Monday, March 27, 2006

Vibaka wakizidi tusije kamatana mashati

SIKU zote kitu maamuzi ni kitu kinatakiwa kuchukuliwa kwa tahadhari na mazingatia makubwa.

Maamuzi yanaweza kuharibu, kubadilisha mambo na au kuboresha, lakini pia yanaweza kuwa chanzo cha matatizo mengine makubwa ambayo huwa magumu sana kuyazima.

Yanapochukuliwa maamuzi siku zote huwa zipo pande zinafaidika na zingine zinataabika, lakini cha msingi kinachoangaliwa mara zote hizo ni 'rationality'

Yapo mengi yanaweza kuzungumzwa kuhusu 'rationality' ambayo kwa upande mmoja inaweza ikawa sawa sawa, lakini upande mwingine ikawa 'wrong' mathalani mtu akiiba chakula sababu ana njaa upande mmoja sawa upande mwingine noomaa!

Alhamisi iliyopita wachimba kokoto wapatao 3,021 waliokuwa wakiendesha shughuli zao eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam, waliamriwa kuondoka katika eneo hilo mara moja na leseni za wengine kufutwa.

Agizo la kuwaondoa wachimbaji hao, 21 wakiwa na leseni 3,000 wakiwa ni wadogowadogo, lilitolewa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya kutembelea eneo hilo kujionea uharibifu wa mazingira uliofanyika hapo.

Lowassa alichukua hatua hiyo baada ya kushuhudia uharibu wa kutisha wa mazingira ambao unatishia kubomoka kwa barabara ya Bagamoyo, aliagiza leseni za madini walizopewa wachimbaji wa kokoto wanaoendesha biashara hiyo katika machimbo ya Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam, zifutwe mara moja ili kunusuru mazingira na barabara kuu.

Kama hilo halitoshi maelfu ya wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na majiji mengine waliondolewa kwa operesheni kamambe kutokana na kufanya biashara katika maeneo ambayo hayakupangwa kwa matumizi hayo.

Sambamba na hayo kundi jingine kubwa la waliokuwa wakifaidika kutokana na biashara ya mkaa na upasuaji na usafirishaji magogo nao lilionja chungu baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii kupiga marufuku biashara hiyo hadi hapo baadaye yatakapotolewa maelezo ya kina.

Balaa kubwa zaidi ni lile lililosababishwa na upungufu wa nishati ya umeme iliyosababisha mgao wa umeme ambayo kwa maana nyingine ni kwamba wale wengine waliokuwa wakifaidika na shughuli ndodondogo za umeme sasa ndiyo basi tena wanashinda njaa!

Siwezi kusema kuwa ni sahihi kwamba serikali imechukua hatua kwasababu tatizo linakuja kwamba watu hawa walioondolewa katika maeneo waliyokuwa wakijipatia kipato watakwenda wapi.

Nafahamu kabisa kwamba zipo hatua zimependekezwa zikiwamo za kuwahamishia maeneo mengine yaliyopangiliwa, lakini pia hayo maeneo yatafahamika lini? Na muda wote huu watakaokuwa watu hawa wakisubiri watakula nini? Na je watu hawa wajitafutie kazi wapi?

Naamini kabisa kwamba Serikali zilizopita zilikuwa na ujasiri na nguvu zote za kufanya maamuzi magumu kama haya, lakini tatizo lilikuwa hali halisi ya watu wao na mazingira wanamoishi.

Ikumbukwe kwamba siyo tu wale waliotimuliwa katika maeneo husika ndiyo watakaoathirika na maamuzi machungu haya, bali ni mlolongo wa watu wengi wanaofaidika nao watakosa kupata huduma, wamo ndugu na jamaa na watoto wa familia husika, lakini pia watumiaji!

Ikumbukwe pia wakati serikali ya awamu ya kwanza ilipokuwa ikijenga vijiji vya ujamaa ilikuwa na lengo zuri, lakini lilikuja kuwa tatizo kubwa watu walipoteza maisha, vijiji vingine vilifutika, uchumi ukayumba na mambo mengi. Hivyo maombi yetu sisi ni kuwa maamuzi haya yasije kusababisha matatizo mengine. Hatua za haraka zichukuliwe.

