Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na waombolezaji mara baada ya ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama, katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiongoza waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama, katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba 2025.
Picha za matukio mbalimbali wakati wa ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Marehemu Jenista Joakim Mhagama alikuwa kiongozi aliyeitanguliza mbele maslahi ya Taifa kabla ya kitu kingine chochote, akibainisha kuwa sehemu ya uimara na mafanikio ya Taifa yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na uchapakazi na uadilifu wake.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Marehemu Jenista Mhagama iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu la Dodoma, tarehe 13 Desemba 2025. Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa Bunge, viongozi wa dini pamoja na mamia ya wananchi waliokusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.
Akizungumza mbele ya waombolezaji, Rais Samia amesema Mhe. Jenista Mhagama alipendwa na kuheshimiwa sana na watu wote, hususan waliokuwa chini ya uongozi wake, kutokana na utendaji wake uliotukuka na moyo wa kujitoa kwa ajili ya nchi. Rais ameeleza kuwa alimpa jina la “kiraka” kwa sababu kila sehemu alipowekwa aliitumikia kwa ufanisi, uaminifu na matokeo chanya.
Aidha, Rais Samia amesema mafanikio ya Bunge na Taifa kwa ujumla yanategemea mshikamano wa viongozi wote wakiwemo Wabunge na Mawaziri, bila kujali tofauti zao. Amesisitiza kuwa Mhe. Jenista Mhagama alikuwa kiongozi jasiri, mlezi wa wengi ndani ya Bunge na Serikali, na nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana, akiongozwa na nidhamu ya hali ya juu katika utendaji wake.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema Marehemu Jenista Mhagama alikuwa mtumishi wa kweli wa wananchi, mnyenyekevu na mwenye mapenzi ya dhati kwa watu wake. Makamu wa Rais amesema katika maisha yake ya utumishi, jambo alilolitanguliza zaidi ni kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Peramiho kwa moyo wote.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa kama angepewa nafasi ya kuomba jambo moja kwa Mwenyezi Mungu, angeomba viongozi wote—Wabunge na Madiwani—wapende na kuwahudumia wananchi wao kwa kiwango cha kujitolea na uadilifu alioonyesha Marehemu Jenista Mhagama.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ametoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia ya marehemu, Wabunge na Watanzania kwa ujumla, kwa kuondokewa na kiongozi mahiri aliyeipenda nchi yake kwa dhati. Spika amesema Marehemu Mhagama alikuwa mtu aliyekuwa mnyenyekevu, aliyejishusha na kuwaheshimu watu wote bila kujali nafasi zao.
Akizungumza kwa niaba ya familia, mtoto wa Marehemu Jenista Mhagama, Victor Mhagama, amesema mama yao aliwafundisha kupenda kazi, kuwa na uzalendo wa kweli na kumcha Mungu. Amesema marehemu aliwausia kuchapa kazi kwa bidii, kujali utu wa watu wote na kusimamia haki bila upendeleo.
Victor ameongeza kuwa marehemu hakubagua watu kwa misingi ya hadhi, mali au umri, bali aliwahudumia wote kwa upendo na haki, akibaki kuwa kiongozi wa maendeleo na mwenye mapenzi makubwa kwa wananchi wa Peramiho na Taifa kwa ujumla.
Mwili wa Marehemu Jenista Joakim Mhagama unatarajiwa kuzikwa tarehe 16 Desemba 2025 katika Kijiji cha Ruanda, Wilaya ya Mbinga, ambako ndiko atakapopumzishwa katika nyumba yake ya milele.
#JenistaMhagama #RIPJenistaMhagama #RaisSamia #UongoziWaHuduma #TaifaKwanza #Peramiho
#Dodoma #Tanzania