Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (mwenye koti la suti) akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Pemba kwa ajili kuhuduria sherehe za uzinduzi wa Redio Jamii Mkoani jimbo la Mkanyageni, Kusini Pemba na kupokelewa na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Bw. Al Amin Yusuph (kulia) aliyeambatana na Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu (aliyeongoza mbele).
Na Mwandishi wetu, Pemba
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kwamba itaendelea kuruhusu kuanzishwa kwa Redio za jamii kutokana na umuhimu wake katika kuhimiza maendeleo na kutumika kama daraja kati ya wananchi na serikali yao.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa jamii, Vijana, wanawake na watoto, Zainab Omar Mohammed wakati akizundua kituo cha redio ya jamii jimbo la Mkanyageni, Mkoani Pemba.
Shughuli hiyo ambayo ilifanyika kama sehemu ya shamra shamra za sherehe za mapinduzi kutimiza miaka 51 zilihudhuriwa pia na wafadhili wa mradi huo ambao ni Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Waziri huyo alisema kwamba uzinduzi wa kituo cha redio ya jamii katika jimbo la Mkanyageni Mkoani Pemba ni moja ya azma ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapa haki wananchi wake ya kupata habari ikiwa ni sehemu muhimu sana ya maisha ya wanadamu.
Munekano wa sehemu ya jengo la Redio Jamii Mkoani jimbo la Mkanyageni Kusini Pemba kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Alisema habari ni kitu muhimu sana katika maisha ya sasa na wakati taifa likiadhimisha miaka 51 ya mapinduzi yaliyolenga kubadili maisha ya wazanzibari uwapo wa redio za jamii ni kitu ambacho kitasukuma mbele zaidi madhumuni ya mapinduzi , kumkomboa mzanzibari kiuchumi na kifikira.
“Redio hizi Jamii, zimewekwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa madhumuni ya kuwapa fursa wananchi kupata habari,kupata burudani, kupata elimu, lakini pia kutoa fursa ya kutoa mawazo yao kupitia redio hizi ili serikali ipate kujua zaidi nini hasa changamoto za wananchi na iweze kuzifanyia kazi kwa urahisi zaidi” alisema Waziri Zainab.
Pamoja na kuushukuru Umoja wa mataifa kwa kusaidia redio za jamii aliutaka Umoja huo uendelee kuimarisha uwezo wa redio hizo ili wananchi wazitumie kupata maendeleo.
Naye Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez amesema Umoja wa mataifa unajisikia fahari kuwezesha asilimia 60 ya wazanzibari kusikiliza redio za jamii na kuzitumia katika maendeleo yao.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez aliyeambatana na mkewe akisalimiana na Ofisa mdhani kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar na Mjumbe wa bodi ya usimamizi Redio Jamii Micheweni, Ali Mohamed mara baada ya kuwasili eneo la tukio.
Alisema umoja huo utaendelea na ushirikiano wake na serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuweka mazingira ya upatikanaji wa habari kuwa bora zaidi, ushirikiano ambao waliuanza mwaka 2008 wakati wa kutengeneza sera ya utangazaji.
Alisema ni sera hiyo iliyowezesha kuwepo kwa redio za jamii na utangazaji wa umma.
Alisema Redio za jamii ni msaada mkubwa katika kutoa elimu kwa jamii inayozunguka kituo hicho na kusema kwamba ni imani yake kituo cha Mkoani kitafanya kazi iliyokusudiwa kwa kuhamasisha mawazo chanya ya maendeleo na kuleta ushirikiano na amani inayotakiwa katika jamii.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Bw. Al Amin Yusuph wakipitia ratiba kabla ya kuanza rasmi sherehe za uzinduzi wa Redio Jamii Mkoani uliofanyika Kusini Pemba.
No comments:
Post a Comment