Mkapa aula Zimbabwe, Ulaya

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa. (Picha ilipigwa na Suleiman Kimaro wa Wizara ya Mambo ya Nje)

NEW YORK, UN

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan amejitoa katika juhudi za upatanishi wa kutatua mgogoro nchini Zimbabwe na nafasi yake imechukuliwa na Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Uteuzi wa Mkapa ambaye alikuwa rais wa serikali ya awamu ya tatu ya Tanzania, kuchukua nafasi hiyo ya Annan, umefanywa baada ya kupata baraka za Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Kutokana na uamuzi huo, Annan sasa hatafanya ziara ya kuitembelea Zimbabwe kama ilivyokuwa imeripotiwa awali.

Serikali za Afrika Kusini na Uingereza hivi karibuni zilieleza kuwa Annan angeweza kutoa mchango mkubwa katika kumaliza mgogoro za wa kiuchumi na na kisiasa unaoikabili Zimbabwe.

Annan alikutana na Rais Mugabe mjini Banjul, Gambia wiki iliyopita wakati wa mkutano wa wakuu wa serikali na nchi wanachama wa Muungano wa Afrika (AU) na kusema kuwa Mugabe alimweleza kuwa Mkapa ameteuliwa kuwa mpatanishi.

"Sote tumekubali kuwa Mkapa apewe nafasi na sehemu ya kufanyia kazi hii," Annan ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP.

Alipoulizwa iwapo bado ana mipango ya kufanya ziara nchini Zimbabwe, Annan alijibu kwa kusema: "Haiwezekani kuwepo wapatanishi wawili."

Mugabe alimbana Annan kuitembelea Zimbabwe mwaka jana, baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat), Anna Tibaijuka kuwasilisha ripoti iliyokosoa operesheni ya Zimbabwe ya kubomoa nyumba na kuwaondoa wafanyabishara waliodaiwa kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa katika miji mbalimbali, ukiwamo Harare.

Mei mwaka huu, Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, alisema UN ilikuwa na mchango muhimu katika kutatua mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini Zimbabwe, na kwamba ziara iliyokuwa imependekezwa kufanywa na Annan nchini Zimbabwe ingesaidia kuboresha uhusiano kati ya Zimbabwe na nchi za magharibi.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, alisema anaamini kuwa kuhusishwa kwa Annan kungesaidia kupatikana kwa mafanikio kwa wananchi wa Zimbabwe.

Afrika Kusini ilikwisha kueleza kuwa inaguswa sana na athari zilizokuwa zinaikabili Zimbabwe ambayo ni jirani yake.

Zimbabwe hivi sasa inakabiliwa na athari kubwa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei ambao ni zaidi ya asilimia 1,000 kwa mwaka na wananchi wengi wa nchi hiyo wameikimbilia nje, hasa Afrika Kusini.

Nchi nyingi za magharibi zinadai kuwa matatizo ya kiuchumi ya Zimbabwe yamesababishwa na sera mbovu za Mugabe. Hata hivyo, kwa upande wake, Mugabe anazishutumu nchi hizo kuwa zinahujumu uchumi wa nchi yake kwa lengo la kumwondoa madarakani kutokana na mpango wake wa mageuzi ya ardhi.

Comments

Jeff Msangi said…
Upatanishi huu ni kati ya nani na nani?Raia na raisi wao au mataifa ya magharibi dhidi ya Mugabe?
mloyi said…
Waarabu wa pemba wajuana kwa vilemba. Mkapa hajulikani ni wa msimamo gani, akiwa raisi wana-ulaya walimpenda sana kiasi cha kutia mashaka imani yao kwake, bado hatujui aliwapa/aliwafanyia nini? lakini kuna siku nilimsikia akiongea kwa kumuunga mkono Mugabe! tunategemea maamuzi yake yatakuwa pasipo kuingiliwa na nguvu fulani.
Jeff upatanishi ule tunaoambiwa wa mkapa ni kati ya Rais Mugabe na mataifa ya magharibi si wanajua wameshahenya vya kutosha na mzee mwanamapinduzi kang'ang'ana hataki mchezo natamani tungekuwa na mtu mwenye msimamo kama yeye ukiachilia mbali mabo yake machache machache mabaya.

Mloyi ni kweli unavyosema Mkapa na Mugabe mambo yao ni yale yale lakini msimamo wake unaeleweka kwamba yeye ni extenalist anaamini mengi mazuri lazima yaanzie nje na siyo ndani ndo maana alikuwa akijitahidi kutoa dharau katika kili kilicho cha mbongo.