Monday, September 08, 2025

BILIONI 51 KUTUMIKA UJENZI WA BARABARA, MASOKO NA STENDI JIJINI ARUSHA





Mradi wa Uendelezaji wa Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) unatekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 51 katika Jiji la Arusha ikiwa ni sehemu ya uendelezaji wa Jiji hilo katika eneo la miundombinu ya barabara, masoko na stendi. 

Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Arusha, Mhandisi Godfrey Bwire wakati akitoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na TACTIC katika Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa ni miongoni  mwa Majiji yanayonufaika na mradi huo.

Amesema mradi wa TACTIC katika Jiji la Arusha unatekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km 10.2 ambazo ni pamoja na barabara ya Oljoro Km 1.45, barabara ya Olasiti Km 3.96 na barabara ya Ngoselotoni Km 4.8 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 72 na inagharimu shilingi bilioni 20.7

Vile vile, Mhandisi Bwire amesema kuwa mradi huo unatekeleza miradi mingine ya ujenzi wa Soko la Kilombero, ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya Bondeni City kwa ajili ya mabasi ya mikoani ambayo inajengwa katika kata ya Murieti pamoja na kuboresha eneo la kuuzia nyama choma la Kwa Mromboo ambapo litajengwa soko jipya katika eneo hilo na kuongeza kuwa ujenzi wa miradi hiyo umefikia asilimia 6 na inagharimu shilingi bilioni 30.6.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt. Maduhu Nindwa amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha wameipokea kwa furaha  kubwa miradi hiyo kwa sababu wameiona faida kubwa kabla hazijatokea kwa mtu mmoja mmoja mpaka ngazi ya mkoa na taifa pia.

"Tulipokea miradi hii kwa upekee na kwa heshima kubwa kwa Serikali yetu kutukumbuka kwamba tuna uhitaji wa hii miundombinu ambayo itasaidia moja kwa moja kukuza biashara hususani katika ujenzi wa masoko ya Kilombero, soko la kwa Mromboo na ile barabara ya kwenda mji wa Bondeni City", amefafanua.

Dkt. Nindwa amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara itasaidia pia katika maeneo mengine ya utoaji huduma za kijamii hasa elimu na afya.

Amesema kwa upande wa elimu kutakuwa na magari mengi ya abiria ambayo yatapita katika barabara hizo kwa hiyo wanafunzi watachukuliwa kwa urahisi na kufika shuleni kwa wakati hivyo kusaidia kupandisha kiwango cha elimu katika Jiji hilo. 

"Kwa upande wa afya, tunafahamu kwamba Mhe. Rais alianzisha mfumo wa usafirishaji wa akina mama na watoto kwa njia ya dharura kwa kutumia ambulance za jamii maarufu kama  'm-mama', ujenzi wa barabara hizi utasaidia watu wengi kuwachukua akina mama wenye changamoto kutoka kwenye mitaa yetu na kuwawahisha hospitali kupata huduma kwa hiyo moja kwa moja unaona miradi hii inalenga kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga", amebainisha.

Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Oloresho, Bw. James Stephano amesema ujenzi wa barabara ya Oljoro utasaidia kurejesha biashara pembezoni mwa barabara hiyo zilizokuwa zimefungwa kutokana na kukosekana kwa wateja walioacha kutumia barabara hiyo kwa sababu ya ubovu wa barabara hiyo, lakini baada ya barabara hiyo kujengwa biashara zimerejea tena katika mtaa wake.

Sunday, September 07, 2025

Makamu wa Rais wa Tanzania Afika Addis Ababa Kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi








Addis Ababa, Ethiopia – 07 Septemba 2025 – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amewasili leo mjini Addis Ababa, akiwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Mkutano huu unaanza rasmi tarehe 08 hadi 10 Septemba 2025 na unalenga kuimarisha sauti ya Afrika katika mijadala ya kimataifa, kuongeza uhimilivu wa bara hili dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na kuendeleza ubunifu na juhudi za pamoja barani Afrika.

Utahudhuriwa na wawakilishi wa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti, pamoja na jamii asilia.

Aidha, Makamu wa Rais Dkt. Mpango anatarajiwa kushiriki katika mikutano ya kando yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na mataifa pamoja na mashirika mbalimbali yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania inasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuhakikisha Afrika inakabiliana vyema na changamoto za tabianchi na kuimarisha maendeleo endelevu.

MAJALIWA AZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE JIMBO LA MCHINGA.



















▪️Asema Rais Dkt. Samia anatosha, aomba wananchi kumchagua kwa kishindo

▪️Autaja mradi wa gesi pamoja na bandari ya uvuvi Kilwa

▪️Asisitiza kuwa Rais Dkt. Samia amedhamiria kujenga upya barabara ya Dar-Lindi

▪️Agusia Ujenzi wa Reli ukanda wa kusini

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 07, 2025 amezindua kampeni za Ubunge jimbo la Mchinga zilizofanyika katika kijiji cha Rutamba mkoani Lindi

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 imejielekeza katika kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini ikiwemo katika jimbo la Mchinga.

“Katika kipindi kilichoisha Rais Dkt. Samia ameleta hapa miradi mikubwa, ya kati na midogo, anafanya hivi kwa kutambua wananchi wanapaswa kuhudumia, hata ilani hii imeonesha maeneo mengine yatakayotekelezwa katika mkoa huu wa Lindi”

Amesema kuwa Wana-Lindi wanapaswa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza miradi ya gesi, bandari ya uvuvi Kilwa, ujenzi upya wa barabara ya Dar-Lindi, maboresho ya uwanja wa ndege wa Lindi, ujenzi wa reli ya kanda ya kusini pamoja na kuunganisha mkoa wa Lindi kwenye gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika.

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Lindi, ilani hii imeendelea kusheheni miradi inayokwenda kutekelezwa katika maeneo yetu, hii ni sababu pekee ya sisi kumchagua Rais Dkt. Samia.

“Ilani ya uchaguzi ya 2025/2030 imeonesha kuwa kutaanza kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Ngongo-Ng’apa, Mandawa hadi Chikundi, barabara hii itakuwa ni mkombozi kwa wakati wa wakazi wa maeneo haya na itafungua uchumi kwa Wana-Lindi.”

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jimbo hilo limefanikiwa kuwa na magari ya wagonjwa Manne pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha huduma za afya katika jimbo hilo. 

“Mheshimiwa Salma Kikwete amejikita katika kuwahudumia wananchi, kwa namna jimbo hili lilivyokaa linahitaj mtu mahiri na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake, hakika Mheshimiwa Salma ameonesha ameweza, mchagueni tena”

Kwa Upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo Salma Kikwete amesema kuwa katika katika kipindi chake amefanikiwa kushirikiana na WanaMchinga kutafuta majibu ya changamoto yaliyo katika jimbo hilo

“Tumepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na changamoto zetu, hali ilivyo leo sio sawa na tulikotoka, tumepata mafaniko katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, nishati, elimu, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi, nikipata ridhaa tena tutafanya makubwa zaidi”

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano amefanikiwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ng’apa ambao utawezesha kuvifikia vijiji vingi katika jimbo la Mchinga. “kama hiyo haitoshi tumefanikiwa kujenga zahanati, tutaongeza juhudi za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya”

Naye Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kuwa anatosha katika nafasi ya Urais, kwani katika kipindi kifupi amefanya mambo mengi tumpe nafasi aendelee

“Alipata Urais katika wakati ambao hakutarajia, lakini amefanya kazi nzuri, tutanufaika mara dufu, tukimpa nafasi, nimeangalia orodha ya mambo yaliyo kwenye ilani kwa hakika amejipanga”

Akizungumza kwa niaba ya wagombea ubunge mkoa wa Lindi, Mgombea ubunge jimbo la Mtama Nape Nnauye amesema kuwa wanakusini watamchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika mkoa huo ikiwemo utoaji wa Ruzuku ya pembejeo kwenye mazao.

Dkt. Salem Al-Junaibi na Ujumbe wake Awasili nchini kwa Ziara ya Kibiashara













Mwenyekiti wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman Dkt. Salem Al-Junaibi (Mb) na ujumbe wa Wafanyabiashara wa Oman, amewasili nchini leo, tarehe 7 Septemba 2025, kwa ziara ya siku tano, kuangazia fursa za uwekezaji na biashara za Tanzania, katika sekta mbalimbali.

Mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake, alipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Twaibu, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdalah Kilima. 

Viongozi wengine waliompokea ni Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania, Rashid Al Mandhir, pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali na Sekta binafsi.

Katika ziara yao, Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake wanatarajiwa kukutana na viongozi wa Serikali pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, zikiwemo Tume ya Ushindani (FCC), Kiwanda cha Nyama – Kibaha, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), KAMAKA, TISEZA, BRELA, TANTRADE, TBS, TIRDO na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Aidha, ujumbe huo pia utatembelea Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), pamoja na Bodi ya Chai Tanzania (TTB). 

Vilevile ujumbe huo pia utashiriki katika mazungumzo na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Nishati, pamoja na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji. Katika mikutano hiyo, pande hizo mbili pia zitasaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Oman.

Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake pia watatembelea Zanzibar ambako watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ZIPA, ZNCC, pamoja na kutembelea Eneo Maalum la Uchumi Zanzibar.

Mbali na mazungumzo hayo na Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar, ujumbe huo wa wafanyabiashara wa Oman pia utafanya mawasilisho kuhusu hali ya biashara na viwanda nchini Oman, pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano wa kibiashara kati ya Oman na Tanzania.

Ziara hiyo ya Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake inatarajiwa kukamilika tarehe 12 Septemba, 2025, kabla ya kurejea nchini Oman.

Friday, September 05, 2025

TANZANIA IMEJENGWA KWA MISINGI IMARA YA AMANI NA UZALENDO-MAJALIWA








WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania imejengwa kwa misingi imara ya amani, uzalendo na maadili mema ambayo yameasisiwa na viongozi wa Taifa hilo.

Amesema kuwa wakati wote viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali kuhamasisha amani, kukemea uovu na utovu wa nidhamu katika jamii ili kujenga kizazi chenye heshima, mshikamano na uzalendo kwa Taifa.

Amesema hayo leo Ijumaa (Septemba 05, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika Wilayani Korogwe mkoani mkoani Tanga

Amesema kuwa Maulid ni tukio lililobeba mwongozo wa kiroho kwa wanadamu wote. “Maisha ya Mtume yanaonesha mfano na yanatufundisha kuwa waadilifu, kuishi kwa maadili, na kumtegemea Mwenyezi Mungu. katika kila jambo”. Amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin Ali ametoa wito kwa Masheikh nchini kuendelea kuhubiri amani katika maeneo yao kwa kuwa amani si jambo la hiari hivyo kila mmoja anapaswa kusimamia uwepo wake. “Wafundisheni waumini katika majukwaa yenu ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, kemeeni vitendo vyote vyenye ishara ya uvunjifu wa  amani”

Akisoma salam za Baraza kwenye sherehe za baraza la maulid, Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaj Nuhu Jabir Mruma amesema kuwa amani na utulivu ni  kigezo kikuu cha maendeleo kwa bila amani hakuna Ibada, hakuna maisha wala maendeleo yoyote. 

“Hali kubwa ya maendeleo tuliyonayo na yanayoshamiri leo katika nchi yetu msingi wake mkubwa ni amani. Hatuna budi Watanzania wote kuienzi TUNU ya amani tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kupitia jukwaa hili tunawanasihi Waislamu na wananchi kwa ujumla kuzingatia misingi ya amani na utulivu katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025”.

BILIONI 51 KUTUMIKA UJENZI WA BARABARA, MASOKO NA STENDI JIJINI ARUSHA

Mradi wa Uendelezaji wa Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) unatekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 51 katika Jiji la Arusha ikiwa...