JK aongoza mazishi ya Penza

Mzee Athumani Janguo akimzika rafiki yake mzee Penza leo jioni
Mwenyekiti wa mkoa wa Shinyanga Khamisi Mgejja akimzika bwana Penza

Nape Nnauye akishiriki katika Mazishi ya Penza
Rais Kikwete akiweka mchanga katika kaburi la marehemu Juma Penza jioni hii
Waombolezaji wakiwasili kwenye makaburi ya kisutu kwaajili ya maziko ya mkongwe huyo
Rais Kikwete akiwa na wajukuu wa marehemu Juma Penda kwenye makaburi ya Kisutu jioni hii

********************

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jioni ya leo, Alhamisi, Oktoba 13, 2011 ameungana na waombolezaji kumzika mwanahabari mkongwe, Ndugu Juma Fugame Penza katika makaburi ya Kisutu, mjini Dar es Salaam.

Ndugu Juma Penza alifariki dunia usiku wa kuamkia leo kwenye Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 63.

Marehemu Penza ambaye amekuwa katika tasnia ya habari kwa karibu miongo minne iliyopita na miongoni mwa walioshiriki mazishi yake katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam ni pamoja na viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alichokifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 20.

Katika salamu za rambirambi ambazo Mheshimiwa Rais Kikwete amempelekea Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Wilson Mukama na kupitia kwake kwa familia na ndugu wa marehemu, Mheshimiwa Rais amemwelezea Hayati Penza kama mwandishi wa habari aliyefanya kazi zake kwa weledi na uzalendo akiongozwa na misingi imara ya taaluma yake na uzalendo kwa nchi yake.

“Nilimfahamu binafsi Ndugu Penza wakati tulipofanya kazi pamoja katika Chama cha Mapinduzi. Hakuna shaka kuwa Marehemu Penza aliitumia taaluma yake ipasavyo, akiongozwa na weledi wa kazi hiyo na uzalendo kwa nchi yake. Kamwe, hakupata kutumia ujuzi wa kazi yake kugawa wananchi kwa misingi ya aina yoyote ile.”

Katika maisha yake, marehemu Juma Fugame alishikilia nafasi za uandamizi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na kuwa Kaimu Mhariri wa Mazageti ya Serikali ya Daily na Sunday News, Kaimu Mkuu wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) kabla ya kujiunga na utumishi wa CCM.

Katika utumishi huo, Marehemu Penza alipata kuwa Mwandishi wa Habari wa Katibu Mkuu wa CCM, Mzee Rashid Mfaume Kawawa ambaye pia ni marehemu, Mwandishi wa Habari wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee John Malecela, Mkurugenzi wa Redio Uhuru na Afisa Mwandamizi wa masuala ya habari na vyombo vya habari katika makao makuu ya Chama.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,DAR ES SALAAM.

13 Oktoba, 2011



Comments