Monday, January 19, 2015

WAKAZI WA WILAYA YA ILALA WALALAMIKIA MKANDARASI WA UJENZI WA DARAJA LA MAGOLE

index

WAKAZI wa Kata Kibeberu na Magole, Kata ya Kitunda, Manispaa ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam wamemlalamikia mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Magole kwa kushindwa kukamisha ujenzi wa daraja hilo hadi sasa.Aidha wakazi hao wamesema pamoja na daraja hilo kuchelewa kukamilika pia kwa mtazamo wao wanaamini kuwa lipo chini ya viwango ambavyo vinatakiwa.Mjumbe wa Kamati ya Ujenzi wa daraja hilo Samir Ibrahim alisema daraja hilo lnatakiwa kukamilika ifikapo Februari mwaka huu lakini hadi sasa hakuna dalili za kukamilika kwake.
Ibrahim alisema pamoja na kuchelewa kukamilika kwa daraja hilo pia wamejaribu kutoa ushauri kuwa urefu wa daraja hilo hautaweza kuhimili maji mengi ambayo yanapita hasa wakati wa mvua.
Mjumbe huyo alisema jambo lingine ambalo linawatia shaka kwa kutodumu kwa daraja la Magole ni pamoja na aina ya nondo zinazotumika ni ishara tosha kuwa haliwezi kudumu kwa muda mrefu.
“Mimi ni mjumbe wa kamati ya ujenzi lakini
kusema ukweli hali ya ujenzi wa daraja hili naitilia shaka sana sidhani kuwa litadumu na ukiangalia mto huo ni mkubwa sana unahitaji daraja la viwango,” alisema.
Ibrahim alisema pamoja na jitihada zao za kutoa taarifa za hali ya daraja hilo kukosa ubora hakuna juhudi zozote ambazo zimechukuliwa na Serikali kufuatilia.
Kwa upande wake Aisha Athuman alisema iwapo daraja hilo la Magole halitakamilika kwa wakati ni wazi kuwa watoto na mama wajawazito wataathirika kwa kiwango kikubwa.
Athman alisema daraja hilo likipitisha maji watoto hawaendi shule jambo ambalo linawaathiri kitaaluma.
“Unajua hapa njia ya kuendea shule ya Msingi Magole ni moja tu hivyo iwapo hali ya daraja kutokamilika ka wakati itaendelea ni dhahiri kuwa madhara yataongezeka,” alisema Athuman.
Akizungumzia adha hiyo Mwendesha Boda Boda Mbonamengi Charles alisema kinachoonekana ni Serikali kuwasahau wakazi wa pembezoni hali ambayo inafifisha maendeleo.
Charles alisema kutokana na kutokamilika kwa daraja hilo mambo mengi ya maendeleo yamekuwa yakikwama kutokana kero ya eneo hilo.
Aidha Mkazi huyo alihoji kuwepo kwa vifusi kwa muda mrefu ambavyo vimewekwa barabarani bila kusambazwa huku wakiwa wameahidi kwa muda mrefu kuwa vitasambazwa.
Diwani wa Kata ya Kitunda Daniel Julias alipotakiwa kuelezea tatizo hilo la daraja kuchelewa alisema sababu kubwa ni ukosefu wa fedha.
Alisema mkataba kati ya Manispaa na Mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kuisha mwezi Februari hivyo anachoamini ni kuwa wakati huo ukifika hatua zingine zitachuliwa.
Diwani huyo alisema suala la vifusi kutosambazwa linatokana na maagizo yake kuwa visubiri daraja litakapo kamilika.
Julias aliwataka wakazi wa Magole kuwa wavumilivu kwani Serikali yao inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa changamoto mbalibali zinatatuliwa kwa wakati.
Mwisho.

No comments: