Tuesday, January 08, 2013

PRECISION KUANZA SAFARI ZA DAR - MBEYA WIKI IJAYO

  Mkuu wa Idara ya Masoko na Uhusiano wa Shirika la Ndege la Precision, Linda Chiza akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa safari za ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya zitakazoanza wiki ijayo. Kushoto ni Meneja Mauzo, Tuntufye Mwambusi na kulia ni Meneja Mpangomkakati wa shirika hilo, Lilian Massawe.
*******
Shirika la Ndege la Precision linatarajia kuzindua safari za kwenda mkoani Mbeya kuanzia wiki ijayo, baada ya matengenezo ya Uwanja wa Ndege wa Songwe kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uhusiano wa shirika hilo, Linda Chiza alisema baada ya uzinduzi huo, abiria wake watahudumiwa na ndege aina ya ATR-72 ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 70.

Alisema kwa mujibu wa ratiba ya shirika, wamepanga kuruka mara nne kwa wiki kwenda Mbeya kutokea Dar es Salaam, kwa kuanzia na kadri njia hiyo itakapo imarika, wataongeza safari za kwenda na kutoka Songwe. 

“Tunajivuna kuzindua safari hii mpya kuelekea Mbeya ambayo itatuwezesha sasa kuwapatia huduma abiria kutoka Mbeya na kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Tutaanza kwenda Januari 16 mwaka huu,”alisema na kuongeza:

“Tunaamini kupeleka huduma zetu Mbeya itarahisisha usafiri kwa watalii, wafanyabiashara na  watu wengine wanaopenda kutembelea mkoa huo ambao ni tajiri kwa vivutio vya utalii kama Mbuga ya Taifa ya Wanyama ya Ruaha, Katavi pamoja na utajiri wa madini kama makaa ya mawe, dhahabu, chuma na vito”.

Linda alibainisha kuwa uzinduzi wa safari ya Mbeya inafikisha idadi ya maeneo 18 yanayofikiwa na ndege za shirika hilo.

“Baada ya uzinduzi huu, tutajikita kutanua zaidi idadi ya maeneo tunayofikia pamoja na kuongeza idadi ya safari hizo katika maeneo tunayoenda kwa sasa. Baada ya uzinduzi wa safari za Mbeya, tutarejesha safari za Dar es Salaam – Kigoma ambayo ilisitishwa kupisha ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kigoma,” alisema.

Hatua hii ya kuzindua safari za kwenda Mbeya inakuja mwezi mmoja baada ya shirika hilo kuzindua ndege yake mpya aina ya ATR 42-600, ambayo inatumia teknolojia mpya na ya kisasa ya aina ya ndege hizo za ATR.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...