Monday, February 14, 2011

Precision Air yatua Bukoba


Ndege ya shirika la ndege la Precision juzi Jumamosi, ilitua rasmi katika uwanja wa ndege wa Bukoba na kulakiwa kwa furaha na watu wa mkoa wa Kagera baada ya kuisha kwa matengenezo ya uwanja wa ndege wa Bukoba.

Akizungumza baada ya kutua Bukoba Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air Alfonse Kioko alisema;

“Hii ni fursa na furaha kubwa kwetu kupata nafasi ya kutoa huduma zetu kwa wakazi na wadau wa mkoa wa Kagera baada ya kutokuwepo kwa muda wa mwaka mmoja sasa”

Uzidnuzi wa safari hizo unafuatia kumalizika kwa ukarabati wa kiwanza cha ndege cha Bukoba uliofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania.

“Huduma ya safari itakuwepo kila siku kutoka Dar es Salaam kupitia Mwanza na kutoka Bukoba kwenda maeneo tofauti katika mtandao wetu,” alisema Kioko.

“Tunaanza na bei ya Tshs. 454,000 kwa safari ya kwenda na kurudi,” aliongeza Kioko.

Katika safari za Bukoba Precision Air itatumia ndege aina ya ATR42-500 iliyobatizwa jina la Bukoba kama ishara ya shukrani kwa watu wa Kagera.

Ndege hii inauwezo wa kubeba abiria 48. Ndege ya aina ya ATR42-500 ni ya kisasa kabisa katika soko la ndege kwa sasa. Ndege hii ni mpya kabisa ambayo imefungwa na vifaa vya kisasa na bora zaidi vya michezo ya kufurahisha abiria. Ndege hii ilinunuliwa mnano mwezi wa Nane mwaka jana kwa hiyo ni moja kati ya ndege mpya kabisa za Precision Air.


Kampuni ya ndege ya Precision imedhamiria kutoa huduma bora kwa wateja wake kwa kutumia vifaa vyake vipya na vya kisasa katika soko la biashara ya ndege. Pia kampuni ina mpango wa kupanua mtandao wake nje ya nchi ikiwemo kuanzisha safari kwenda Johannesburg- Afrika Kusini.

Hivi karibuni watanzania watapata nafasi ya kumiliki sehemu ya Precision Air kwa kunua hisa zake katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Mnamo mwaka 2006 Kampuni ya Ndege ya Precision na kampuni ya kutengeneza ndege ya ATR walisaini mkataba wa Dola milioni 129 kwa ajili ya ununuzi wa ndege saba mpya katika mpango wake wa kuboresha ndege zake. Ndege ya mwisho kutoka ATR iliwasili Jijini Dar es Salaam mwezi Septemba mwaka jana.

Thursday, February 10, 2011

Mkapa: Kura ya maoni Sudan Kusini ilikuwa ya uhuru


Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya watu watatu iliyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuangalia mchakato wa maandalizi na hatimaye upigaji kura ya maoni katika Sudan ya Kusini. Ameliambia Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa matokeo ya kura hiyo ni ya haki, huru na kuaminika.

Rais Mstaafu Mkapa, ameyasema hayo siku ya jumatatu wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa yake mbele ya Baraza hilo, ikiwa ni siku mbili zimepita tangu kutangazwa rasmi matokeo ya kura hiyo yaliyoonyesha, kuwa asilimia 98.83 ya wananchi waliopiga kura wameamua kujitenga na kuwa na taifa lao.

“ Timu yetu inapenda kuhitimisha kwamba matokeo ya kura hiyo ya maoni yameonyesha matakwa ya wananchi wa Sudan ya Kusini, mchakato mzima wa upigaji wa kura ulikuwa wa uhuru, haki na wa kuaminika”. Anasema Mkapa.

Akasema kukamilika kwa zoezi hilo ni moja ya hatua muhimu sana kuelekea upatikanaji wa amani ya kudumu.

Baada ya matokeo ya mwisho ya kura hiyo kutangazwa na baada ya pande zote mbili kuridhia na kuyakubali, huku Jumuia ya Kimataifa ikiyaridhia, Taifa huru la Sudan ya Kusini litakaribishwa rasmi katika Jumuia ya Kimataifa Julai 9 mwaka huu.

Mkapa ambaye timu yake ilitembelea Sudan ya Kusini mara tano katika kipindi cha kuelekea upigaji wa kura hiyo. Amelieleza Baraza hilo kwamba, katika kutathimini mchakato huo wote, timu yake ilizingatia misingi yote iliyoainishwa katika Sheria ya Kura ya Maoni ya Sudan ya Kusini. Na kwamba Timu imejiridhisha kuwa zoezi lilifanyika katika mazingira ya uwazi wa hali ya juu.

