Sunday, June 29, 2025

 









Leo Tarehe 29 Juni, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Said Shaib Mussa amempokea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Mhe. Abdisalam Abdi Ali ambaye amewasili leo nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Mhe. Abdisalam Abdi Ali anataarijia kuhudhuria maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru wa Somalia ambayo Mgeni rasmi ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)

Pamoja na Mambo Mengine, Mhe. Abdi Ali anatarajiwa kushiriki mazungumzo ya Uwili kwa ajili ya kujadili na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya mataifa haya mawili na kutembelea Mbuga ya Wanyama ya Mikumi iliyopo Mkoa wa Morogoro.

Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia ni marafiki wa muda mrefu

TUTAENDELEA KUILINDA NA KUIDUMISHA AMANI NCHINI-MAJALIWA





▪️Asema falsafa ya 4R ya Rais Dkt. Samia imekuwa msingi imara wa kulinda amani.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kulinda na kudumisha amani nchini ili kuhamasisha maendeleo na kuziba mianya ya kuibuka kwa migogoro miongoni mwa wanajamii.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili Juni 29, 2025) wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufunga kongamano la Afrika Mashariki la Amani lililoandaliwa na The Islamic Foundation, katika viwanja vya shule ya msingi Mirongo jijini Mwanza

“Nataka niwaambie bila amani hatuwezi kupata mafanikio yoyote, kupitia kongamano hili mmepata nafasi ya kujadili kuhusu tunu hii ya amani, ambayo wakati wote tumeshuhudia viongozi wa dini mkiwa kwenye majukwaa yenu mkihimiza amani miongoni mwa wanajamii, tuishike tunu hii”. 

Kadhalika, amewataka Watanzania kuangalia kwa upana wake suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii hasa kwa vijana. “Ni muhimu sana suala hili mkaliweka kama agenda katika mikutano na vikao vyenu, kila kiongozi wa dini anapozungumza, suala la maadili na mmomonyoko wa liwe ni ajenga ya kudumu”

Amesema kuwa mabadiliko ya teknolojia na kuiga tamaduni za mataifa ya nje imekuwa miongoni mwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili. “Siku hizi vijana kuwaita wazee kwa majina yasiyo na heshima ni kitu cha kawaida, viongozi ndio wenye jukumu la kusimamia eneo la maadili, mkifanya hivyo tupata vijana wenye maadili mema”

Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa falsafa ya 4R ya Resilience (Ustahimilivu), Reconciliation (Maridhiano) and Reforms (Mageuzi), Rebulding (Kujenga upya) iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi imara ya kulinda amani. “Falsafa hii imeifanya Tanzania kuwa tulivu na salama”

Wakati huo huo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa jamii inapaswa kuona umuhimu wa kukuza utamaduni wa majadiliano na maridhiano katika kushughulikia tofauti zilizopo mingoni mwa jamii.

“Tunapaswa kujenga jamii inayoheshimu maoni tofauti, na kuhimiza mijadala kwenye majukwaa na kwa nafasi hii viongozi, taasisi na wanajamii mnapaswa kuwa daraja la maridhiano badala ya kuwa vyanzo vya migawanyiko”

Naye Mwenyekiti wa Islamic Foundation Aref Nahdi amesema kuwa taasisi zao zitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuijenga Tanzania yenye haki, Amani, usawa, maendeleo na heshima kwa wote.

Aidha, amesema kuwa taasisi hizo zitaendelea kukemea vikali kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa amani, upendo na kuvunja heshima za viongozi wa kitaifa. “Kwa kufanya hivyo inakuwa ni sehemu ya mafundisho ya dini”.

Thursday, June 26, 2025

RAIS SAMIA ASAFIRI KWENDA DODOMA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA BUNGE LA 12








Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 26 Juni 2025, amesafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Jijini Dodoma kwa ziara rasmi ya kiserikali.

Safari hii inaambatana na tukio muhimu la kitaifa, ambapo kesho tarehe 27 Juni 2025, Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kutoa hotuba maalum na kuhitimisha rasmi shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hotuba ya Rais inatarajiwa kugusa masuala muhimu ya kitaifa ikiwemo tathmini ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo, mwenendo wa kisiasa na kijamii nchini, pamoja na mwelekeo wa Serikali katika kipindi kijacho. Tukio hili ni muhimu kwa taifa kwani linaweka msingi wa maelekeo mapya kwa mihimili ya dola, hasa Bunge na Serikali.

