Wednesday, June 18, 2025

MAJALIWA: FANYENI TAFITI ZENYE TIJA KWA WANANCHI







Dar es Salaam, 18 Juni 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa watafiti na wapangaji wa sera nchini kufanya tafiti zenye matokeo yenye tija kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuyatumia matokeo ya tafiti hizo badala ya kuyaacha kwenye makabati.

Akizungumza kwenye Kongamano la 13 la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Kampasi ya Mloganzila, Mhe. Majaliwa alisema matokeo ya tafiti yanapaswa kutumika katika kuandaa sera na mipango ya utekelezaji itakayochochea maendeleo ya kweli katika jamii.

“Tunahitaji kuona tafiti zetu zikisaidia kuimarisha mifumo ya afya, kutatua changamoto zilizopo na kuleta mageuzi chanya. Kongamano hili ni jukwaa muhimu la kutoa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili wananchi wanufaike kikamilifu na mapinduzi ya kisayansi,” alisema.

Aidha, aliwataka wadau wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika vifaa tiba na teknolojia za kisasa ili kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na changamoto za kiafya kwa wakati. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuwekeza kwenye miundombinu, rasilimali watu, huduma za kibingwa, na mifumo ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, salama na rafiki popote alipo,” aliongeza.

Mhe. Majaliwa pia alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, chanjo, na vifaa tiba ndani ya nchi. “Tayari tumeanza kushuhudia mafanikio ya hatua hizi, yakichochewa na mchango wa wataalamu wetu wa ndani.”

Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, Waziri Mkuu alieleza kuwa hospitali nyingi sasa zinatumia mifumo ya kidijitali kubaini magonjwa, kutoa tiba sahihi, na kufuatilia maendeleo ya wagonjwa, hatua inayoboresha kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma za afya nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu Prof. Daniel Mushi alisema Serikali imeweka kipaumbele katika kukuza elimu, sayansi na teknolojia, huku akieleza kuwa mageuzi makubwa yanaendelea chini ya uongozi wa Rais Samia, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi za elimu ya juu.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alieleza kuwa Serikali imekuwa mshirika mkubwa katika kufanikisha miradi ya kimkakati ya chuo hicho, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki (East African Centre of Excellence for Cardiovascular Sciences).

Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo iligharimu shilingi bilioni 21.62, huku awamu ya pili iliyozinduliwa Mei 2025 ikilenga kujenga Hospitali ya Kisasa ya Kufundishia wataalamu bingwa wa magonjwa hayo, kwa gharama ya shilingi bilioni 221.57.

Hospitali hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi kutoa huduma za kibingwa, kufundisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi, na kufanya tafiti mahsusi katika eneo la magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

No comments:

MAJALIWA: FANYENI TAFITI ZENYE TIJA KWA WANANCHI

Dar es Salaam, 18 Juni 2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa watafiti na wapangaji wa s...