Mkurugenzi
wa Huduma za Usafiri wa Wizara ya Uchukuzi, Peter Lupatu, akikata utepe
kuzindua Safari za Ndege za Shirika la Precision Air za Mbeya kupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Precision Air, Michael Shirima.
Mkurugenzi
wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi, Peter Lupatu, akishuka
kutoka katika ndege ya shirika la Precision Air wakati wa uzinduzi wa
Safari za Mbeya – Dar kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe
kabla ya kukata utepe kuzindua safari hizo. Nyuma yake ni Mwenyekiti wa
Bodi ya shirika hilo, Michael Shirima.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Precision Air (PW), Michael Shirima, (Kushoto) akiteta jambo
na abiria wa kwanza kununua tiketi ya safari ya Mbeya wakati wa
uzinduzi wa Precision Air wa njia ya Mbeya – Dar, Bw. Alfred Mwambeleko Jumatano hii.
Mzee
akisaidiwa kupanda ndege, ambaye ni mkazi wa mkoani Mbeya wakati wa
uzinduzi wa Safari za Ndege za Shirika la Precision Air za Mbeya – Dar
uliofanyika Jumatano hii kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe
uliofanyiwa marekebisho kutumika kwa safari za kimataifa.
========= =============== =========
Shirika la ndege la Precision Air yazindua safari za Mbeya
SHIRIKA
la ndege la Precision Air (PW) jana lilizindua safari zake za mkoani
Mbeya, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ambao umekamilika
kukarabatiwa hivi karibuni na kuuwezesha utumike katika safari za
kimataifa.
Huu
ni ujio mpya wa safari za shirika hilo ambapo walikuwa wanaruka kuenda
mkoani Mbeya kati ya miaka ya 1997 hadi 2000 wakitua kastika uwanja
mdogo uliopo katikati wa mji wa Mbeya.
Uzinduzi
ambao ulifanywa na Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi, Peter Lupatu kwa
niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, na kuhudhuriwa na
wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri wa anga ulifanyika katika uwanja wa
ndege wa Songwe, ambapo wakazi wa Mbeya walielezea furaha yao juu ya
uzinduzi huo.
Shirika
hilo lilitumia ndege yake aina ya ATR-72 yenye uwezo wa kubeba abiria
70, katika kuzindua njia hiyo mpya, kwa kuanza na ratiba ya kuruka Mbeya
mara nne katika wiki (Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili) kwa nauli
ya shilingi 249,000/= kwa tiketi ya kwenda na kurudi na shilingi
165,000 /= kwa tiketi ya njia moja, zikijumuisha kodi na gharama
nyinginezo.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Lupatu alisema kuwa hatua iliyochukuliwa na
Precision Air itauwezesha mkoa wa Mbeya na majirani zake kuwa na fursa
nyingi za kibiashara na maendeleo kwa upatikanaji wa usafiri wa anga
katika eneo hilo.
“Natoa
wito kwa wakazi wa Mbeya na majirani zake kutumia fursa hii kikamilifu
iliyotolewa na Precision Air baada ya kuanzisha safari zake za
kibiashara katika mkoa huu. Hii ni hatua kubwa kwa mkoa na sekta ya
usafiri wa anga nchini.
“Uwepo
wa usafiri wa uhakika wa ndege tunaouanzisha leo hii unaonyesha kwamba
Mbeya na mikoa ya jirani sasa itapata fursa kubwa za kibiashara pamoja
na kuunganishwa na miji mikubwa ya kibiashara na miji mingine duniani.
“Kuanzishwa
kwa njia hii mpya itakuwa ni chachu ya ukuaji mkubwa wa shughuli
mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huu ambazo ni pamoja na kilimo cha
mbogamboga na maua, kwa kuwa sasa wakulima wanauhakika wakusafirisha
mazao yao kwa wakati katika masoko yanayostahili,” alisema.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Precision Air, Michael Shirima,
aliiomba serikali kutafuta mwekezaji ambaye atawekeza katika uuzaji wa
mafuta ya ndege katika uwanja wa ndege wa Songwe ili kuwasaidia
wawekezaji katika sekta ya usafiri wa anga kupunguza gharama za
uendeshaji.
“Ombi
langu kwa serikali ni kuhakikisha kuwa kunakuwepo na upatikanaji wa
mafuta ya ndege ya kutosha katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Songwe. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji
kwa mashirika ya ndege. Kwa sasa, tunalazimika kubeba mafuta ya akiba
ambayo huongeza mzigo katika ndege, hivyo inatulazimu kubeba abiria
wachache na kuacha nafasi kwa ajili ya mafuta ya akiba, “alisema Bw
Shirima.
Muasisi
huyo wa PW pia aliiomba serikali kuhakikisha kuwa uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Songwe unakuwa na vifaa bora vya kuongozea ndege kutokana
na eneo lilikojengwa ili kulinda usalama wa ndege na abiria wake. Pia
aliiasa serikali kufunga rada katika uwanja huo wa ndege, kama ilivyo
katika viwanja vingine vya kimataifa.
Aliwahakikishia
wakazi wa Mbeya kwamba shirika katika siku za usoni litaongeza idadi ya
safari zake za Sogwe endapo abiria wa kwenda na marudio itaongezeka.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Norman Sigala akizungumza
wakati wa kuwakaribisha wageni alisema kuwa anafuraha na uamuzi wa
Precision Air wa kufika mkoani Mbeya kwa kuwa jitihada hizo zitapunguza
changamoto za usafiri kwa wakazi wa mkoa huo za usafiri hususani usafiri
wa Dar es Salaam na kuungana na miji mingine duniani.
“Uzinduzi
tunaoushuhudia leo ni wa baraka kubwa kwa Mkoa wa Mbeya na majirani
zake. Napenda kuwahakikishia wakazi wa Mbeya kuwa Mbeya ya leo haifanani
na Mbeya ya jana na ya siku zijazo. Kwa kuwa Precision Air imezindua
safari zake kwa mkoa huu, utaona mashirika mengi ya ndege yakileta ndege
zao hapa. Uwepo kwa usafiri wa anga sasa kutafanya ndoto zetu za
kuendeleza kilimo cha mbogamboga na matunda katika mkoa wetu kufanikiwa.
Shughuli zaidi za kiuchumi sasa zitafanyika katika mkoa na hivyo
kuwainua watu wetu kiuchumi,” alisema.
No comments:
Post a Comment