RAIS 2015 NI MWANAMKE

*Sheikh asema atashinda kwa nguvu kubwa
*Awakata maini Lowassa, Membe, Sitta, Dk. Slaa
MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, amejitokeza hadharani na kutabiri matukio yatakayojiri mwaka huu kuelekea mwaka 2015.

Sheikh Khalifa ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa Kiislamu nchini, alisema mwaka 2013 utatawaliwa na mjadala mkubwa kuhusu mrithi wa Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake.

Kiongozi huyo wa kidini alisema, upo mpango unaoandaliwa kwa siri wenye lengo la kuwasambaratisha wanasiasa wanaojipanga kuwania urais, ili kumweka katika soko la siasa mwanamke msomi atakayegombea nafasi hiyo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Sheikh Khalifa alisema mwaka 2013, unatazamiwa kuwa wenye matukio makubwa yakiwamo majanga ya moto, mafuriko na vimbunga vitakavyoleta fazaa kwa watu.

Hata hivyo Sheikh Khalifa, alisema utabiri wake huo unatokana na elimu ya kuambiwa, tofauti na ule uliokuwa ukifanywa na marehemu Sheikh Yahaya Hussein, unaotokana na elimu ya nyota.

Kiongozi huyo alisema iwapo hakutatokea sababu za kuahirishwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ishara zinaonesha kuwa rais ajaye aidha atatokea Kaskazini au Kusini, lakini hatokani na majina ya viongozi wanaotajwa kwa sasa.

Kwa upande wa Kaskazini viongozi wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015 ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), DK. Willbrod Slaa.

Kwa upande wa Kusini anayetajwa kuwania urais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (Magharibi).

Wengine wanaotajwa kwa mbali ni Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa zamani wa Hanang’ Frederick Sumaye, anayetoka Kanda ya Kaskazini na Zitto Kabwe (Magharibi).

Kiongozi huyo alikwenda mbali zaidi katika utabiri wake na kusema kuwa, upo mpango unaoandaliwa kwa siri na kundi dogo la viongozi serikalini.

Alisema mpango huo wa siri unalengo la kumuandaa na kumuweka kwenye soko la siasa mwanamke msomi na maarufu, kwa lengo la kumjengea uwezo wa kusimama kugombea nafasi hiyo mwaka 2015.

“Ingawa mpango huo unaonyesha utaundiwa mkakati wa hali ya juu, lakini pia utapingwa kwa kutumia nguvu kubwa sana na endapo utafaulu mwanamke huyo anaweza kuwa ndiye rais ajaye,” alisema.
Siasa
“Katika medani ya siasa mwaka huu hapa nchini, kutakithiri na kuenea habari nyingi za uzushi, uongo na utesi wenye shabaha ya kuchafua majina ya baadhi ya viongozi waandamizi wa kiserikali na wanasiasa wenye mvuto.

“Janga hili litawaangukia zaidi wanasiasa ambao wako katika nafasi nzuri ya kukubalika mbele ya wananchi, kuelekea maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema.
 Mbio za urais 2015
“Pamoja na baadhi ya wanasiasa kujidhatiti katika maandalizi ya kujiweka tayari kugombea nafasi ya juu ya uongozi wa nchi (urais), mjadala utakaotawala mwaka huu 2013 ni kuhusu rais ajaye, baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake.

“Lakini pamoja na jitihada zilizokwishafanyika na zitakazoendelea kufanyika katika kipindi cha mwaka huu, hakuna ishara inayoonesha nyota njema kwa yeyote miongoni mwa majina yanayotajwa hivi sasa kuweza kufikia lengo hilo,” alisema.

 Vyama vya upinzani
Kuhusu vyama vya kisiasa, alisema hakuna ishara inayoonesha kuibuka kwa vyama vipya vyenye nguvu au kuimarika zaidi vyama vilivyopo, badala yake inaonesha katika kipindi cha mwaka 2013, chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) kitaendelea kuimarika.

“Ishara yenye kuonyesha kuendelea kwa ghasia za kisiasa, maandamano na maneno ya kejeli dhidi ya Serikali na viongozi wake, bado imesimama.

“Lakini hata hivyo wazo la kuunganisha nguvu za wananchi pamoja kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani nje ya utaratibu wa Katiba halitafanikiwa,” alisema Sheikh Khalifa.
 CCM
Kuhusu hali ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sheikh Khalifa, alisema katika kipindi cha mwaka huu kuna ishara ya kuongezeka kwa mizozo, chuki na makundi yenye uhasama ndani ya chama hicho kikongwe.

“Hali hiyo itakifanya chama hicho kuwa katika uongozi wa makundi, kwani baadhi ya wanachama wake waandamizi watatokwa na staha na adabu kwa viongozi wao wa ngazi za juu na kufikia katika hatua ya kuingia katika magomvi na kutangaza aibu za baadhi yao hadharani.

“Katika kipindi cha mwaka huu, hakuna ishara inayoonesha kuwa makundi hayo yatakuwa na nguvu ya kupindukia na kusababisha chama hicho kusambaratika.

“Bali yanaonesha makundi hayo yatakuwa ndiyo sababu ya chama hicho tawala hatimaye kuja kuongoza Serikali itakayofanana na meza ya mraba, lakini yenye miguu mitatu.

“Ipo ishara inaonesha kuwa, kuna misaada mingi itakayoingizwa nchini kwa anuani ya kuimarisha demokrasia, wakati lengo na madhumuni ni kuundoa utawala wa CCM, chama ambacho wakoloni hawakitaki,” alisema.

Hata hivyo kiongozi huyo alimfagilia Rais Jakaya Kikwete nakusema kuwa, mwaka huu atang’ara zaidi katika medani ya kimataifa na kusifika katika eneo la utawala bora na usimamizi mzuri wa misaada ya wahisani.
CHANZO:MTANZANIA

Comments