Wednesday, March 22, 2006

Tunauondoa umaskini kwa kutumia?

UMASKINI kama ulivyo au lilivyo neno lenyewe ni maarufu sana katika mataifa yetu haya, hasa yanayoendelea. Kila kukicha kuna suala moja au mawili au hata zaidi yataugusia au kuuzungumzia au kuihusu jamii. Ni wachache au hakuna kabisa kati yetu ambaye ataepa kuguswa na umaskini.

Wengine wanadiriki kusema umaskini hauwezi kuisha, eti kwa sababu utajiri upo, hawa wanatumia 'lojiki' au mantiki za falsafa za kijamii. Inawezekana wakawa na ukweli ndani yake. Tofauti na hao, lipo kundi jingine la wenye mwelekeo wa wastani, hao hudhani umaskini unaweza ukaondoka na jamii ikaishi maisha inayotaka! Sijui.

Katika somasoma yangu, nimekumbana na kauli mojawapo iliyopo katika kitabu kimoja cha kuvutia chenye jina "The Undercover Economist" kilichoandikwa na Tim Harford inayohusu nchi ya China, ambayo nafikiria Watanzania wenzangu wanapaswa kuipata. Taarifa hii inasema hivi: "China imefanikiwa kuwaondoa mamilioni ya watu wake kutoka katika wimbi la umaskini kila mwezi." Kumbuka kwamba nchi hii ina watu zaidi ya bilioni moja.

Kauli hii inaweza kuonekana nyepesi, lakini imebeba ujumbe mzito. Sijaangalia bado katika takwimu, lakini nachoweza kukigundua katika kauli hii inaonekana kuna mafanikio. Kama hii ndivyo ilivyo, basi ni taarifa ambayo inatia faraja na kila mmoja miongoni mwetu anapaswa kuipata.

Watu katika medani za siasa wanapiga kelele katika kiwango wanachoweza kila siku na kuainisha programu na sera mbalimbali za namna ya kuupunguza umaskini, lakini wanakuwa wanaonyesha shauku kidogo sana katika mipango ya namna umasikini ulivyopunguzwa, iwe hapa kwetu au kwingineko.

Wanapanga kila aina ya mkakati, ziwe semina, sijui warsha na halafu mikakati ambayo inakuja na majina ya ajabu ajabu, nadhani majina yamekwisha! La hivi karibuni kabisa lafahamika kama MKUKUTA, Mkurabita na kadhalika. 'Mikukuta' hii haiondoi umaskini kama inavyokusudiwa badala yake yenyewe inatumia pesa na halafu mwisho wa siku maskini anabakia palepale.

Sisemi kuwa haifanyi kitu kabisa. La hasha, inapunguza umaskini, lakini kwa kasi ndogo sana, tena kwa makundi yasiyokusudiwa. Tunataka watu wetu maskini halisi waondokane na umaskini!

Msomaji wangu, nadhani unaweza kuotea kiasi ambacho watu wa magharibi wanavyochukizwa na mafanikio haya ya China. Mataifa hayo tajiri hupata shauku sana wakati mataifa mengine hasa ya kimaskini yanapokumbwa na majanga na maelfu kwa mamilioni ya watu wakiwa wanakufa ama kwa njaa au maafa. Wao, hufurahia zaidi kama mataifa hayo yana almasi, dhahabu, mafuta na maliasili zinginezo.

Wale miongoni mwetu wasiokuwa na mtazamo huo wa kimagharibi habari hii ni yenye kutia shauku na kuvutia kwa China kuweza kujitoa katika umaskini.

Awali ya yote kwa tuanze kwa kujiuliza, hivi ina maana gani kwa "China kuwainua watu milioni moja kutoka katika wimbi la umaskini kwa mwezi"? Ni wapi serikali ya China inapata fedha hizo kutekeleza jukumu hilo muhimu na nyeti? Bila shaka watu pekee serikali inayoweza kuwatoza kodi ni watu wa China pekee.

Kiuhakika kabisa nchi haiwezi kujinyanyua yenyewe kwa kiasi kikubwa namna hiyo kwa kutumia uwezo wake wa ndani pekee au hata kwa kutumia msaada wa nje hauwezi kutosha kuwaondoa masikini milioni moja kwa mwezi. Kama serikali ya China haijafanya hivyo, nani ameweza kufanya hivyo?

Hawaondolewi katika umaskini eti kwa kwa ukarimu wa mtu fulani. Kitu pekee kinachoweza kutibu umaskini ni utajiri. Wachina wameupata utajiri kwa njia ya kikale kidogo: Waliutengeneza. Baada ya kifo cha Mao Tsetung, udhibiti wa serikali katika biashara ukaanza kupungua taratibu --kwanza kwa kufanya majaribio katika maeneo waliochagua wenyewe na viwanda maalumu.

Halafu baada ya viwanda hivyo kupata mafanikio ya haraka, serikali ikaendelea hatua kwa hatua lakini kwa umakini mkubwa katika maeneo mbalimbali na maeneo yote hayo yakaibuka na matokeo yaleyale.

Umasikini hauwezi kuondoka kwa kuutumia kwa kusema sana kisha wachache wakaingia katika kumbi za mikutano na kujifaidisha kwa posho nono huku kukiwa hakuna utekelezaji. Unaondoka kama kuna utashi, nia na mipango inayotekelezeka. Jambo la maana ni kama hivi China ilivyofanya.

12 comments:

boniphace said...

