Shirikisho sawa tunalikubali, lakini siyo sasa

KAMA Mtanzania wa kawaida mlalahoi, mvuja jasho mpambanaji, mtaabikaji, mhangaikaji na majina mengine yoyote utakayopenda kuniita, ni juu yako na wala sijali, lakini leo hebu tukae kitako na tujadili hili suala linalotuhusu sote na linayoyagusa maisha yetu ya kila siku, hili jambo lililolipuka mithili ya moto wa mwituni, yaani la kuanzishwa kwa Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.

Kwanza, kama muungwana yeyote yule hebu nichukue fursa hii kupongeza mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kuweza kuainishwa vyema kwa mkataba wa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayotuelekeza katika Shirikisho la Afrika Mashariki ambao umeweka wazi masuala muhimu.

Si jambo rahisi sana kuweza kufikia hatua kama hii hasa katika mazingira yenye utofauti kama ya kwetu na yaliyopata kusigana wakati fulani hasa miaka ya 1970, baada ya kuwa tumeparaganyishwa na Mkoloni katika miaka ya 1885.

Tumesikia na kwa kweli ndivyo hali halisi ilivyo ushirikiano ni kitu muhimu sana katika kujiletea maendeleo ya kweli na ya kudumu kuliko utengano, lakini ushirikiano lazima uzingatie maslahi ya kila mmoja miongoni mwetu.

Inawezekana kabisa kuwa tuna mkataba mzuri sana ambao umezingatia hatua muhimu, lakini huko mbeleni usije kutusaidia kama mambo yenyewe ndio haya!

Tunaelezwa kwa mfano, kuwa ushirikiano huu unaanzishwa ili kuweza kuimarisha na kudhibiti miundombinu ya kiviwanda, kibiashara, usafiri na usafirishaji, kiutamaduni, kijamii, kisiasa na mahusiano mengine ya mataifa wanachama.

Zipo hatua muhimu za kuzingatia katika kuanzisha ushirikiano huu, nazo ni kama kuanzisha ushuru wa pamoja wa forodha ambao umeshaanza, soko la pamoja (lipo katika hatua mbalimbali), sarafu ya pamoja (bado) na hatimaye Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2013.

Lakini, ninavyokumbuka mkataba wa ushirikiano ulisainiwa Novemba 30, 1999; na kuanza kutekelezwa Julai 2000, na kisha baada ya hapo ukasainiwa mkataba wa makubaliano ya kuanzisha ushuru wa pamoja wa forodha, Machi 2004; na kuridhiwa Desemba 2004; umeanza kutumika Januari 2005.

Makubaliano ya kusaini kuwapo kwa sarafu moja bado kukubalika; Na kila hatua angalau inahitaji mjadala na maridhiano ya kina baina ya nchi na nchi na kwa maana hiyo kama hatua hii ya sarafu ya pamoja bado haijaridhiwa bila shaka hata Shirikisho linalosukumwa kwa kasi ya ajabu, bado sana kufikia hatua yake, ingawa inapendekezwa kamati iharakishe ili Shirikisho lifikiwe mwaka 2010.

Hii ina maana mpaka kufikia hatua ya mwisho Afrika Mashariki inatakiwa kupita hatua kuu tano hadi sasa imepiga hatua mbili tu bado mbili kufikia ya mwisho.

Lakini, hivi sasa tumeruka na kuingia hatua ya mwisho kabisa ya Shirikisho ambapo maoni yanakusanywa kwa nchi wanachama, sijui ili iweje halafu na huo mustakabali wake utakuwaje, hakuna fursa ya kutosha iliyotolewa kwa wananchi (hata kama wanakusanya maoni yao) hadi sasa na hakuna mpaka sasa mwelekeo unaoonyesha hiyo serikali ya shirikisho itaendeshwa vipi.

Katika hili la kutafuta maoni inawezekana kukawa na tatizo moja kwamba wananchi hawafahamu mkataba ukoje zipi faida na zipi hasara kwa maana hiyo wakatoa uamuzi mbovu, tuombe Mungu uamuzi huo uisaidie Tanzania usipokuwa wa manufaa tutajuta.

Yapo maswali mengi tunapaswa kujiuliza mathalani: Hivi, uchaguzi huo wa shirikisho utaendeshwaje? Nini, itakuwa vigezo vya kugombea nafasi za kisiasa? Na katika hali ya sasa, ambapo kuna tofauti za dhahiri za kiitikadi ndani ya nchi husika , Je siasa za kishirikisho zitaendeshwaje?

Kwa maana hiyo, kwa maoni yangu naona ni mapema sana kujiingiza katika hatua za juu kutaka kushirikiana kisiasa wakati masuala ya msingi hayajashughulikiwa, tujijenge kwanza na tujiimarishe kwa kasi ile ile, ili kusudi wenzetu wasije kuturudisha nyuma kama ilivyokuwa mwaka 1977.

Comments

Alex Mwalyoyo said…
Pole sana kwa mihangaiko Bw Charahani. Nimesoma makala hii inayohusu shirikisho la Afrika Mashariki, katika mtandao, pamoja na maoni ya Wasomi wa Tanzania kuhusu wasiwasi wao na jumuia hii. Mimi, kama walivyo Watanzania wengine, bado nina wasiwasi sna na shirikisho hili. Nasema hivyo kwa sababu mpaka sasa bado tuna wakimbizi wengi sana wa Rwanda na Burundi, sasa basi iwapo tunawaruhusu kirahisi namna hio kuingia katika jumuia hii basi tunawarahisishia suala la kuwatunza watu hao hapa kwetu. Siamini kama viongozi wetu walikaa na Watanzania na kuwaeleza kinagaubaga kuhusu suala hili, pamoja na faida na hasara zake. Naona kama walikurupuka tu kuwaingiza wananchi wa nchi tajwa. Naomba sisi wana blogu tuwe na mjadala wa kina kuhusu suala hili, hasa nchi hizi mbili za mwisho kuingizwa katika jumuia hii. Hatujatatua suala la wakimbizi bado, sasa kwa nini tunawaingiza kichwa kichwa? Tuna mzigo mkubwa wa kubeba kwa ajili ya nchi yetu, sasa basi kwa nini tunajitwisha mzigo mwingine zaidi? Jadili...