Saturday, February 01, 2025

TEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAFUNZO YA AMALI

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha (wa pili kushoto) akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Dkt. Leonard Akwilapo walipokutana kwenye maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo Jijini Dodoma. Kulia ni Bw. Godfrey Boniventure mjumbe wa Bodi ya TEA na kushoto ni CPA. Mwanahamis Chambega Kaimu Mkurugenzi huduma za taasisi TEA
Mjumbe wa Bodi ya TEA Bw. Godfrey Boniventure akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la TEA kwenye maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo jijini Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha akizungumza na vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwa ajili ya kutekeleza Sera mpya ya Elimu na Mafunzo jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi, Mjumbe wa Bodi pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti wa TEA walipokuwa kwenye uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo jijini Dodoma.


Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imejipanga kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia mafunzo ya amali kama sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, amesema jukumu la TEA ni kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa sera mpya ya elimu unahitaji miundombinu imara na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya amali.

Dkt. Kipesha ameeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haiwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuboresha miundombinu, hivyo TEA ina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa kwa viwango vinavyohitajika.

Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha, takribani shilingi bilioni 3 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa miundombinu katika shule 20, zinazotoa mafunzo ya amali kwenye fani za kilimo, TEHAMA, mapishi, ushonaji, michezo, na sanaa.

Katika kutekeleza Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kutafuta rasilimali fedha ili kuhakikisha miundombinu ya mafunzo ya amali inaboreshwa na vifaa vinapatikana kote nchini.

 

DC MPOGOLO USAFI ZOEZI LA KUDUMU ILALA


 





Katika kuhakikisha  zoezi la usafi linakua la kudumu, Mkuu wa wilaya ya Ilala  Edward Mpogolo amewataka wananchi, wafanyabiashara na taasisi zote ndani ya halmashauri hiyo kufanya usafi kuwa zoezi la kudumu.

Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala ameyazungumza hayo wakati wa zoezi maalum la usafi lililofanyika february mosi 2025.

 Mpogolo amesema mkakati wa Ilala ni kwa  Kanda namba 1 na 2 za Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuanzia eneo la Kamata, Mtaa wa Gerezani kupitia barabara ya Sokoine, Kivukoni front, Luthuli, barabara ya Barack Obama kuelekea fukwe za Dengue kufanyike usafi wa kila mara.

Amesema ili zoezi ilo liwe endelevu kwa kila mwananchi, taasisi, wafanyabiashara na wadau wengine waweke utaratibu wa usafi kila siku kabla na baada ya kuanza na kumaliza shughuli zao wahakikishe mazingira yanakua safi. 

Mpogolo amebainisha viongozi wamekubaliana  kulifanya Jiji la Ilala  kuendeleza usafi wa mazingira, taasisi, makazi  na fukwe zote  kuendelea kuwa safi.

Mpogolo amesisitiza   zoezi  la usafi kwa sasa katika wilaya ya Ilala ni la kila siku, huku zoezi la usafi wa pamoja la kila mwisho wa mwezi litaendelea ikiwa ni pamoja na kampeni za usafi za kila mara kuweka jiji safi. 

Aidha  Mpogolo ametoa wito kwa Wananchi, Taasisi na wadau mbalimbali wa mazingira kujitokeza katika mazoezi ya usafi  endelevu ili kuhakikisha jiji la Ilala  linaendelea kuwa safi kwa jitihada za pamoja kutokomeza uchafu na magonjwa ya mlipuko. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam amesema ofisi yake itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufanyia usafi vinapatikana katika mazoezi hayo kwa kushirikiana na Wakandarasi wa usafi wanaofanya kazi ndani ya jiji la Ilala.

Mkutano wa 19 wa ACA Kufanyika Dar es Salaam 2025, Kuangazia Uwekezaji katika Sekta ya Korosho

 





NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji katika Mkutano wa 19 wa mwaka wa Jukwaa la Korosho Afrika ambao kufanyika Novemba 18 hadi 22, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umendaliwa na Jukwaa la Korosho Afrika (ACA) kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania na Umoja wa Wabanguaji Wakubwa wa Korosho Tanzania (TACP).

Pia Mkutano wa 19 wa Mwaka wa ACA unakusudiwa kuhudhuriwa na washiriki wasiopungua 500 kutoka nchi zote Duniani zikiwemo nchi 33 zinazolima korosho.

Baadhi ya nchi hizo ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa habari Januari 31, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Tanzania , Francis Alfred amesema Mkutano huo unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye tasnia ya Korosho kuanzia shambani ambapo wanategemea kupata uwekezaji kwenye mashamba makubwa ya korosho, kuongeza ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi za Afrika.

"Kwa upekee Mkutano huu utatumika kuhamasisha matumizi ya korosho na bidhaa zake kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid - CNSL), sharubati (juice), maziwa ya korosho (cashew milk), mvinyo (wine), nyama ya mabibo (cashew apple meat) na pombe kali. Aidha bidhaa nyingine kama ethanol zinaweza kutumika kwenye maabara za hospitali na shule zetu na hivyo kupanua wigo wa soko la korosho". Amesema Alfred.

Amesema mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.

Aidha amesema Serikali imefanya juhudi kubwa za kuendeleza zao la korosho ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa imekuwa ikitoa pembejeo za korosho kwa wakulima kwa ruzuku ya 100%.

"Kwa mfano katika msimu wa 2024/2025 ruzuku ya pembejeo ilikuwa shilingi billioni 182. Utoaji wa pembejeo za ruzuku umechagiza kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 310,000 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia tani 410,000 kwa msimu wa 2024/2025 zilizouzwa kupitia minada". Amesema

Pamoja na hayo amesema ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji unaendelea kwa kukusanya takwimu za korosho zinazobanguliwa majumbani kwenye vikundi vidogo na watu binafsi pamoja na uzalishaji katika mikoa mipya.

Amesema hadi mwisho wa msimu makadirio ni kuzalisha jumla ya tani 500,000 katika msimu wa 2024/2025.

"Bei ya korosho ghafi katika msimu wa 2024/2025 iliimarika na kufikia shilingi 4,195 kwa kilo ikiwa ni bei ya juu kuliko bei zote zilizopatikana kutoka nchi yetu ipate uhuru.". Ameeleza Alfred.

Hata hivyo amesema pamoja na uwepo wa mahitaji makubwa ya korosho ghafi katika soko la dunia, uamuzi wa Serikali kutumia mfumo wa mauzo wa Soko la Bidhaa (TMX) umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushindani katika minada na kuchangia katika kuimarika kwa bei.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ACA, Ernest Mintah amesema Mkutano huo unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo hii itakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huukwani mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka sita, baada ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo mwaka 2008 na 2019.

Amesema Mkutano wa ACA umekuwa ukijikita kwenye mada kuu inayoundwa kupitia mchakato wa kina ili kuakisi hali halisi na kushughulikia changamoto kuu zinazoikabili sekta ya karanga duniani ambapo katika Mkutano huu itajikita zaidi na kauli mbiu ya "Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Karanga kwa Ukuaji Endelevu wa Uchumi."

"Mkutano wa mwaka huu utaangazia hitaji muhimu la kuwekeza kimkakati katika maeneo kama vile utafiti, maendeleo ya uwezo wa binadamu, miongozo ya sera, ubunifu na teknolojia, ufuatiliaji, usalama wa chakula, na mengineyo katika sekta ya karanga ili kuhamasisha ukuaji endelevu". Amesema Mintah.

Nae Mwenyekiti wa Umoja wa wabanguaji wa Korosho, Bahati Mayoma amesema ili kuweza kushiriki kwenye mkutano wa 19 wa mwaka wa ACA kila mshiriki atatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 400,000 kwa watakaojisajili na kulipia kabla ya tarehe 15 Oktoba 2025 na shilingi 500,000 kwa watakaojisajili na kulipia baada ya tarehe 15 Oktoba 2025 kwa watanzania .

Aidha kwa wageni amesema itakuwa nia dola za Marekani 500 kwa wanachama wa ACA na dola za Marekani 700 kwa wasio wanachama wa ACA kwa watakaojisajili na na kulipia kabla ya tarehe 13 Agosti 2025 na dola za Marekani 700 kwa wanachama wa ACA na dola za Marekani 1,000 kwa wasio wanachama wa ACA kwa wakakaojisajili na kulipia baada ya tarehe 31 Agosti 2025.

Tanzania Yajivunia Mafanikio Makubwa Katika Sekta ya Utalii















Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imevunja rekodi kwa kufikisha watalii milioni 5.3 (5,360,247) ambapo idadi ya watalii wa kimataifa 2,141,895 na watalii wa ndani 3,218,352 sawa na lengo lililojiwekea la kufikisha watalii milioni 5 ifikapo 2025.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) katika hafla ya kutangaza mafanikio katika sekta ya utalii,iliyofanyika jijini Dar es salaam, tarehe 31 Januari, 2025.

“Ninatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake makubwa na uongozi wake thabiti uliotuwezesha kufikia hatua hii. Kupitia jitihada zake, Tanzania imepata nafasi kubwa zaidi kwenye ramani ya utalii duniani, na tunazidi kuona matunda ya kazi hiyo kila siku” amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, ameweka bayana kuwa bado Wizara yake ina wajibu wa kuifikisha Sekta ya Utalii katika viwango vya juu zaidi ili kustahimili ushindani katika soko la Kimataifa na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta hiyo kuhakikisha inaendelea kuimarisha huduma, kuboresha miundombinu, na kupanua masoko ya utalii ili Tanzania izidi kuwa kivutio kinachopendwa zaidi duniani.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawapongeza na kuwashukuru wote mliochangia mafanikio haya. Kazi yenu ni ya thamani kubwa, na tutaendelea kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha mafanikio haya yanazidi kuimarika mwaka hadi mwaka” amesema Mhe. Chana.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwa na utashi wa kisiasa katika kuiendeleza Sekta ya Utalii.

"Pamoja na kazi kubwa mnayoifanya na kufika malengo ya ilani ni jambo kubwa sana lakini bado tuna kazi ta kufikia malengo kwenye mapato tuko bilioni 4 na malengo ni bilioni 6" amesema Mhe. Mnzava.

Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi amesema Wizara imejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa inatimiza lengo la makusanyo ya dola bilioni sita za kimarekani na kuzidi ifikapo Desemba mwaka huu.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Taasisi za Serikali, Mashirika binafsi na wadau wa utalii.

Rais Samia Azindua Sera ya Elimu na Kukabidhi Mobile Clinic

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini bango maalum lenye ujumbe kuhusu Elimu mara baada ya kukagua mabanda ya maonesho ya masuala ya Elimu katika viwanja vya ukumbi wa mikutano ya Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua mabanda ya maonesho kuhusu masuala mbalimbali ya Elimu kabla ya kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014, toleo la 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa kampuni ya SC Johnson Family Dkt. Fisk Johnson kutoka Marekani pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma leo tarehe 1 Februari, 2025.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014, toleo la 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.



Matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo kwa mwaka 2014, toleo la 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2025.

Dodoma, 1 Februari 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki katika hafla muhimu zilizofanyika jijini Dodoma, ikiwa ni hatua nyingine katika kuboresha sekta ya elimu na afya nchini.

Katika tukio la kwanza, Rais Samia amekabidhi magari ya huduma ya afya inayotembea (Mobile Clinic) kwa Wilaya za Sikonge na Uyui, mkoani Tabora. Magari hayo yametolewa na Jakaya Kikwete Foundation kwa ufadhili wa kampuni ya SC Johnson Family ya Marekani. 

Hafla hiyo imefanyika Ikulu Chamwino, ambapo Rais Samia amepiga picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa SC Johnson Family, Dkt. Fisk Johnson, pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Baadaye, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Rais Samia amezindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023. 

Kabla ya uzinduzi huo, alitembelea mabanda ya maonesho kuhusu masuala mbalimbali ya elimu na kusaini bango maalum lenye ujumbe kuhusu sekta hiyo.

Hafla hii imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa elimu na maendeleo, pamoja na wananchi waliojitokeza kushuhudia hatua hii muhimu katika mageuzi ya elimu nchini.


Rais Samia Akabidhi Mobile Clinic kwa Sikonge na Uyui






Dodoma, 1 Februari 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Matiku Chacha, mfano wa ufunguo wa magari maalum ya huduma ya afya inayotembea (Mobile Clinic) kwa ajili ya Wilaya za Sikonge na Uyui.

Magari hayo yametolewa na Jakaya Kikwete Foundation kwa ufadhili wa Kampuni ya SC Johnson Family ya Marekani, ikiwa ni juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa maeneo husika. Hafla hiyo imefanyika Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.

WAZIRI WA ULINZI NA JKT AWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA WIZARA BUNGENI

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb.), tarehe 22 Oktoba 2026, amewasilisha taarifa za utekelezaji wa Wizara ...