzetu wanabeba kila kilicho chetu wanapeleka katika mataifa yao, sisi wanatuachia madhila, wanatuachia mashimo, wanatuachia balaa. Mbaya zaidi wanabeba mpaka akili zetu, tunabakia na akili za kushikiwa.

Mengi yamekua yakifanyika hivyo huku wanaofanya hivyo wakitumia zaidi 'ujomba' wa kisiasa na wakati mwingine kujificha katika kivuli cha utaifa.

Kitu ambacho ni kinyume kabisa na ninavyoufahamu utaifa unaotokana na shauku ya kujiambatanisha na kundi unaloshirikiana nalo historia na uzoefu.

Hisia hizi hutokana mara nyingi na utashi wa makundi yaliyodharauliwa kujikomboa kutoka katika minyororo ya ukandamizaji na kutamani kunufaika na matunda ya uhuru.

Hisia hizi zimekuwa zikipotea na mara chache sana kujirejesha. Zinapotea kwa sababu wapo wajanja wanatujazia ujinga kwamba huu ni wakati wa dunia huria na sisi kujisahau kabisa na kuiacha mipaka yetu wazi bila ulinzi wa kutosha matokeo yake ni kuletewa madhila mengi lakini leo nitazungumzia hili la ujambazi.

Kwao wenzetu pamoja na kwamba wapo hulia lakini wapo makini kuilinda mipaka yao, kuwajaza watu wao utaifa na kuwaimarisha kisaikolojia ili wanapokutana na masuala yasiyoendana na utaifa wao hupinga na kushirikiana kwa namna zote na kuondokana nayo.

Hebu kumbuka matukio mengi ya mabaya ya kihalifu likiwamo hili la juzi pale Ubungo la ujambazi ni dhahiri yanatokana na kuyeyuka na pengine kushuka kwa ari ya utaifa ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuwaribisha na kuwatunza raia wasio wema wa nchi jirani.

Imeripotiwa mara kadhaa kuwa wanaopora fedha mara nyingi huwa si watanzania si kwa muonekano bali hata kwa lafudhi. Wengi wanatoka nchi jirani za Kenya, Burundi na au Rwanda, sasa hapa kunakuwa na faida gani ya kuzembea?

Na mara zote hizo wanazopora wanapotea na hawapatikani na hata fedha wanazopora hazipatikani hii tafsiri yake nini? Ni kwamba tunawapokea na kuwalea na kuwatunza humu ndani ya nyumba zetu, wengine miongoni mwetu kwa posho kidogo sana, badala ya kuwashughulikia.

Aina hii ya uzembe itatupeleka pabaya tutakuwa hata hatuwezi kutembea kwa amani kwani iwapo sasa hivi upitaji wa baadhi ya maeneo ni matatizo je tunavyoendelea 'kuwabeba' wahalifu tunategemea nini?

Nyingine inatokana tu na ubinafsi uliosheheni miongoni mwetu kwani haiwezekani kabisa wale waliopora pesa na kuua watu wakawa wamejiamulia tu, ni mpango uliosukwa aidha ndani ya NMB au BoT.

Hivyo cha msingi ni kuhakikisha wale wote waliosuka mchoro wa uporaji wa pesa hizo wakakamatwa na kufikishwa panapohusika kama Rais Jakaya Kikwete alivyoagiza kwani wote ni wauaji.

Jitihada zilizoonekana juzi Ubungo wakati majambazi yalipopora Sh 150 milioni zinatakiwa kupongezwa na kutiwa nguvu kwa kuwa sasa kama nilivyotangulia kusema hapo juu, zimeonyesha ipo serikali.

Hatujazoea kuona helikopta ikifanya doria, wala kusikia risasi zikimiminwa mtaani kama cheche za moto majumbani kwetu, lakini uzembe wetu (raia) ndiyo unaosababisha yote haya.

Kwa hiyo uchungu wetu kwa taifa letu, kutopenda kuwatunza wahalifu kutatufanya tujiokoe na mengi yanayofanana na haya yanayotokea sasa, tusiogope kuwaumbua wahalifu wanapopanga mikakati ya uhalifu.

Comments

boniphace said…
kaka mimi nipo hapo para ya nne tu! Hiyo ndiyo Afrika yetu leo, nani aliruhusu ufa huu? Tunatakiwa kujadili na kuumiza bongo ili tufunge safari.
Jeff Msangi said…
Charahani,
Matukio haya ya ujambazi,kuporomoka kwa uzalendo,kushikiwa akili zetu ni matokeo tu ya historia yetu na jinsi ambavyo tumeamua wenyewe kujihukumu.Ingawa nipo mbali huwa bado nina kumbukumbu kamili ya jinsi ambavyo ukosefu wa ajira umeshamiri nchini Tanzania.Nimekuwa nje kwa muda sasa lakini nina uhakika "vijiwe" vinazidi badala ya kupungua.Lazima tutazame upya kabisa mifumo yetu ya kiuchumi na kijamii bila kuacha kielimu.Lazima tubinue merikebu nzima.Kama ulivyosema hivi sasa yaonyesha pana serikali.Vyema.Basi ni wakati wa kuangalia ufa anaosema Makene kwa kutumia darubini hata kama tupo karibu na tunadhani tunaona!Lakini leo hebu tujiulize swali moja..hivi tulipomfukuza mkoloni tulibadili nini...au tulirithi yale yale tuliyoyapigania?Hili ni swali tu,nia yake ni kuangalia ubwanyenye,uonevu na vyote tulivyorithi.Ndio hukumu yetu ya leo?