Tuesday, January 27, 2015

WAZIRI MAGUFULI AZINDUA MIRADI SITA YA UJENZI WA BARABARA ZA KUPUNGUZA MSONGAMANO KATIKA JIJI LA DAR


Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akiweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara ya Mbezi mwisho-Goba- Tangi Bovu.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akiweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara ya External –Kilungule.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akiweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara ya Msewe-Baruti
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akipiga tumba huku Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akicheza kuashiria furaha yao kabla ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Mbezi mwisho-Goba- Tangi Bovu.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kushoto akiwa na mbunge wa Kawe Mheshimiwa Halima Mdee pamoja na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Ramadhan Madabida kulia wakifurahia mara baada ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Mbezi mwisho-Goba –Tangi bovu.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akisalimiana na wananchi kabla ya uzinduzi wa miradi hiyo ya kupunguza msongamano.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akiwashika mikono Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mheshimiwa John Mnyika pamoja na mbunge wa Kawe Mheshimiwa Halima Mdee mara baada ya kuzindua mitambo itakayofanya kazi katika ujenzi wa barabara ya Mbezi mwisho-Goba –Tangi bovu.
Mbunge wa Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akizungumza jambo na Waziri wa Ujenzi katika shule ya Msingi Msewe.
Uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Kigogo-Tabata dampo.
Taaswira ya barabara ya Mbezi mwisho-Goba-Tangi bovu eneo la Goba ambalo limeshajengwa kwa kiwango cha lami. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Ujenzi. 

Waziri wa Ujenzi Mheshimkiwa Dkt.John Pombe Magufuli leo amezindua na kuweka  mawe ya msingi katika Ujenzi wa barabara za pete zitakazopunguza msongamano jijini Dar es salaam.

Barabara hizo zilizowekewa mawe ya msingi ni pamoja na ile ya  Kinyerezi –Kifuru hadi Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilometa 14.0, Kigogo-Tabata Dampo yenye urefu wa kilometa 1.6, na Kimara Baruti-Msewe hadi Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 2.6.

Barabara nyingine ni ile ya External –Kilungure hadi Kimara Korogwe kilometa 8.0, Wazo Hill-Goba hadi Mbezi mwisho kilometa 20 na Goba-Tangi bovu kilometa 9.0.

Akizungumza wakati akizindua ujenzi wa barabara hizo Waziri Magufuli amewataka wananchi kufuata sheria za barabarani kwa kutoingilia hifadhi za barabara na wale wenye nyumba pembeni mwa barabara kuzibomoa wenyewe ili kupisha ujenzi huo kwenda kwa wakati.

“Nawahakikishieni kwamba mkifuata sheria za kutojenga karibu na barabara barabara hizi zitajengwa kwa kiwango cha lami na kwa wakati ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu na ninyi mtanufaika na fursa za kibiashara kwa kuwa karibu na barabara za lami na hivyo kujikwamua kiuchumi”,amesisitiza Waziri Dkt. Magufuli.

Waziri Magufuli amesema barabara ya Wazo HilL –Goba yenye urefu wa kilometa 20 ikikamilika kwa kiwango cha lami itaziunganisha barabara za Bagamoyo na Morogoro ambazo zimekuwa zikikabiliwa na msongamano kwa muda mrefu.

Aidha, amesema barabara ya Kinyerezi- Kifuru hadi Mbezi mwisho yenye urefu wa kilometa 14 itapunguza pia msongamano kwa kiasi kikubwa kwa kuwa itakuwa inaunganisha barabara ya Morogoro na Nyerere hivyo kuwataka wananchi kuanza kuzitumia barabara hizo ambazo zitakamilika kwa wakati.

Amewataka vijana wanaopata fursa za ajira katika ujenzi wa barabara hizo kuwa waadilifu,waaminifu na wachapa kazi na kujiepusha na vitendo vya wizi vitakavyosababisha kuongeza gharama za ujenzi wa barabara hizo.

“Kumbukeni mkiiba vifaa vya ujenzi hamuibi vifaa vya kampuni zinazojenga bali mnajiibia wenyewe kwa sababu hizi ni fedha za kodi ya wananchi bali kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kutawezesha ujenzi wa barabara kukamilika kwa wakati na ninyi kujihakikishia uhakika wa ajira”,alisema Waziri Magufuli.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam mheshimiwa Said Meck Sadik amezungumzia umuhimu wa wakazi wa jiji la Dar es salaam kutunza barabara kwa kutofanya biashara kwenye hifadhi za barabara na kuahidi hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaokiuka taratibu za kisheria na kutupa takataka katika mitaro ya barabara.

Amewataka wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam na wabunge wengine wanaoishi mkoani  Dar es salaam kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa barabara jijini Dar es salaam ili kuhakikisha Wizara ya Ujenzi inamudu kuzijenga barabara za pembezoni zitakazopunguza msongama na kuliwezesha jiji la Dar es salaam kupitika wakati wote.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini  (TANROADS), Eng.Patrick Mfugale ameiomba Serikali kuongeza bajeti ya barabara ili kuwezesha Miradi ya barabara kukamilika kwa wakati na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili barabara zijengwe kwa kiwango kilichokubalika katika mikataba.

Ziara hiyo ya Uzinduzi wa barabara za pete imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa jiji la Dar es salaam akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Bw.Ramadhani Madabida,Mbunge wa Ubungo Mheshimiwa John Mnyika,Segerea-Dkt Makongoro Mahanga,na Kawe mheshimiwa Halima Mdee ambapo kwa pamoja wamekubaliana kushirikiana ili Wizara ya Ujenzi ipate fedha za kukamilisha miradi hiyo itakayopunguza kwa kiasi kikubwa kero ya msongamano jijini Dar es salaam.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...