Maonyesho ya Harusi kufanyika Dar



Maandalizi ya maonyesho ya pili ya Harusi Tanzania ‘Harusi Trade Fair 2011’, yanayotarajiwa kuanza tarehe 1- 3 mwezi ujao katika ukumbi wa Diamond Jubilee yanaendelea vizuri , huku yakiwa yanajumuisha wataalamu waliobobea katika nyanja zote zinazohusiana na suala zima la Harusi.

Muaandaaji na msimamizi wa maonyesho haya makubwa ya Harusi Tanzania , Mustafa Hassanali amesema kuwa “maonyesho ya mwaka huu yatakuwa makubwa, mazuri na yenye kuvutia zaidi ya mwaka uliyopita, na tunatazamia kuyafanya yawe maonyesho makubwa zaidi kwa ukanda huu kwa miaka ijayo”

Nukuu zinasema kuwa, maonyesho ya mwaka huu tayari yameshawavutia zaidi ya washiriki 32 , wakiwemo washiriki wa maonyesho yaliyopita na wapya.

Maonyesho ya Harusi ya mwaka 2011, ni maonyesho ambayo uboreshaji wake umevuka kutoka siku mbili za maonyesho hadi siku tatu kwa mwaka huu, huku likiongezewa na kujumuisha vionjo vingi zaidi.

“Harusi ni tukio zuri, ambalo hutokea mara moja tu, huku likiunganisha familia na jamii pamoja, hivyo nia yetu ni kuwapa maharusi mahitaji yao yoote muhimu kwa pamoja na kwa wakati mmoja, na maonyesho haya ndio sehemu muafaka kwa hilo ” alisema Mustafa Hassanali.

Maonyesho haya ya Harusi ambayo hufanyika kila mwaka, huwaleta pamoja wahusika wote wa mambo ya Harusi katika kujenga na kutengeneza mtandao wa kimafanikio baina yao, na ndio maana maonyesho haya yamekuwa ni ya kwanza na ya aina yake Tanzania, ambapo kwa mwaka huu yatapambwa na vitu kama keki, maua, wapiga picha, magauni ya Harusi, bila kusahau mengi na yenye ubunifu katika Harusi.

Gabriel Makupa wa ‘GRM Production’, ambae ni mmoja wa washiriki wa mwaka huu wa maonyesho haya alisema kuwa, wamekuwa na wakati mzuri kibiashara, hali iliyosababishwa na ushiriki wao katika maonyesho haya kwa mwaka uliyopita.

“tumekuwa na wakati mzuri kibiashara, hii imetusaidia kujenga mtandao mzuri kibiashara, tulitangaza huduma zetu vilivyo, na hii ndo sababu ya sisi kushiriki tena mwaka huu” alisema Gabriel wa GRM, kampuni inayojihusisha na upigaji picha katika maharusi.

“makampuni yajitokeze kutangaza huduma zao mwaka huu katika maonyesho haya, ni nafasi nzuri, kwani tumeshapata makampuni 32 mpaka sasa yatakayoshiriki mwaka huu, idadi ambayo inaongezeka kila siku, “ alisema Mustafa Hassanali.

Mmoja wa washiriki wa mwaka huu wa maonyesho kutoka ‘Karibu Holiday’, kampuni inayoshughulika na maandalizi ya fungate kwa maharusi na mapumziko binafsi nchini, Bw. Susai Nathan alisema kuwa, maonyesho ya mwaka huu ni njia mbadala ya kutangaza huduma zao mpya zenye ubora maalum kwa fungate, mahususi kwa maharusi au watakaofunga ndoa katika miezi hii mitatu ijayo.

Haya ni maonyesho ya siku tatu ambayo yana mengi, na si yakukosa kushiriki ama kuhudhuria kwa maharusi, familia, na wale wote wanaohusika na kamati za Harusi, ili kujionea na kujua mengi yahusuyo Harusi na mahitaji yake.


Monday, February 07, 2011

Usafiri wa mitaa ya Mbambabay




Hii ni sehemu ya barabara ya Mbinga - Mbambabay kama ilivyoshuhudiwa na mdau wetu aliyepita maeneo hayo juzi.

Sunday, February 06, 2011

JK aunda tume matatizo ya vyuo vikuu


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEUZI WA TUME YA KUTAYARISHA MFUMO MPYA WA KUGHARIMIA/KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

Katika hotuba yake ya kukizindua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma Novemba 25, 2010, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliahidi mambo makubwa mawili kama ifuatavyo, nanukuu:

Moja: “Kuhusu mikopo ya elimu ya juu napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni. Serikali iliongeza fedha za mikopo kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/06 hadi kuwa shilingi 237 bilioni mwaka 2010/11 na wanafunzi waliopatiwa mikopo hiyo wameongezeka kutoka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi; na

Pili: Pia tutautazama upya mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ikiwepo na utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuuboresha na kuleta ufanisi zaidi. Mawazo ya wadau wakiwemo wamiliki wa vyuo, wahadhiri na wanafunzi, yatasaidia sana”.