4 comments:

boniphace said...

Charahani kumbuka kidogo kauli ya Mbunge wa Ilala wakati huo simtaji leo kwa heshima yake alipowakingia kifua wakazi wa mabondeni na baadaye Elninyo ilipotwanga akabaki domo wazi! Nadhani kushindwa kutekeleza majukumu kusifanye mikakati ipindishwe. Je wanaonufaika na rasilimali hizi ni wangapi, tazama uuzaji mkaa, kokoto nk Je hizo si ni za umma lakini wananufaika nazo wangapi? Kumbuka athari ya kukosa mvua kunakotokana na mazingira kuharibiwa kunavyotana hata wasiokata kuni na kuchimba kokoto? Wanapokosa ajira ndipo linakuja suala la kusaka hizo ajira milioni moja. Hapo ndipo utabaini umuhimu wa kupeleka watu wetu shule tena. Hapo ndipo serikali inapata picha halisi ya ugumu wa tatizo. Kuwaacha hao ni kuzima ili muda upite si unajua serikali ina react pale panapokuwa na picha ya kisiasa? Kama umeona hilo na kupata picha hii basi huu ni mwanzo mwema wa kuwazalisha hawa vijana wasio na kazi ili waungane na wapambanie mali zao zinazouzwa na wakubwa na pia kuhoji kuhusu mali zote zilizobinafsishwa na tena kutazama inakuwaje wewe Charahani unatajirika kiharakaharaka tu wakati wao wahnazidi kuwa maskini. Hapa ndipo upo mchezo aliotabiri Marx na Lenin akataka kuumba.

Jeff Msangi said...

Charahani,
Habari hii naweza kuifananisha na neno moja ambalo kwa mujibu wa kazi yangu hapa Canada nalisikia karibuni kila siku.Neno lenyewe ni "alternative".Kabla ya serikali kufanya maamuzi magumu kama haya ni lazima iwe na alternative solution kwa pande zote..mazingira na hao wachimbaji wenyewe.Pili,hivi mazingira ni Dar-es-salaam tu au Tanzania ni Dar tu?Kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanyika nchi nzima.Kama serikali inakusudia kweli kuboresha mazingira basi mkwala huu usiishie Dar peke yake.Na kama ukiishia Dar vipi kuhusu ile bahari iliyopo pale pale Ikulu inavyonuka?

mloyi said...

Charahani, nimesoma nakala zako kadhaa kwenye mwananchi, nikafikiria kwanini na wewe usiingie kwenye blogu tupate mawazo tofauti zaidi. leo nimekuta umeingia tena kwa kishindo na kikamilifu, hujachungulia kama utaweza kiwanja hiki! Karibu sana.

mzee wa mshitu said...

Kweli Makene ulichosema kina uhakika na ni makini hasa katika karne hii kwamba watoto waende shule ili kusudi masuala haya yasiwe yanatokea.

Lakini kitu kimoja kinanipa uzito Mbona hapo Marekani wana elimu kubwa na tena kubwa kupita kiasi na bado wanaharibu mazingira tena kwa kiasi kikubwa kuliko sisi, hebu cheki emmissions zinazotoka viwandani. Sisi tunaharibu kidogo sana.

halafu hata hawa watoto wakienda shule kama mimi na wewe wakirudi mtaani hawakubaliki sababu ya mfumo wa elimu uliopo unaofundisha vijana kusaka 'white collar jobs' wachache sana wanaweza kujitegemea na kujitegemea kwenyewe ndiyo kama huku kwa kujenga vibanda, kutembea na mashati mawili kutwa nzima na mengine kama hayo.

Kama alivyosema ndugu yangu Msangi kunatakiwa kuwapo altenative solution bila hivyo sisi tutataabika tutalazimika kuwa tunaondoka kurejea home saa 9 au 10 sababu baada ya hapo itakuwa hatari. Vijana watatafuta solution ya haraka.

Ndugu yangu mloyi ahsante sana nimeshaingia mtandaoni na sasa ni kubadilishana mawazo tu na kuchota busara na hekima ndani ya hiki kisima.