Kwanini rushwa haiwezi kuondoka?

KWA kipindi cha karibu miezi mitatu sasa suala kubwa linalotikisa katika kila pembe za Afrika limekuwa ni rushwa. Tanzania Rushwa. Kenya Rushwa. Uganda hivyo hivyo na kwingineko kwingi Afrika.

Vyombo vya habari, jumuiya ya Wanadiplomasia na jumuiya za hiyari katika maeneo yote hayo zimekuwa zikijaribu kupigia kelele suala hilo kwa uwezo wao wote, lakini wapi.

Kote huko rushwa inakuwa ni kwa kiasi kikubwa inatokea katika ofisi za umma. Wapo wanaodhani kuwa watumishi wa umma wanakula rushwa sababu wanalipwa kidogo, lakini kwa upande mwingine hoja hii inaonekana kulemewa.

Rushwa inakuja kwa aina nyingi, ya kwanza ikiwa utoaji "kitu kidogo"; Upendeleo kwa kuweza kupatiwa nafasi, huku wanaostahili wakiachwa, ukabila au rushwa ya ngono.

Aibu gani hii! Bila shaka siku ambapo rushwa itaondoka nadhani siku hiyo hiyo ndiyo itakuwa mwisho wa umasikini, vita, Ukimwi, uhalifu n.k. Hata hivyo habari mbaya ni kwamba suala hili hadi sasa limeshindikana.

Kule Kenya serikali ya Mwai kibaki imepata kashfa ya kula mamilioni ya pesa ya walipa kodi wa Kenya. Maafisa wa ngazi za juu wa serikali hiyo, wamegundua namna ya kutafuna pesa kwa staili ya kisasa kwa kutengeneza makampuni bandia kama ya Anglo Leasing.

Siri ambayo imejitokeza ni kuwa katika kashfa hizo, viongozi wa serikali wamehusika kwa kuwekeza katika makampuni kwa kuficha utambulisho wao.

Huko Zambia, Rais mstaafu Fredrick Chiluba anakabiliana na mashitaka ya rushwa anayodaiwa kuyatenda akiwa madarakani.

Kwetu Tanzania vita dhidi ya rushwa imeendelea lakini kwa staili tofauti si kama ile ya Kenya. Serikali imetangaza rasmi kuanza kupitia upya mikataba ya kuchimba madini eneo mojawapo linalolalamikiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa.

Akitangaza haya wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete akiwa ziarani Gaborone, Botswana, alisema serikali yake itaongeza kasi ya kupambana na rushwa na jambo la kwanza ambalo imelifanya ni kuangalia upya mikataba mbalimbali iliyoingiwa kwa sababu, ndio chimbuko la rushwa kubwa ya kujineemesha.

Alisema tayari Baraza la Mawaziri limeanza kulizungumza suala hilo na kuangalia namna ya kupitia mikataba ya kuchimba madini na ili sekta hiyo iweze kunufaisha Watanzania pia. Na siyo kwa upande huo peke yake bali maeneo yote yanayohusishwa na rushwa.

Hatuwezi kufanana na Kenya, Lakini hata hapa kwetu kama ukweli utasemwa na haki itatendeka, basi wengi wa wale waliopo madarakani na walijificha katika kivuli cha uadilifu, watajikuta katika orodha ya aibu.

Kwamba, kama itakuwa ni suala la wanasiasa kuumbuana. Basi ni afadhali kusubiri kizazi kingine cha wanasiasa.

Jambo liletalo huzuni ni kwamba, kama 'mapapa' wa rushwa hawaondolewi, kama inavyojulikana, mamilionea watarajiwa wanaopata utajiri kwa njia za rushwa hawatajifunza wala kupata somo lolote. Wanalindwa kama vile wamekuwa miungu watu. Jambo jingine kubwa ni 'kuabudu' rushwa ambako kumo ndani ya bongo za watu. Kulijejenga hivyo na kutaendelea kuwa hivyo.

Kwa maana hiyo kutokana na mtindo huu, vijana masikini waliotoka vijijini kwa wazazi makabwela na hata kama wakiwa na vijipesa kidogo, wanaoingia katika ofisi za umma watalazimika kufuata nyayo za watangulizi wao ambao wanachota pesa za umma na kutokomea na hawaulizwi.

Rushwa haitatokomea kama hatutaachana na na utamaduni wa kutoa kitu kidogo kama ahsante. Rushwa kwa Afrika imekuwa kama ndiyo utamaduni na imekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

Ni lazima pia mtindo wa kuwaabudu na kuwasifia waliotajirika kwa kuiba mali za umma au za matajiri wao uachwe, ionekane kama dhambi isiyo mfano, tuwafundishe watoto wetu kuwa utajiri unatokana na kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika na si wizi wa mali ya umma na si vinginevyo na tujenge utamaduni huo kweli.

