Wizara ya Afya imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 1.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za afya nchini, kuimarisha hospitali na taasisi zake pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta hiyo.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa amesema wizara hiyo inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,800,262,058,000.00.
Waziri Mchengerwa amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 652,236,871,000.00 sawa na asilimia 36 ya bajeti yote zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku Shilingi 1,148,025,187,000.00 sawa na asilimia 64 zikielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameeleza kuwa katika fedha za matumizi ya kawaida, kiasi cha Shilingi 516,323,356,000.00 kimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Wizara, hospitali pamoja na taasisi zilizo chini yake, huku Shilingi 135,913,515,000.00 zikitengewa matumizi mengineyo.
Kwa upande wa fedha za maendeleo, Waziri huyo amesema Shilingi 789,458,609,000.00 ni fedha za ndani, wakati Shilingi 358,566,578,000.00 ni fedha kutoka vyanzo vya nje kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya afya nchini.
Aidha, Wizara ya Afya imekadiria kukusanya maduhuli ya Shilingi 747,200,091,299.81 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kupitia Wizara, taasisi pamoja na hospitali zake.
Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, kati ya fedha hizo, Shilingi 76,195,850,735.53 zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vya ndani vya Makao Makuu ya Wizara, Shilingi 165,804,149,264.47 kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa, huku zaidi ya Shilingi bilioni 505 zikitarajiwa kukusanywa kutoka taasisi, Hospitali ya Taifa, hospitali maalum pamoja na hospitali za kanda.
Waziri huyo amesema fedha zinazoombwa zitawezesha Wizara ya Afya kuendelea kuboresha huduma za afya nchini, kuimarisha miundombinu ya matibabu, kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

No comments:
Post a Comment