Karibu Charahani, nitapita kusoma maandishi haya baadaye maana hapa nimeamkia vikaratasi fulani. Kubwa ni kukushukuru kutumia haki yako ya kimsingi kufungua Gazeti Tando. Hapa unaungana na wananchi lukuki wanaotumia haki zao za msingi za kujieleza. Karibu huku na kula chakula cha fikra za wenzako kama ambavyo utatushibisha huko home.

mzee wa mshitu said...

Ahsante sana nami nimekaribia katika kisima hiki cha fikra nimepitapita na kucheki chakula kibao cha kushibisha nadhani nitavimbiwa.

Jeff Msangi said...

Charahani,
Nianze kwa kukukaribisha.Karibu sana.Katika siku za hivi karibuni nimekuwa nikijadili sana masuala haya.Katika mijadala mingi nimepinga dhana ya kwamba nchi kama Tanzania ni masikini au watu wake ni masikini.Napinga dhana hii kwa kutumia maana halisi ya neno umasikini/masikini.Nani ni masikini?Jibu langu ni kwamba masikini ni asiye na kitu.Aliyenacho bila kujua jinsi ya kukitumia sidhani kama ni masikini.Tanzania/watanzania tuna utajiri wa ajabu wa rasilimali.Tunachotakiwa kufanya ni kukumbushana/kuwezeshana fikra zetu kwanza.Ukiambiwa kila kukicha kwamba wewe ni masikini utaamini.Ni kama vile kuambiwa kwamba "unaonekana unaumwa" asubuhi na mapema unapoingia ofisini.Nakuhakikishia kabla siku haijaisha utakuwa unaumwa kweli.Hivyo tuanze kwa kupambana na dhana hizi zinazotoka kwa wenzetu wa magharibi zaidi.Tuwezeshane kujiletea utajiri ambao umetuzunguka!Nadhani China hawajawahi kuamini dhana hizi!

Egidio Ndabagoye said...

Karibu sana kaka pamoja na kwamnba nilikuwa sipo kwa siku kidogo mtandaoni.Nashukuru kupata mtu kama wewe katika ulimwemgu huu blogu.

Karibu sana!

Rama Msangi said...

Kwa leo nimefika hapa kwa ajili ya kukukaribisha tu ndugu yangu mzee wa Mshitu(ni), karibu saaaana

mzee wa mshitu said...

Wazee nashukuruni sana kwa kunikaribisha katika ulimwengu huu huru wa kumwaga na kuelezea fikra ama kwa hakika katika kipindi cha siku mbili hizi nimeingia katika mashubaka (book shelf) za magazeti tando yenu kwa hakika nimepata kiu ya kuendelea kuchota fikra mpya.

Ndugu yangu Msangi nakusoma kila Jumapili kule Tanzania Daima na huwezi kuamini gazeti lile kwa kiasi kikubwa linanunuliwa sababu ya makala zako.

Hapa kwetu watu tunavutika sana na kufahamu mambo ya huko na kisha tunaanza kusafiri kwa ndoto hadi huko.

Ndugu yangu boni wewe sina la kusema maana mengi huwa tunachat katika email kuanzia ulipoondoka kwenda huko ughaibuni na hata wakati ule nilipokuwa jijini New York kwa hakika sina cha kusema sababu nikisema zaidi ntakuwa nasema sijui nini.

Bwana Egidio pia thanx very much hii ni baaab kubwa maana sasa naingia kichaa maana hiki kisima cha maarifa mlichokiingia muda mrefu kwa hakika mmevuna mengi ahsanteni sana.

Halafu ndugu yangu Ramadhani Msangi hivi ulifikiria nini mpaka blogu yako ikabeba mada hatari namna hiyo( Im joking) yasije yakawa yale ya vikaragosi maana kuna watu wana imani za ajabu.

Ahsanteni sana!

Frank said...

karibu baba nitakuwa nakutembelea mara kwa mara,ila kwa sasa nami niko bize kufuatila na kutengeneza makala ya jumapili ya simba na yanga.big up sana

Fikrathabiti said...

Karibu sana mwanamapinduzi.Mimi nipo zanzibar ila makazi yangu ya kudumu ni Dar es salaam
Huu ni uwanja wa kuchambua chuya na mchele.Tulio na njaaya habari kama walivyosema wenzangu naamini sasa tutashiba kutokana na rehema zako za kihabari.

Ndesanjo Macha said...

Charahani, karibu mwanakwetu. Hujui jinsi tunavyoingiwa na furaha mnavyotuunga mkono na kuamua kujenga kurasa binafsi za majadiliano, elimu, na maarifa. Karibu sana. Tupo wote.

Innocent Kasyate said...

Charahani nakukaribisha sana.Ila nikuombe usome katika nchi ya jirani ya Tanzania kuna misukosuko sana. Ukinisoma utajua nini kinatukia huku Uganda.

Reggy's said...

Charahani karibu sana. Nakuahidi kitu kimoja, tu, nitakusoma sana ikiwa utakuwa unaweka mambo mapya mara kwa mara katika gazeti tando lako. Hili usilione kama lako bali la wasomaji dunia nzima. ukiingia hapa hakikisha hau-bip, bali unapiga moja kwa moja.

mwandani said...

Naam nami nimesoma na kuwaza huu ujumbe.Karibu sana.
Naungana mkono na Jeff, nia, ya kuendelea kwanza. Maendeleo yatafuata. Nia sio mikutano.