Mwandishi Wetu
Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umeingia rasmi kwenye familia kubwa ya vyombo vya habari baada ya kukabidhiwa hati za uanachama katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), uliofanyika Septemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam. TBN ilikuwa miongoni mwa wanachama wapya wanane (8) waliopokelewa rasmi na Baraza.
Mwenyekiti wa TBN, Ndugu Beda Msimbe, alisema hatua hiyo ni mwanzo mpya kwa wanablogu nchini kwani inaleta heshima, uhalali na ulinzi wa kitaaluma.
“Uanachama huu unatoa uhalali wa kutambulika mbele ya jamii, Serikali na wadau wengine. Sasa wanablogu tumetambulika kama chanzo cha habari kinachowajibika na tunashirikiana na vyombo vingine vya habari katika kulinda maadili ya taaluma,” alisema Msimbe.
Aliongeza kuwa wanachama wa TBN sasa wananufaika na mfumo wa ulinzi wa Baraza, hususan katika usuluhishi wa malalamiko, jambo linalowalinda kisheria na kiuchumi dhidi ya vitisho vinavyoweza kuathiri maisha na kazi zao.
Katibu Mtendaji wa MCT, Bw. Ernest Sungura, alisisitiza mshikamano na mshikikiano wa wanachama, akibainisha kuwa kauli mbiu ya mkutano, “Uhai wa Wanachama ni Nguvu na Usalama wa Taaluma ya Habari”, inapaswa kuongoza kila chombo cha habari.
“Uhai wa Baraza upo mikononi mwa wanachama. Ni wajibu wetu kushiriki kikamilifu na kulipa ada ili taasisi hii iendelee kuimarika,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Ndugu Yusuf Khamis Yusuf, alikumbusha kuwa kwa miaka 30 MCT imeendelea kujipambanua kama ngao ya uhuru na maadili ya habari nchini.
Akifungua mkutano huo, Rais Mstaafu wa Nne wa Baraza, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, aliweka msisitizo mkubwa kwa wanahabari kusimama na ukweli bila kuyumba.
“Kusimama kwenye haki ni kugumu kuliko kujipendekeza. Ni njia yenye gharama, lakini ndiyo njia ya baraka na inayompendeza Mungu,” alisema huku akiwahimiza wanahabari kuendelea kuwa nguzo ya ukweli kwa jamii.
Katika tukio hilo pia, Jaji Mihayo alizindua rasmi Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT 2025) zitakazoendeshwa kwa mfumo wa kidijitali, pamoja na kuzindua tovuti mpya ya MCT, hatua inayothibitisha dhamira ya kuimarisha weledi na udugu ndani ya tasnia ya habari.
Kwa kupokelewa kwake MCT, TBN sasa si tu sauti ya wanablogu bali pia sehemu ya familia pana ya wanahabari nchini, ikionyesha mshikamano na mshikikiano wa kweli kwa ajili ya kulinda taaluma, kuendeleza uhuru wa habari na kudumisha mshikikiano wa vyombo vya habari Tanzania.