MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) Nehemia Kyando Mchechu, amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Mikopo ya
Nyumba ya Umoja wa Afrika (AUHF) kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi
huu. Atatumikia katika Bodi hiyo hadi Oktoba, 2014.
Uchaguzi wa Mchechu na Wajumbe wenzake nane wa
Bodi ya AUHF kushika nafasi hiyo muhimu barani Afrika, umefanyika hivi karibuni.
AUHF hivi sasa ina wanachama 38 kutoka nchi 17 duniani, za Botswana, Ghana,
Kenya, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini,
Swaziland, Tanzania, Gambia, Uganda, Uingereza, Marekani na Zimbabwe.
AUHF
ilianzishwa kama ya wanachama wakopeshaji wa mikopo ya nyumba mwaka 1984. Hivi
sasa ina wanachama 38 kutoka mataifa 17, ikiwa na lengo la kuboresha ustawi wa
mikopo ya nyumba barani Afrika kwa kujenga uwezo wa kitaasisi kwa taasisi husika
na kufanya kazi na serikali za nchi wanachama kuwa na sera za maendeleo zenye
mazingira bora ya soko.
Kupitia mikutano yake na kazi inazofanya
sambamba na tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa mbalimbali inazozitoa
kwa wanachama, AUHF imekuwa kiongozi mkuu katika kustawisha masoko ya mikopo ya
nyumba kwaajili ya jamii ya kiafrika.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuchaguliwa
kuingia katika bodi ya Shirika hilo, Mchechu alisema kuwa maendeleo ya soko la
mikopo ya nyumba nchini Tanzania yatakuwa kwa kasi zaidi sasa.
“Tunaamini ya kwamba, ujuzi tulio nao hapa
Tanzania unaweza kuwa na mchango mkubwa saana katika maendeleo ya sekta ya
nyumba barani Afrika na Duniani. Faida ya kuwa na jumuiya kama hii ya kikanda
ni kwamba tunaweza sasa tukabadilishana uzoefu na ujuzi kutoka maeneo
yote,”alisema Mchechu.
Mchechu amechaguliwa kuingia katika Bodi hiyo ya
Afrika, sambamba na Mtanzania mwingine Oscar Mgaya, ambaye ni Kaimu Afisa
Mtendaji Mkuu wa wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba (TMRC).
TMRC ni kampuni binafsi ambayo ilianzishwa kwa
mkopo wa dola milioni 30 kutoka Benki ya Dunia, ili kufanikisha upatikanaji wa
mtaji wa mikopo ya nyumba hapa nchini.
Benki ambazo mpaka sasa zimenunua hisa katika
kampuni hiyo kuwa ni CRB, Azania Bank, TIB, Exim Bank, Dar es Salaam Community
Bank, NIC Bank, Banc ABC, NBC, People Bank of Zanzibar na BoA.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam
Mgaya alisema kuwa “AUHF ina historia ndefu ya kuchagiza maendeleo ya mifumo ya
mikopo barani Afrika. Mwenyekiti wa Bodi hiyo ni Colin Chimutsa, ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara
ya Zimbawe (CBZ), ametumikia pia nafasi ya ujumbe chini ya Mwenyekiti Mstaafu, Reginald
Motswaiso.
Makamu Mwenyekiti ni Charles Bonsu, ambaye ni
Meneja Mkuu wa mikopo na masuala ya wateja wakubwa wa Benki ya Biashara yenye
mtandao mkubwa ya HFC ya Ghana.
Mweka Hazina ni Cas Coovadia, Mkurugenzi Mkuu wa
Jumuiya ya Kibenki ya Afrika Kusini, pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa
ya utoaji mikopo ya nyumba, amechaguliwa tena katika bodi hiyo kwani alikuwapo
katika bodi iliyopita.
Katibu
Mkuu, Oscar Mgaya, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba
(TMRC, yeye ni mpya katika bodi hiii.
Reginald Motswaiso, ambaye ni Afisa Mtendaji
Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa la Botwana, amechaguliwa tena kuingia katika
bodi hii mpya baada ya kutumikia kama Mwenyekiti katika Bodi iliyopita.
Mwingine ni Manilall Seetohul, ambaye ni
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Nyumba ya Mauritius naye kama walivyo wengine
amechaguliwa tena kuingia katika bodi hii, baada ya kutumikia katika bodi
iliyopita..
Katika orodha hiyo ya wajumbe wa bodi pia yupo Madu
Hamman, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Fedha na Utawala wa Kampuni ya Abbey
Building Society PLC ya nchini Nigeria.
No comments:
Post a Comment