Absalom Kibanda,Mwenyekiti wa Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF)
UTANGULIZI
1.
JUKWAA
la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa masikitiko taarifa kwamba Bunge linaandaa
utaratibu wa kuzuia vyombo vya habari kurusha moja kwa moja (live) matangazo ya
Bunge.
2.
Taarifa
ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah aliyoitoa juzi Jumatano, Februari 13,
2013 inasema kwamba eti ni kosa pia kwa wapigapicha kuwapiga picha wabunge
wakiwa wamesinzia ndani ya ukumbi wa bunge.
3.
Kwamba
baadhi ya wabunge wanazomoka kwa kujua kwamba michango yao inarushwa moja kwa
moja hewani na hivyo kufanya vituko bungeni, kwahiyo kuzuia matangazo ya moja
kwa moja ni kuwadhibiti wale wanaofanya fujo na vituko Bungeni.
4.
Dk.
Kashililah anasema kwamba ofisi yake inaandaa mpango wa kurekodi vipindi hivyo
na kuvirusha baadaye vikiwa vimehaririwa na kwamba ofisi yake inawasiliana na
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupata njia ya kurusha matangazo hayo ya
Bunge yaliyohaririwa.
MAONI YA TEF
Hatua
hii ya ofisi ya Bunge inatupa shaka na pengine ni ishara ya mwendelezo ya kile
ambacho kinaonekana kama jitihada mpya za kuuminya uhuru wa habari nchini. Kwa
maana hiyo;
1.
Tunashangaa
Bunge la Tanzania limejifunza wapi siasa hizi za kufunika mambo yanayowahusu
wananchi, huku likijua kwamba wanaofuatilia vikao hivyo ndio walipa kodi na
wapiga kura wa wabunge ambao uongozi wa Bunge unataka kuwalinda?
2.
Ni
kama Taifa letu linarudi katika enzi za giza la usiri ambao kimsingi hatupaswi
kuurejea. Tangazo hili ni moja ya mambo ya bahati mbaya yanayoikuba nchi yetu
kwa sasa, wakati ambao dunia inahimiza uwazi hasa katika vyombo vya uamuzi.
3.
Ikumbukwe kwamba Tanzania imetokea katika
mfumo wa chama kimoja kilichoshika hatamu hadi 1992, ambao uliifanya Serikali,
Bunge na Mahakama kuendeshwa kwa usiri wa hali ya juu.
4.
Mara
zote, usiri ni chimbuko la matumizi mabaya ya madaraka ni kinyume na misingi ya
utawala bora na usiri unatoa mamlaka yasiyositahiki kwa kikundi cha watu
wachache wenye masilahi binafsi ya kufisadi nchi.
5.
Hali
hii inatufanya tuwe na shaka iwapo serikali yetu ilifanya kwa dhati mambo
yafuatayo:(a)
Kuridhia
Tamko la Haki za Binadamu, Desemba 10, 1948 ambapo Kifungu cha 19 cha tamko
hili (Article 19) kinatoa uhuru wa mtu kutoa na kupokea mawazo bila kujali mipaka
ya nchi na haki hii ya kutoa mawazo haipaswi kuingiliwa.
(b)
Kufanya
mabadiliko ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1984 ambayo kwa
mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, yaliliingiza tamko hili la Haki za
Binadamu hivyo kuwezesha Ibara ya 18 ya katiba hiyo ya 1977 kuakisi Kifungu cha
19 cha tamko hiko kwa kutoa uhuru mawasiliano na haki ya kupewa taarifa.
(c)
Kutia saini Mpango wa Sherikali ya Uwazi (Open
Government Partnership/Initiative) unaongozwa na Rais Barrack Obama wa Marekani
mwaka 2010, ambapo tayari Wizara ya Katiba na Sheria imeanza mchakato wa
kutunga Sheria ya Haki ya Kupata Habari, itakayoruhusu nyaraka zote muhimu za
Serikali kuwekwa wazi kwa wananchi.
SIMAMO WA TEF
1.
Tunautaka
uongozi wa Bunge kuachana na harakati
hizo kwani hazitasaidia kukuza demokorasia au kuboresha maadili ya Bunge. Badala
yake zitazidisha mashaka ya umma dhidi ya chombo hicho cha uwakilishi kwa wananchi
kutaka kufanya kazi zao “gizani”.
2.
TEF
tunamaani kwamba kazi ya utangazaji si kazi inayopaswa kusimamiwa na uongozi wa
Bunge, wala hatuna kumbukumbu za matukio na hatua za namna hii katika miaka ya
karibuni, hata katika nchi nyingine.
3.
Ikumbukwe
kuwa, kama si ufinyu wa nafasi na mfumo wa uwakilishi bungeni tunaoutumia,
ilibidi wananchi wote waingie bungeni na kutoa mawazo yao. Kwa maana nyingine
wabunge ni wawakilishi wa wananchi na hivyo ni dhambi kuweka usiri wa yale
yanayozungumzwa au kuhariri alichozungumza mbunge aliyetumwa na wananchi.