Wananchi wanaendelea kufuatilia kwa karibu matukio haya ya kihistoria ambayo yanadhihirisha uimara wa demokrasia na utawala bora nchini Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia.

Wednesday, June 25, 2025

SERIKALI YAWAREJESHA WATANZANIA 42 KUTOKA NCHINI IRAN NA ISRAEL








 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwarejesha salama nchini Watanzania 42 kutoka nchini Israel na Iran kufuatia vita vilivyokuwa vikiendelea baina ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea Watanzania hao kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amesema zoezi la kuwarejesha Watanzania wote salama nchini ni utekelezaji wa agizo maalumu la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kwamba Watanzania wote waliopo katika mataifa hayo mawili wanarejeshwa nchini salama

Aidha Balozi Shelukindo amesema leo juni 25, 2025 wameingia Watanzania makundi mawili, kundi moja liliwasili mchana wa leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume na kwamba gharama zote za kuwarejesha Watanzania hao zimegharamiwa na serikali na kuongeza kuwa Watanzania wengine kutokea nchini Iran wanatarajiwa kuwasili nchini kesho Juni 26, 2025.

Balozi Shelukindo pia kupitia hadhara hiyo, ametoa rai kwa Watanzania wote kuhakikisha kwamba tunaendelea kuilinda tunu yetu ya utulivu na amani kama ambavyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotuasa mara kwa mara.

Akizungumza katika mapokezi hayo, mmoja kati ya wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini Israel Bi. Neema Dasina amesema hali ya usalama nchini Israel ilikuwa mbaya kufuatia milipuko ya mabomu ya mara kwa mara isipokuwa kupitia maelekezo mahususi kutoka kwa ubalozi wa Tanzania nchini humo na ule wa nchini Misri, huku akiishukuru serikali na Mhe. Rais Samia kwa kwa ujumla jinsi ambavyo wameonyesha thamani ya Watanzania hasa katika kipindi hiki cha hatari iliyokuwa mbele yao.

Mama mzazi wa mmoja wa vijana waliorejea salama kwa niaba ya wazazi wengine Bi. Asela Luena, ameishukuru serikali ya Mhe. Rais Samia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa juhudi za dhati za kuwapigania watoto wao, na kuhakikisha kwamba wanarejea salama na kuungana na familia zao.

 “baada ya kupata taarifa za hali ya usalama nchini Israel hatukulala usingizi, niliwasiliana na binti yangu, aliniambia mama usiwe na wasiwasi kwasababu sisi wote tupo kwenye mikono salama, serikali imeingilia kati na kila kitu tunafanyiwa na serikali, kwakweli sisi wazazi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa upendo wake wa dhati kwa taifa letu, tumefarijika sana kama familia lakini kama taifa hii ni heshima kubwa duniani” alimalizia mama Asela Luena.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefikia uamuzi huo wa kuwarejesha Watanzania wote waliopo katika mataifa ya Israel na Iran kufuatia mapigano yaliyozuka baina ya mataifa hayo mawili, japokuwa siku chache zilizopita zilitolewa taarifa za kumaliza vita hivyo vilivyodumu kwa takribani siku kumi na mbili mfululizo.

Viongozi wengine walioambatana na Katibu Mkuu Balozi. Dkt. Samwel Shelukindo katika mapokezi hayo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ni pamoja na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga

MAKAMU WA RAIS MHE. DKT. PHILIP MPANGO AWASILI ABUJA, NIGERIA KUMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MKUTANO WA AFREXIM







Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amewasili leo tarehe 25 Juni 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nnamdi Azikiwe uliopo Jijini Abuja, Nigeria, kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 32 wa Benki ya Maendeleo ya Mauzo ya Nje ya Afrika (Afrexim Bank).

Makamu wa Rais anahudhuria mkutano huo akimwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amenominate uwakilishi huo wa juu katika mkutano unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 Juni 2025.

Aidha, Watanzania mbalimbali waishio nchini Nigeria walijitokeza kumpokea kwa furaha na heshima Makamu wa Rais alipowasili, wakionesha mshikamano na mapenzi kwa taifa lao. Tukio hilo limeonesha uzito na umuhimu wa ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kikanda na kimataifa yenye lengo la kuimarisha uchumi na ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa ya Afrika.

Mkutano wa Afrexim ni jukwaa muhimu linalokutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha na wawekezaji kujadili fursa za maendeleo ya biashara barani Afrika, ambapo Tanzania ina nafasi muhimu ya kuchangia na kunufaika.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unatarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kifedha na kibiashara kati ya Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Benki ya Afrexim.

