Mgeni rasmi Jaji wa Mahakama ya Rufani, Edward Rutakangwa (katikati) akiwasili kufungua rasmi mafunzo ya siku nne juu ya sheria za kimataifa za kazi kwa majaji na wasajili wa mahakama nchini yalioandaliwa na Shirika la Kazi Duniani mjini Bagamoyo. Kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la kazi duniani kwenye nchi nne Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Alexio Musindo.
Na Damas Makangale, Bagamoyo, MOblog Tanzania
JAJI wa Mahakama ya Rufani, Tanzania, Edward Rutakangwa amesema bado kuna upungufu mkubwa wa majaji katika mahakama za Tanzania kiasi cha kusababisha mrundikano wa kesi katika mahakama hapa nchini. MOblog inaripoti.
Akifungua rasmi mafunzo ya siku nne kwa majaji, wasajili na wasajili wasaidizi wa Mahakama ya Kazi, Jaji Rutakangwa amesema kwamba pamoja na Mheshimiwa wa Rais kuteua majaji bado kuna upungufu mkubwa wa majaji nchini.
“Tatizo la majaji kuwa wachache ni la muda mrefu pamoja na juhudi za Mheshimiwa rais kupunguza ukubwa wa tatizo kwa minajili ya kuleta ufanisi katika idara ya mahakama,” amesema Jaji Rutakangwa
Amesema mafunzo hayo ya siku nne yataleta matokeo mazuri kwa majaji na wasajili wa mahakama katika kuleta haki kwa wafanyakazi na kufanya kazi kwa viwango vya kimataifa vya kazi duniani.
Jaji Rutakangwa alilisisitiza kwamba kuna umuhimu wa majaji kujua haki na sheria za kazi kwa hiyo mafunzo hayo yatatoa fursa kwao kuelewa sheria za kazi ili kuwawezesha kutoa hukumu kwa kuzingatia sheria na haki za wafanyakazi nchini.
Amesema kuna umuhimu wa majaji na wasajili wa mahakama kuelewa kwa kina sheria za kimataifa za kazi na jinsi ya kuzitumia katika mahakama za ndani ya nchini.
Kwa upande, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la kazi Duniani, Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda, Alexio Musindo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa walifanya mabadiliko kadhaa ya kijamii na kiuchumi.
Amesema moja ya mipango ya serikali hizo mbili ni kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya soko huria pamoja na kuweka vyombo vya kudhibiti soko hilo kama vile Mahakama ya kazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
“Shirika la kazi duniani litaendelea kufanya kazi kwa karibu na mahakama ya kazi pamoja na Tume Usuluhishi katika kuleta ufanisi katika sekta ya kazi kwa kujali maslahi ya wafanyakazi katika maeneo ya kazi duniani,” amesema Musindo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Edward Rutakangwa akifungua rasmi mafunzo ya siku nne juu ya sheria za kimataifa za kazi kwa majaji na wasajili wa mahakama nchini yalioandaliwa na Shirika la Kazi Duniani mjini Bagamoyo.
Musindo amesema katika mafunzo hayo yatatoa fursa kwa majaji na wasajili wa Mahakama kujifunza sheria za kimataifa za kazi na utatuzi wa migogoro katika sehemu za kazi.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), Nicholas Mgaya amesema kwa kuwa sheria ya kazi ni mpya ya mwaka 2004 bado kuna majaji na wasajili wa mahakama haifahamu vya kutosha ili kukidhi haya ya jamii.
Amesema mafunzo hayo ya siku nne ni fursa pekee kwa majaji na wasajili wa mahakama kujifunza sheria za kimataifa za kazi ili kuleta tija katika maamuzi yao mbalimbali.
Baadhi ya majaji na wasajili wa mahakama nchini wanaohudhuria mafunzo ya siku nne juu ya sheria za kimataifa za kazi yalioandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mjini Bagamoyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la kazi duniani (ILO) kwenye nchi nne Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Alexio Musindo akizungumza na washiriki kwenye mafunzo hayo mjini Bagamoyo.
Jaji Regina Rweyemamu kutoka Mahakama ya kazi, akizungumza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kama majaji katika mahakama za kazi nchini.
Baadhi ya majaji na wasajili wa mahakama nchini wakifuatilia yanayojiri kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku nne yaliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) yanayoendelea mjini Bagamoyo.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), Bw. Nicholas Mgaya akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo ya siku nne kuhusu changamoto katika mahakama za kazi, upungufu wa majaji na vitendea kazi kama moja ya vitu vinavyochangia mrundikano wa kesi katika mahakama hapa nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri (ATE) Wakili, Cornelius Kariwa akitoa hotuba yake kwa niba ya chama cha waajiri nchini umuhimu wa kufahamu sheria za kimataifa za kazi duniani.
Baadhi ya wasijili wa Mahakama ya kazi wakiwa kwenye mafunzo ya siku nne yanayoendelea mjini Bagamoyo.
Mgeni rasmi Jaji wa Mahakama ya Rufani, Edward Rutakangwa (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la kazi duniani (ILO) kwenye nchi nne Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bw. Alexio Musindo wakati wakielekea kupiga picha ya pamoja. Kulia ni Afisa Mipango mwandamizi wa shirika la kazi duniani (ILO) Anthony Rutabanzibwa.
Mgeni Rasmi Jaji wa Mahakama ya Rufani, Edward Rutakangwa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo ya siku nne yanayoendelea mjini Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment