UANZISHWAJI WA WAKALA WA KUSIMAMIA UENDELEZAJI WA MJI MPYA KIGAMBONI (KIGAMBONI DEVELOPMENT AGENCY)

IMG_1724Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya New Africajijini Dar es salaam  leo wakati alipotangaza rasmi kuanzishwa kwa Wakala wa kusimia maendeleo ya mji wa Kigamboni inayoitwa Kigamboni Development Agency (KDA) Kushoto ni Christian Mwangaja Kaimu Kamishna mambo ya Ardhi na katikati ni Sellasie Mayunga Upimaji na Ramani.
1. Serikali imedhamiria kujenga Mji Mpya Kigamboni katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, Dhana ya mji mpya Kigamboni ni kuwa na mji wa kisasa ambao ni kitovu cha kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jiji la Dar es Salaam ili liweze kushindana na miji mingine duniani katika kuvutia uwekezaji, biashara na utalii na kukuza ajira, hasa kwa vijana. Ujenzi wa mji mpya ni hatua mojawapo katika mkakati wa serikali wa kukabiliana na changamoto za ukuaji wa jiji la Dar es Salaam.
 2. Tarehe 18 January, 2013 Serikali ilianzisha kisheria wakala maalumu, Kigamboni Development Agency (KDA) itakayosimamia uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni kama Mamlaka ya Upangaji Mji (Planning Authority). Eneo litakalosimamiwa na KDA lina ukubwa wa hekta 50,934 na linahusisha Katat za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila, Kisarawe II, Kimbiji na Pemba Mnazi . katika kusimamia uendelezaji huo, KDA itaongozwa na mpango kabambe. Rasimu ya mpango huo imekwishaandaliwa kwa baadhi ya kata.
 3. Uendelezaji wa Mji Mpya utagharimiwa na Serikali pamoja na sekta binafsi kwa kutumia fedha zilizo ndani na nje ya bajeti rasmi ya serikali. Utaratibu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public Private Partnership) utatumika. Aidha, mbinu za kisasa za kupata fedha kama vile kuuza hisa na kutoa hatifungani (bonds) zitatumika.
 4. Ili kutekeleza kusudio la kuendeleza eneo la Kigamboni, hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na:-
    1. Kutoa elimu kwa umma juu ya manufaa ya kuendeleza eneo la Kigamboni na taratibu za uendelezaji.
    1. Kutafuta fedha za kutosha kutekeleza mradi.
    1. Kupima maeneo husika na kuyaandaa kwa ajili ya uendelezaji.
    1. Kujenga nyumba mpya za kuishi kwa ajili ya kuwahamishia wananchi ambao makazi yao yataathiriwa na ujenzi wa Mji Mpya; na
    1. Kufanya uthamini wa mali na kuwafidia wananchi watakaolazimika kahama kutokana na ujenzi wa mji.
5. Muundo wa KDA unatokana na Sheria ya Wakala za Serikali ya mwaka 1997. wakala itaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji na Wakurugenzi sita ambao watakuwa Wakuu wa Idara, KDA itasimamiwa na Bodi ya Ushauri pamoja na Baraza la Ushauri ambalo  litakuwa na wajumbe wanaowawakilisha wadau wote, hususan Wabunge na Madiwani waeneo litakaloendelezwa na KDA.
6. Matokeo ya utekelezaji wa Mpango kabambe wa Mji Mpya ni kama ifuatavyo:
    1. Kuwa na mji uliopangwa kwa kiwango cha kimataifa utakaokuwa mfano wa kuigwa na miji mingine nchini.
    1. Kupunguza ujenzi holela;
    1. Kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na shughuli za kiuchumi na kijamii kama vile za viwanda , hotel, utalii, biashara, elimu, ofisi, afya na vituo vya michezo;
    1. Kupunguza msongamano wa magari na huduma za kiuchumi na kijamii katikati ya jiji la Dar es Salaam;
    1. Kuongezeka kwa thamani ya ardhi katika maeneo ya mji kutokana na kuboreshwa kwa miondombinu ya barabara, maji na umeme itakayowezesha kukuza biashara, ujenzi wa majengo na viwanda.
    1. Kuhamasisha uwekezaji ili kuongeza ajirra, has kwa vijana; na
    1. Wananchi  wengi wataweza kumiliki nyumba katika maeneo yaliyopangwa na kutumia nyjmba zao kupata mikopo kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali.
 Taarifa na elimu kwa umma kuhusu hatua zote za uendelezaji wa mji  zitaendelea kutolewa na Wizara pamoja na KDA kwa njia mbalimbali (k.m. kupitia mikutano maalum, vyombo vya habari na vipeperushi).
 Prof. Anna K. Tibaijuka (Mb)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
23 January, 2013

Comments