4.
Tunaamini
kwamba jitihada zozote za kuwafungia wabunge ndani na kuhariri kazi wanazofanya
na matamko wanayotoa, ni ishara kwamba Bunge linataka kuficha maovu au udhaifu
wa mhimili huo au mihimili mingine inayowajibishwa na wabunge.
5.
Hatua
hii ya kuzuia vikao vya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja itakuwa inawachimbia kaburi
la kisiasa wabunge kwani ndio wanaomulikwa kwa majibu ya maswali wanayoulizwa
na hatua wanazochukua.
6.
Jukwaa
la wahariri linaamini kwamba utaratibu huu unaoandaliwa sasa na Dk. Kashililah
ni wa kidikteta na ni mbaya kuliko udikteta wowote uliowahi kutokea hapa nchini
kwa miaka yote ya uhuru wa Tanzania.
7.
Kwa
hatua hii uongozi wa Bunge utakuwa umedhihirisha udhaifu usiomithilika ambao uongozi
wa Bunge uliopita uliuondoa kwa kuweka misingi na kanuni za uwazi na
uwajibikaji. Ni kwa sura ya nje, harakati hizi za uongozi wa sasa wa Bunge
zinaonekana kama hatua za kufuta yaliyofanywa na uongozi wa Bunge la tisa.
8.
Katika
mazingira haya, tunaamini kwamba iwapo hili litatokea, jitihada ndogo za uwazi
zilizokuwa zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete,
zitafutika na kiumfanya raia aonekane mbele ya jumuiya ya kimataifa kuwa kiongozi
dhalimu na dikteta asiyevumilia kukosolewa.
9.
Na
kwa kuwa hili linatokea kueleka mwisho wa uongozi wake, ni dhahiri litakuwa
limefuta mema mengi aliyotenda na kujivunia katika misingi ya uwazi na
uwajibikaji.
10.
Kwa
ujumla hatua hii itavifanya serikali na Bunge visiaminike kwa umma na
itasababisha zogo na vurugu zisizomithilika kwani waliojifungia ndani watatoka
na kusema hadharani kwa jinsi watakavyoona inafaa hivyo kuharibu kabisa mfumo
wa taarifa za chombo hicho.
11.
Jukwaa
linaamini kwamba njia halisi ya kurejesha amani Bungeni ni uongozi wa Bunge
kutenda haki wa wabunge wote; maana hata vikao vyao visiporushwa moja kwa moja,
vurugu hazitaisha iwapo wahusika hawataamini kwamba wanatendewa haki.
12.
Kuhusu
suala la wabunge kulala bungeni na wakapigwa picha, tunasema magazeti na
televisheni zinazofanya hivyo zinastahili kupongezwa badala ya kulaumiwa.
Bungeni si mahala pa kusinzia, ni mahala pa kuchapa kazi. Wabunge wanaotaka
kulala usingizi wabaki hotelini na si kulala kwenye ukumbi wa bunge.
HITIMISHO
1.
Watanzania
wamepata fursa ya kuwafahamu wabunge wao baada ya utaratibu wa kurusha moja kwa
moja mijadala ya wabunge kuanza miaka ya 2000. Kwa maana hiyo jaribio lolote la
kuzuia matangazo hayo ni kuturejesha enzi za Bunge mazongwe na kadhia ya kuficha habari ambapo hata barua za
mialiko ziligongwa mihuri ya siri.
2.
Ndiyo
maana tumesema hatua hii inakiuka misingi ya uhuru, uwazi na uwajibikaji wa
vyombo vya umma na viongozi wa serikali. Ni mpango unaoweza kusababisha vurugu
zitokanazo na kiu ya wananchi kujua kinachoendelea na kutumia taarifa potofu
watakazozipata popote wanapojua na kwa staili wanayojua.
3.
Iwapo
kuna kasoro katika Kanuni za Bunge zinazotokana na Sheria ya Haki, Wajibu na
Mamlaka ya Bunge ya Mwaka 1988, basi kasoro hizo zirekebishwe na kuwabana
wabunge wanaozikiuka. Lakini
hatukubaliana na mpango wa Bunge kuwaadhibu wananchi wasione kinachoendelea
bungeni eti kwa lengo la kuwalinda wabunge.
4.
Mwisho
tunasema nia ya kudhibiti (censorship), kuhariri na au kuzuia baadhi ya habari
kutoka bungeni, kamwe Jukwaa la Wahariri halikubalini nayo na litaendelea
kuipiga hadi hatua ya mwisho. Tunawataka wananchi watuunge mkono katika msimamo
huu na sisi kama wahariri tutahakikisha tunachapisha maoni yao kwa kina kupinga
suala hili.
Absalom Kibanda,
Mwenyekiti wa Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam
Februari 15, 2013
No comments:
Post a Comment