Tuesday, February 23, 2016

WAZIRI MUHONGO ATAKA MAKAMPUNI KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA UTAFITI WA MAFUTA, GESI

hog1
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akiongoza kikao kati yake na kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na teknolojia katika utafutaji wa mafuta na gesi ya  Schlumberger. Pia kikao hicho kilihusisha watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na  taasisi zake  likiwemo  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la Taifa(STAMICO), Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) na Mamlaka  ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). 
hog2
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Meneja Masoko  kutoka kampuni  ya Schlumberger, Abdul Adeshina (hayupo pichani) katika kikao hicho.
hog3
Meneja Masoko  kutoka kampuni  ya Schlumberger, Abdul Adeshina akielezea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa na teknolojia kwa ajili ya utafiti wa mafuta na  gesi nchini.
………………………………………………………………………………………………………..
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ametaka makampuni yanayojishughulisha na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa  gesi na mafuta nchini kuongeza kasi ya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili sekta ya  gesi na mafuta iweze kukua na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo alipokutana na kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na teknolojia katika utafutaji wa mafuta na gesi ya  Schlumberger yenye makazi  yake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili  utendaji kazi wa  kampuni hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilihusisha watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na  taasisi zake  likiwemo  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) na Mamlaka  ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema  Tanzania kwa sasa ina utajiri mkubwa wa  rasilimali ya  gesi ambayo  itachochea katika  ukuaji wa uchumi wa nchi  kupitia umeme wa uhakika utakaotumika katika viwanda na kuongeza  ajira kwa  vijana wa kitanzania.
Aliendelea kusema kuwa ili  sekta ya gesi na mafuta iweze kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi, Tanzania inahitaji wawekezaji  watakaowekeza kwa kasi kwa kutumia  teknolojia ya kisasa.
Alisisitiza kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na mwekezaji  yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya gesi na mafuta kwa kutumia  teknolojia ya kisasa.
“ Kama serikali  tumedhamiria kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye utajiri unaotokana na rasilimali za gesi na mafuta, hivyo  tunapenda kushirikiana  na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kutumia  teknolojia  ya kisasa,” alisema  Profesa Muhongo
Profesa Muhongo aliihakikishia kampuni ya Schlumberger kuwa  serikali itafanya kazi kwa karibu nayo na kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika ili sekta ya  gesi na mafuta iweze kukua kwa kasi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Awali akizungumza katika kikao hicho Meneja Masoko  kutoka kampuni  ya Schlumberger, Abdul Adeshina alisema  kampuni  yake  imekuwa imekuwa  ikitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kitanzania asilimia  80 wanaofanya kazi katika kampuni  hiyo.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa  ikishirikiana kwa karibu na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) katika shughuli za utafiti wa mafuta na gesi nchini  na kusisitiza kuwa kampuni hiyo  ipo tayari kutumia teknolojia na  vifaa vyake katika kuboresha shughuli za utafutaji wa mafuta na  gesi nchini.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...