Ili kutekeleza ahadi hiyo ya Pili, Mheshimiwa Rais ameteua Tume ya wataalam 11 kufanya mapitio ya mfumo na uendeshaji wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mikopo hiyo. Tume inatakiwa kufanyakazi kwa siku 60, kuanzia tarehe 14 Februari 2011 na kuwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi tarehe 15 Aprili 2011.

Tume hiyo itaongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Makenya Abraham Maboko.

Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Bw. Masoud Mohamed Haji, Ofisa Uhusiano wa Kimataifa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Zanzibar; na Dkt. Eliawony Kristosia Meena, Mhadhiri Mwandamizi (Elimu), Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha.

Wengine ni Bw. Daniel Paul Magwiza, Naibu Katibu, Tume ya Vyuo Vikuu; Bibi Sarah K. Baharamoka, Mkurugenzi Msaidizi (Uandishi Sheria), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Profesa Penina M. Mlama, Mkurugenzi Mtendaji wa Tawi la Tanzania la Taasisi inayopigania Elimu kwa Wanawake (Campign for Female Education Tanzania Chapter).

Katika Tume hiyo pia yumo Bw. Deo Mbasa Daudi, Ofisa Taaluma, Chuo cha Usimamizi wa Fedha, ambaye ni Rais Mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-DARUSO (2007/2008), na Katibu Mkuu Mstaafu wa DARUSO (2006/2007); Bw. Kassim Almasi Umba, Makamu Mkuu wa Chuo (Utawala na Fedha), Chuo Kikuu cha Kiislamu, Morogoro; Bw. Anderson Y. Mlambwa, Mkurugenzi wa Mikopo, Benki ya CRDB; Prof. Wilbert Abel, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Bibi Rosemary Rulabuka, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Tume itateua Makamu Mwenyekiti kutoka miongoni mwa Wajumbe. Sekretarieti ya Tume hiyo itatokana na Wajumbe kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Ikulu.

Hadidu za Rejea za Tume hiyo ni pamoja na kuchambua kwa kina Sheria Na. 9 ya mwaka 2004, iliyounda Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, na Kanuni zake na kubainisha vifungu vinavyohitaji marekebisho kulingana na hali halisi ya utoaji mkopo na kuangalia upya vigezo na sifa zinazozingatiwa katika utoaji wa Mkopo endapo vinakidhi haja na mahitaji halisi ya waombaji na taifa kulingana na makusudio ya kuundwa kwa Bodi ya Mikopo.

Nyingine ni kuangalia kwa kina muundo wa Bodi na ufanisi wake katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na kutoa mapendekezo na kuchunguza kiini cha malalamiko na mahusiano yasiyoridhisha kati ya Bodi na Wanafunzi, Bodi na Taasisi ya Elimu ya Juu na kati ya Bodi na Wizara ya Elimu na kutoa mapendekezo ya namna ya kurejesha mahusiano mazuri.

Hadidu nyingine za rejea ni kuchambua mfumo mzima wa namna ya kubaini wanafunzi wanaohitaji mikopo (Means Testing) ili kuibua mapungufu yake na kupendekeza taratibu za kuuboresha au kuwa na mfumo mbadala na kuangalia mambo yanayosababisha mifuko mingine kama vile “Resource Endowment Fund” wa Maliasili unafanikiwa na Nchi nyingine zenye mazingira kama ya Tanzania zinavyofanikiwa kugharimia Elimu ya Juu kwa mfumo wa Mikopo.

Nyingine ni kutoa ushauri na mapendekezo yatakayowezesha Mkopo utolewe kwa wanafunzi wengi wahitaji wa Elimu ya Juu ili kuondoa lawama zilizopo na kushughulikia mambo mengine yoyote yatakayoweza kuboresha mfumo huo kwa kadri inavyoonekana inafaa.

Ni matumaini ya Serikali kwamba baada ya Tume hiyo kukamilisha kazi yake, itatoa ushauri utakaosaidia kujibu malalamiko mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Mizengo P. Pinda (Mb)

WAZIRI MKUU

6 Februari 2011

Palestina wawasili kukipiga na Stars





Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Palestina wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu JK Nyerere kabla ya kwenda katika Hoteli ya Transoma jijini Dar es Salaam.

Matembezi ya Mshikamano


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mkewe Tunu wakiwapungia wananchi katika matembezi ya mshikamano ya kuadhimisha miaka 34 ya CCM Mkoani Iringa yaliyofanyiak kimkoa kwenye Kijiji cha Tungamalenga wilayani Iringa Mjini jana. Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Mbunge wa Ismani, William Lukuvi na Kushoto ni Kamu Mkuu wa mkoa wa Iringa Issa Machibya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

MAKATIBU WAKUU WAKAGUA AICC MAANDALIZI YA MWISHO MKUTANO WA IPU, ARUSHA

Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali pamoja na Kamati ya Wataalamu ya Maandalizi ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), wamefan...