WAZIRI
wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka (kulia) akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani) kuhusu uzinduzi wa kampeni ya Okoa Mtoto wa Kike Tanzania
itakayofanyika baadaye mwezi ujao wilayani Tarime, Mara. Kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group inayoratibu kampeni hiyo,
Mossy Magere.
MKURUGENZI
Mtendaji wa Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group, Mossy Magere (Kushoto) na Waziri
wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka wakionesha kwa waandishi wa habari kipeperushi
cha uzinduzi wa kampeni ya Okoa Mtoto wa Kike Tanzania, itakayofanyika hivi
karibuni .
*** ***
Na mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imeshauriwa kuangalia upya adhabu
zinazotolewa kwa watu wanaofanya vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto
nchini.
Ushauri huo umetokana na kuendelea kushamiri kwa
vitendo vya unyanyasaji huku vyombo na mamlaka husika vikishindwa kutoa adhabu
kali kwa lengo la kukomesha.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Okoa Mtoto wa Kike Tanzania.
Kwa kuanzia kampeni hiyo itazinduliwa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, na baadaye kusambaa kwenye maeneo mbalimbali nchini hasa yaliyoshamiri kwa vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto.
Gaudentia, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, alisema licha ya kuwepo kwa sheria lakini bado vitendo vya unyanyasaji vimezidi kushika kasi, jambo linaloashiria kuwa adhabu zinazotolewa bado ni ndogo.
“Unyanyasaji umekuwa kwa kiwango kikubwa mno na umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo ya wanawake nchini. Sheria zipo na watu anapewa adhabu, lakini tunadhani kuna kila sababu ya kuangaliwa upya ili kukomesha kabisa vitendo hivi,” alisema Gaudentia.
Alisema zaidi ya moja ya tatu ya wanawake nchini wameshakabiliana na ukatili wa kijinsia na kwamba, mgawanyo wa unyanyasaji ni mkubwa zaidi kwa wanawake hasa waliotalikiwa na wajane.
“Hili ni tatizo kubwa kwani, utafiti unaonyesha asilimia 23 ya wasichana wenye umri kati ya 15 hadi 19 tayari wamejifungua, hivyo kushindwa kuendelea na masomo kwa ajili ya kuajiandaa na maisha yao ya baadaye,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group (NMG), Mossy Magere, alisema kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Machi 3, mwaka huu.
Alisema wameamua kushirikiana na Gaudentia kutokana na kuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanawake na kwamba, tatizo hilo la unyanyasaji limekuwa kubwa mkoani Mara.
Mossy alisema kampeni hiyo itakuwa endelevu na kwamba, itakwenda sambamba na uanzishwaji wa klabu za kupinga unyanyasaji katika shule mbalimbali kwa lengo kuleta usawa.
“Unyanyasaji wa kijinsia unaumiza wanawake na watoto wengi nchini, ni lazima jamii ikubali kubadilika ili kila mtu awe na furaja katika maisha badala ya wengine kufikia hatua ya kujuta kuzaliwa,” alisema Mossy.
No comments:
Post a Comment