Wanafunzi walioongoza mtihani wa taifa wa darasa la saba wa mwaka 2012,
Janeth Kijazi (kushoto) Justina Kalala (katikati)na Kellen Mudogo wakiwa
shule ya sekondari ya wasichana, St Marian Bagamoyo, jana, walikoanza
kidato cha kwanza. Wanafunzi hao walihitimu elimu ya msingi katika Shule
ya Tusiime ya jijini Dar es Salaam. Picha Florence Majani
wa MWANANCHI
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
Florence Majani
WANAFUNZI walioongoza mtihani wa Darasa la
Saba kitaifa mwaka jana, ni wasichana watatu waliokuwa wanasoma katika
Shule ya Msingi Tusiime iliyoko Dar es Salaam, imefahamika.
Wasichana hao, Justina Kalala, Janeth
Kijazi na Kellen Mudogo waliongoza mtihani huo wenye masomo matano kwa
kila mmoja kupata alama 234 kati ya 250.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, mabinti
hao ambao wote wanasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Marian, Bagamoyo, walisema siri ya mafanikio yao ni maombi
na nia ya kutaka kufaulu.
Justina alisema siri ya kufaulu mitihani yake
ni kumtanguliza Mungu kabla hajafanya kitu chochote hata kama ni
majaribio ya kawaida darasani... “Pia elimu bora ninayopewa na wazazi
wangu nayo inanipa nguvu ya kusoma kwa bidii.”
Justina alisema siri nyingine ya kufaulu kwake
katika mitihani hiyo ni kusoma na kisha kuwafundisha wenzake kile
alichokielewa. Alisema jambo hilo lilimjengea uwezo wa kuyashika yale
aliyoyasoma.
“Nilikuwa nawakusanya wenzangu katika makundi ili tusome.”
Mwanafunzi
huyo ambaye alipokuwa shule ya msingi aliteuliwa kuwa mratibu wa
taaluma kutokana na kuwaongoza wenzake katika vikundi vya kujisomea,
alisema anatamani kuwa mfamasia pindi atakapofanikiwa kumaliza masomo
yake na kufaulu.
Pia, Janeth ambaye alisema ufaulu wake
ulimtegemea zaidi Mungu, anapenda zaidi masomo ya sayansi... “Nataka
kuwa daktari ndiyo maana najitahidi zaidi katika masomo ya sayansi.
Nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa naweka juhudi zaidi katika somo la
hesabu na baiolojia.”
Alisema alipokuwa msingi, alikuwa ni kiongozi
wa kikundi cha kujisomea na alikuwa anatumia muda wake mwingi kusoma
vitabu na kuwauliza walimu kile ambacho alikuwa hakijui.
Kwa upande wake, Kellen mbali na kusema kwamba
anamtegemea Mungu zaidi katika masomo yake, alitoa siri nyingine ya
kushinda katika mtihani huo kuwa ni kurudia kile walichofundishwa na
kutumia vyema muda wake.
Kellen alisema anapenda masomo ya sayansi na anatamani kuwa daktari endapo atafaulu masomo yake ya Chuo Kikuu.
Walikuwa na msukumo
Aliyekuwa mwalimu wa
darasa wa wanafunzi hao huko Tusiime, Valentine John alisema wanafunzi
hao walikuwa na msukumo wa ndani wa kusoma tofauti na wengine.
“Pia
wameandaliwa vyema tangu chekechea ndiyo maana wamefanya vizuri, sisi
haitushangazi wao kuongoza kwa sababu tuliujua ubora wao tangu zamani,”
alisema.
Mwalimu huyo alisema wanafunzi hao watatu walikuwa si wakorofi, bali wasumbufu kwa walimu katika mambo wasiyoyajua.
Comments