Comments

John Mwaipopo said…
Umegusa pahala pa ukweli ulipoandika rushwa imekuwa kama utamaduni Afrika. "Rushwa ni Rafiki wa haki" Nadiriki kuandika hivi kwani katika jamii zetu imekuwa hivyo na kukataa kutoa ama kupokea rushwa ni sawa na kujikana si wewe tu bali pia maisha yako. Yule mama aliyepoteza binti yake wa miaka 7 pale hospitali ya Amana alikuwa ama hana chochote cha kutoa rushwa ama alikuwa kang'ang'ania usemi "Rushwa ni Adui wa haki" Amekiona cha mtema kuni.

Lililonigusa sana katika chapisho lako ni hii maneno ya kutaka kupitia upya mikataba ya madini. Sijajua kwa nini madini kwanza na si kwigineko kama nishati na mawasiliano. Hapa nilipo natakia kila la heri tamko hili kwani pengine wanafahamu nini kilienda kombo katika mikataba hiyo huko awali. Lakini kwa kuwa walikuwa wanafikiria siku moja kuikwaa hatamu walinyamaa kimya. Hala hala isije kuwa ni tisha tisha ili wanaomiliki migodi wasijisahau kukata kidogo wakifikiri zama hazijabadilika. Falsafa ndogo niliyonayo ni kuwa ukitaka kukatiwa wewe tishia. Na tusubiri tuone.
boniphace said…
Charahani unapokuwa na taifa linal;osifia mla rushwa na kumuita mjanja hapo ni hatari tupu. tENA VIJIRUSHWA VYA PESA ZA KULA HIVI VINAWEZA KUMALIZWA LAKINI HAYA MARUSHWA MAKUBWA, mabayo yako katika mazingoira ya kutumia nafasi za madaraka kumiliki mali aau huduma funai na hayo mateni percent ambayo makampuni ya Afrika Kusini yamekuwa yakitoa? Halafu unarudisha madarakani watu kama akina Mramba, kufanya nini? Msitutanie jamani kuna watu wanapaswa kuwekwa kando kama kunahitajika kuchunguzwa mikataba. Safari inaendelea
Jeff Msangi said…
Rushwa ni vita,ni adui wa kila kitu kinachohusu maendeleo ya nchi.Hoja yangu siku zote imekuwa tujinyoshee vidole vyote kwetu sisi wenyewe kwanza..tukatae kuuza uchumi wa nchi kwa kutoa au kupokea rushwa..napenda zaidi hoja ya kutokukubali kutoa rushwa..hii inaanza na wananchi kujua haki zao za msingi.Kujua kwamba ukihitaji kiinua mgongo chako ni haki yako ambayo haitaki kabisa kuitolea rushwa..halikadhalika matibabu,elimu na mengineyo.Lililo haki usithubutu kulitolea rushwa.Simama imara,chachamaa unapoombwa rushwa kwa haki!
Mwaipopo, Makene, Msangi

Rushwa bwana sijui imekuwa kama ni ugonjwa wa kifikra kama msemavyo, inabidi watu kujitolea muhanga wasitoe! Lakini wasipotoa si wanaumia, au wanapoteza wapendwa wao kama yule mama aliyepoteza kabinti kake ka miaka saba kama anavyosema Mwaipopo.

Nakubaliana kabisa na hoja zenu wote, lakini utafanyaje hapa bongo ili uepuke kutoa rushwa, hebu chukulia kibanda chako hujakiwekea umeme halafu unaona kabisa ukitoa rushwa utawekewa baada ya siku mbili na usipotoa utakaa miezi nane hadi kumi, utafanyaje? Au huna kazi na unaiona kazi ile pale ukiacha huipati utafanyaje?

Mzunguko huu na mingine mingi inachangia sana kuifanya rushwa iendelee kustawi sijui tufanyeje tuikwepe hali hii. Yaani rushwa imetaasisishwa, kila kona ipo!
mwandani said…
Rushwa ya ukabila au udugu wakati wa kupatiana nafasi za kazi "ulaji" hizo ndiyo zinakwamisha utekelezaji tangu chini. Siku mtu atakapoomba kazi na kuajiriwa bila kutazama makandokando mengine zaidi ya uwezo wake wa kutenda, hapo nitasema sawa. Kwani rushwa hiyo ya udugu - kupeana feva - ndiyo inaleta kulindana, matokeo yake kila kitu kinakwenda visivyo.
Tuswafi huku chini chini kwanza hata tukifika mekoni asilimia kumi itakuwa haitolewi hata kiduchu.

Pagumu sana hapo, kusafisha rushwa kwenye maisha ya kila siku.Pagumu sana kwenye kusafisha akili.

Inatisha sana kwa mfano kuna kijana alitaka kunitemesha mzigo uwanja wa ndege. Wazi akitaka nimuachie kitu kidogo. Kama isingekuwa akili ya haraka angeniumiza.
Nashukuru sana ndugu zangu mwandani na jungu kuu, Rushwa bwana kama mnavyosema imejikita kutokea chini kabisa hadi juu kabisa na hivyo ikitathminiwa mlundikano wake ndiyo tunapata mizigo ya matatizo tuliyo nayo leo. Tuamke basi tuanze kupigana na rushwa kama vichaa vile bila shaka tutafanikiwa.