Afisa uhamiaji Mkoa wa Singida, Faith Ihano akitoa taarifa za kukamatwa kwa wahamiaji haraamu kutoka nchini Ethiopia waliokuwa wakisafirishwa kwenda Afrika ya kusini.
Watumishi wa idara ya uhamiaji Mkoa wa Singida waliofanikisha upatikanaji wa watu 15 ambao ni raia wa Ehiopia.
Wahamiaji haramu 15 waliokuwa wametoka Ethiopia wakisubiri katika nyumba moja ya mtaa wa mitunduruni kusafirishwa kwenda Afrika ya kusini.
Na Jumbe Ismailly,Singida.
IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Singida imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 45 raia wa kutoka nchi za Ethiopia, Demokrasia ya Jamuhuri ya watu wa Congo pamoja na Malawi kwa tuhuma za kuingia na kuishi nchini bila kuwa na vibali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Ofisa Uhamiaji huyo wa Mkoa wa Singida, DSIS, Faith Ihano alisema wahamiaji hao haramu raia wa nchini Ethiopia walikamatwa baada ya kukutwa wakiwa wamefichwa kwenye nyumba ya mtu binafsi iliyopo kwenye Mtaa wa Unyankindi, Manispaa ya Singida,mkabala na nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa(NHC).
Kwa mujibu wa Ihano wakati askari wa jeshi hilo wakiwa katika doria kwa lengo la kukomesha wimbi la wahamiaji haramu hao linaloendelea kujitokeza siku hadi siku,walikuwa wakisafirishwa kwenda nchini Afrika ya kusini,wakitokea Jamuhuri ya Demokrasia ya watu wa Kongo, Malawi pamoja na Ethiopia.
“Wahamiaji hawa haramu waliokamatwa idadi yao ni kumi na tano na hao ni raia wa Ethiopia na kwamba wahamiaji hawa walikamatwa na askari wa kikosi cha uhamiaji wakiwa katika doria na wahamiaji hawa walikuwa wamehifadhiwa katika nyumba moja ya mtu binafsi”alifafanua Ihano.
Hata hivyo kwa mujibu wa afisa uhamiaji huyo kwa sasa wanamshikilia mwenye nyumba waliyokuwa wamehifadhiwa wahamiaji hao haramu kwa mahojiano zaidi na pindi upelelezi wao utakapokamilika,hatua za kisheria zitaweza kuchukuliwa dhidi yake.
Ofisa huyo wa uhamiaji hata hivyo alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa watu wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kuacha mara moja kwani idara ya uhamiaji inaendelea kufanya kila juhudi za kuwasaka wale wote wanaowasaidia kuwaingiza nchini kinyume cha sheria na kuhakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua kali na za kisheria.
No comments:
Post a Comment