Tuesday, March 18, 2014

TASWIRA ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA BAADA YA HALI YA HEWA KUCHAFUKA SIKU YA JANA



Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa 11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema: “Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.
Waliokuwa mstari wa mbele kupinga Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa sehemu kubwa walikuwa ni wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Jaji Warioba akiwa anatafakari mbele ya mimbari, Sitta aliwasha kipaza sauti na kumtaka aendelee kuwasilisha Rasimu ya Katiba ... “Endelea Mwenyekiti, endelea kwa ajili ya kumbukumbu rasmi (hansard).”
Lissu akisikika akijibu kauli hiyo akisema: “Fuata kanuni mwenyekiti... fuata kanuni mwenyekiti,… huku akipiga kelele na kugonga meza na wakati huo Profesa Lipumba akiwa amewasha kipaza sauti chake kutaka kuzungumza huku naye akiendelea kupiga meza kwa nguvu.
Wengine waliosimama ni Mchungaji Christopher Mtikila, Ezekiel Oluoch, Philimon Ndesamburo, Moses Machali na Mchungaji Peter Msigwa.
Dakika tatu zilikatika huku kukiwa hakuna dalili za hali kutulia na kuona hivyo, Jaji Warioba aliamua kuondoka kwenye mimbari na kuketi kimya akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhani.
Baada ya hapo, Sitta alisimama na kuwasha kipaza sauti na kusema: “Waheshimiwa wajumbe, katika mazingira haya tuliyonayo, naomba kutangaza kuwa nasitisha shughuli za Bunge hadi hapo tutakapotangaziwa tena.” SOURCE: MWANANCHI

No comments: