Toka awasilishe rasimu ile bungeni , kumekuwa na maombi mengi sana ya kutaka kujua kama msimamo wa CCM juu ya baadhi ya mambo hasa muundo wa muungano bado ni uleule.
Kwasababu ya maombi hayo CCM imeona bora kueleza kwa mara nyingine tena msimamo na imani ya CCM juu ya swala zima la Muungano na muundo wake.
Kimsingi CCM ndio waasisi wa Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar. CCM inamasilahi makubwa na mapana na Muungano huu kama waasisi pengine kuliko taasisi nyingi ndani na nje ya nchi yetu.
Bado CCM inaamini changamoto za Muungano huu suluhisho lake sio kubadili muundo wa Muungano bali ni kuufanyia maboresho muundo wa muungano tulionao wa serikali mbili. Hivyo basi CCM bado inaamini muundo bora kwasasa utakao dumisha muungano wetu ni muundo wa SERIKALI MBILI.
Kwakuwa kazi ya Warioba na Tume yake sasa imekwisha rasmi, kuisha kwa kazi yao ni mwanzo wa awamu nyingine ya mchakato huu. Mwisho wa kazi ya Tume sio mwisho wa mjadala juu ya Katiba tuitakayo bali ni mwanzo wa awamu nyingine ya mjadala mpana na maboresho kama sio marekebisho ya kuondoa mapungufu kwenye rasimu iliyowasilishwa.
Mwanzo wa awamu hii nyingine ni furusa nzuri ya kupima kama kweli yaliyomo kwenye rasimu na maelezo ya ziada yaliyotolewa na Jaji Warioba yana akisi maoni ya Watanzania walio wengi.
CCM ina amini awamu mbili zilizobaki kwakuwa zinahusisha wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge maalum la Katiba, na hatimaye itawahusisha wananchi wenyewe moja kwa moja kupitia kura yao, zitatumika vizuri kutupa ni nini hasa matakwa ya Watanzania juu ya Katiba waitakayo na sio maoni au matakwa ya wachache.
Wakati haya yote yakiendelea CCM bado tunaamini Muungano huu ni muhimu ukadumishwa na kuimarishwa. CCM tunaaamini ili Muungano huu udumu njia pekee kwasasa ni kufanya marekebisho kwenye Muundo wa serikali mbili ili ujibu vizuri zaidi changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na kukidhi mazingira ya sasa.
Tunawaomba wanaCCM na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi hiki. Ni vizuri Watanzania tukavumiliana,tukashindana kwa hoja tukitanguliza mbele uzalendo na masilahi ya kweli ya nchi yetu.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi
20/03/2014
Comments