Bodi ya TFS yatembelea Hifadhi za Pugu-Kazimzumbwi na Vikindu, yapongeza kasi ya uwekezaji wa utalii wa ikolojia




Na Mwandishi Wetu, Kisarawe – Pwani

Ujumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetembelea Hifadhi za Mazingira Asilia za Pugu–Kazimzumbwi na Vikindu mkoani Pwani, ukielezea kuridhishwa na kasi ya uwekezaji wa miradi ya uhifadhi na utalii wa ikolojia inayoendelea kutekelezwa na TFS.

Ziara hiyo ya siku mbili, iliyoanza tarehe 24 Juni 2025, iliongozwa na Mjumbe wa Bodi, Bi Piencia Kiure, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na maendeleo ya utalii katika maeneo ya hifadhi za misitu ya asili, ambayo ni muhimu kwa bioanuwai na huduma za kiikolojia.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bi Kiure alieleza kufurahishwa na uboreshaji wa miundombinu ya hifadhi hizo, hususan katika maeneo ya kupokelea wageni, vibanda vya mapumziko na ukumbi wa shughuli za kijamii na kitalii.

"Ni dhahiri sasa kwamba hata Mkoa wa Pwani unaweza kuwa kitovu cha utalii wa misitu. Hifadhi ya Pugu–Kazimzumbwi na Vikindu ni maeneo ya pekee kwa utalii wa kimya, kutafakari, na kutuliza akili. Huu ni utalii unaomgusa moja kwa moja binadamu katika afya ya akili na ustawi wa jamii,” alisema Bi. Kiure.

Aidha, alisisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa na TFS chini ya uongozi wa Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, ni ishara ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika uchumi wa Taifa kupitia uhifadhi endelevu na utalii wa mazingira.

"Bodi inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na menejimenti ya TFS. Kasi ya utekelezaji wa miradi ni ya kutia moyo na tunaamini itaongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuimarisha mapato ya serikali na huduma kwa jamii,” aliongeza.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda ya Mashariki wa TFS, Bw. Mathew Ntilicha, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, aliishukuru Bodi kwa ziara hiyo na kupokea mapendekezo yaliyotolewa kwa ajili ya kuboresha zaidi maeneo ya hifadhi.

"Tunaendelea kuboresha huduma, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka hifadhi, na kuandaa vivutio vya kipekee vitakavyovutia wageni wa ndani na wa kimataifa. Tunawakaribisha Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea maeneo haya,” alisema Ntilicha.

Wakati wa ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walitembelea pia baadhi ya miradi ya kimkakati ikiwemo ule wa “Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi,” unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF).

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Bodi ulipata fursa ya kukutana pia na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mh. Petro Magoti, ambaye alipongeza juhudi za TFS katika kulinda rasilimali za taifa.

"Uwepo wa ugeni huu ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za umma. Juhudi za TFS katika uhifadhi ni mfano bora wa utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema DC Magoti.

Ziara ya wajumbe wa Bodi ya TFS inatarajiwa kuhitimishwa leo tarehe 25 Juni 2025, ambapo wajumbe watakutana na Menejimenti ya TFS Kanda ya Mashariki kwa ajili ya majadiliano ya kitaalamu, tathmini ya miradi, na kutoa maelekezo ya kimkakati kwa maboresho ya baadaye.

Tuesday, June 24, 2025

RAIS SAMIA AWASILI MSUMBIJI KWA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU











MAPUTO – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Maputo, Msumbiji leo tarehe 24 Juni 2025, kwa ajili ya kushiriki katika sherehe kubwa za kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Msumbiji.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maputo, Rais Samia alipokelewa kwa heshima zote za kitaifa, kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Rais wa Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, ambaye amemualika kama Mgeni Rasmi katika tukio hilo la kihistoria.

Sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika kesho, tarehe 25 Juni 2025, katika Uwanja wa Machava uliopo jijini Maputo, zikihusisha viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, pamoja na wananchi wa Msumbiji waliojitokeza kuadhimisha mafanikio ya nusu karne tangu taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa wakoloni wa Ureno mwaka 1975.

Ushiriki wa Tanzania katika sherehe hizi ni ishara ya kudumisha uhusiano wa kihistoria na kindugu kati ya Tanzania na Msumbiji, uhusiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Samora Machel.

Rais Samia anatarajiwa pia kushiriki katika shughuli nyingine za kidiplomasia ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

  Leo Tarehe 29 Juni, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Said Shaib Mussa am...