………………………………………………………………………………………..
Na Joachim Mushi
TAASISI ya HakiElimu imeukosoa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ‘Big Results Now’ (BRN) unaotekelezwa na Serikali katika sekta nyeti ikiwemo elimu kwa madai kuwa matokeo yake kwenye sekta ya elimu sio ya kuridhisha.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya tathmini ya kitaalamu iliofanywa katika utekelezaji wa BRN kweye sekta ya elimu.
Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha kuongezeka ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha ya ufaulu huu kuonekana kupanda ghafla kuna changamoto nyingi katika sekta ya elimu ambazo bado hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.
“…Mfano migogoro ya mara kwa mara kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu, ukosefu wa maabara, vifaa vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo katika gharama za utoaji elimu nchini kati ya shule za serikali na shule za binafsi. Mpango wa BRN ni mzuri lakini muda uliowekwa kutekeleza malengo yake ni mfupi kwa kuzingatia mazingira ya utoaji elimu na changamoto zake,” alisema Boniventura.
Kaimu huyo Mkurugenzi alibainisha kuwa kumekuwepo na mabadiliko ya mara kwa mara katika sekta ya elimu likiwemo la hivi karibuni la alama za ufaulu na mabadiliko ya viwango vya upimaji wa matokeo ya wanafunzi ambayo yameleta mabadiliko katika takwimu za ufaulu lakini yasitumike kama ishara ya kuimarika kwa ubora wa elimu itolewayo.
Aidha aliongeza kuwa matokeo mazuri yoyote ya mipango ya maendeleo ikiwemo elimu yanahitaji uwekezaji wa kutosha, ilhali shule za msingi na sekondari zina changamoto nyingi za upungufu wa miundombinu jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kiufasaha zaidi tofauti na inavyofanyika sasa.
“…Serikali haina budi kutafakari na kuona kama uwekezaji uliofanyika mpaka sasa umefanyika kiasi cha kutosha kuleta matokeo kusudiwa. Hali ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu si nzuri ambapo asilimia 24 tu ya fedha ya bajeti inapangwa kwenye miradi ya maendeleo inayohusu miundominu ilihali matumizi ya kawaida yakiwa asilimia 74 ya bajeti ya elimu,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema sekta ya elimu malengo yaliyopangwa kutekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja 2013/2014, ni pamoja na;- Kuongeza ufaulu kufikia asilimia 70 mwaka 2014; kutoa ruzuku iliyopangwa kwa kila mwanafunzi, kutoa mafunzo ya uongozi kwa walimu 19,035 kufikia Septemba 2013, lakini kwenye uhalisia hali hairidhishi.
Alisema BRN ilipanga pia kutoa mafunzo kwa waalimu 12,300 juu ya ufundishaji wa KKK, kujenga nyumba za walimu 500 kwa shule za sekondari, kukarabati miundombinu kwa shule 1,200 za sekondari na kuhakikisha kuwa uwino wa mwanafunzi kwa kitabu unashuka kutoka kitabu kimoja kwa wanafunzi watano hadi vitabu sita kwa mwanafunzi mmoja lakini hakuna mafanikio ya kuridhisha.
“…HakiElimu imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa BRN katika sekta ya elimu kwa karibu sana na kubaini kuwa hali ya utekelezaji wake bado si ya kuridhisha.
Mathalani, BRN ilipanga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za sekondari na msingi hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2013, na asilimia 70 mwaka 2014.”
Mathalani, BRN ilipanga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za sekondari na msingi hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2013, na asilimia 70 mwaka 2014.”
“Pamoja na matokeo kuonesha ongezeko la ufaulu, kutoka asilimia 50.6 Mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 58 mwaka 2013 kwa sekondari na kutoka 30.7 mwaka 2012 hadi 50.6 Mwaka 2013 kwa shule za msingi, bado lengo la asilimia 60 halikufikiwa.”
“…Hii inamaanisha lengo la ufaulu kwa sekondari kufikia asilimia 60 kwa mwaka 2013 limefanikiwa kwa asilimia karibu 79 na kwa asilimia 42 tu kwa shule za msingi. Hatahivyo ufaulu wa sekondari si wa kujivunia kwa sababu matokeo ya mtihani wa mwaka 2013 yametumia viwango vipya vya madaraja, na hivyo hatuwezi kusema yametokana moja kwa moja na utekelezaji wa BRN,” alieleza Boniventura kwa wanahabari.
Hata hivyo alishauri ili kutekeleza Matokeo Makubwa Sasa hatuna budi kujifunza toka kwa nchi zilizofanikiwa kutekeleza mipango kama Malaysia kwamba; Matokeo Makubwa Sasa maana yake ni viongozi kufanya tofauti na wafanyavyo sasa, kuwajibika kwa hali ya juu, viongozi kuwa wabunifu, viongozi kupanga mipango na kuitafutia fedha za utekelezaji, viongozi kufanya kazi na kutenda ili kutekeleza ahadi zao ili kupata matokeo ya haraka.
Mwaka 2013 serikali ya Tanzania ilizindua mpango maalumu wa ufuatiliaji utekelezaji wa mipango na utoaji huduma kwa umma unaojulikana kama BRN huku lengo la mpango likiwa kusukuma maendeleo na kuharakisha utekelezaji mipango na kuleta matokeo yaliyokusuduwa upesi..
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment