ANAYEDAIWA kumuua askari wa kikosi cha usalama barabarani wiki
iliyopita, Elikiza Nnko, Jackson Stephen Fimbo, jana alifikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na makosa ya matatu,
likiwemo kosa la kuingilia msafara wa Rais.
Mbele ya Hakimu Mkazi Kwey Lusema, Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Lasdilaus Komanya, alilitaja kosa la kwanza kuwa ni la kusababisha kifo
cha trafiki huyo kwa kumgonga na gari alilokuwa alikiliendesha.
Ilidaiwa kuwa Machi 18, mwaka huu, katika Barabara ya Bagamoyo kwenye
taa za Bamaga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa anaendesha gari
lenye namba za usajili T328 BML aina ya Land Lover Discovery, alitenda
kosa hilo.
Komanya alidai mshtakiwa huyo aliendesha gari hilo kwa mwendo wa
hatari katika barabara hiyo jambo ambalo huhatarisha usalama wa raia,
hivyo kumgonga askari huyo aliyezikwa Alhamisi iliyopita.
Alidai kosa la pili ni kuingilia msafara wa kiongozi, kuwa tarehe
iliyotajwa hapo juu, mshtakiwa hakutii maelekezo yaliyokuwa yakitolewa
kwa ishara na askari huyo (marehemu Elikiza) ambaye alikuwa na wajibu wa
kuyasimamisha magari kwa njia ya ishara.
Komanya alidai shtaka la tatu ni la kushindwa kutoa taarifa za kusababisha ajali katika barabara hiyo.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikanusha mashtaka hayo na Komanya alidai
upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, anaomba tarehe ya kuja kumsomea
maelezo ya awali mshtakiwa.
Kwa upande wake hakimu Rusema alisema ili apate dhamana ni lazima awe
na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya sh milioni 2 hata
hivyo mshtakiwa alitimiza masharti hayo na kesi hiyo imeahirishwa hadi
Aprili 15 itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,
imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi
inayomkabili aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima na wenzake,
kwa sababu Kibanda bado amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika
Kusini kwa ajili ya matibabu, hivyo kuahirishwa hadi Aprili 29 mwaka
huu.
Comments