JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Burundi Mheshimiwa Pierre Nkurunziza amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa hali ya Burundi ni shwari na kwamba tangu jana (Februari 22, 2016) nchi hiyo imepokea ugeni mkubwa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki-moon na inatarajia kupokea marais watano kutoka nchi za Umoja wa Afrika tarehe 25 Februari, 2016.
Ujumbe wa Rais Nkurunziza umewasilishwa na Mjumbe maalum ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Mheshimiwa Leontina Nzeyimana leo tarehe 23 Februari, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, alipokutana na Rais Magufuli na kufanya nae Mazungumzo.
Pamoja na kumpa taarifa kuwa Burundi inaendelea vizuri, Mheshimiwa Nzeyimana pia amemueleza Rais Magufuli kuwa Burundi ipo tayari kupokea nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa Rwanda, ikiwa ni kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaoelekeza kuwa nchi inayofuata kutoa Katibu Mkuu baada ya Katibu Mkuu wa sasa kumaliza muda wake, ni Burundi.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Balozi wa Uholanzi hapa nchini Mheshimiwa Jaap Frederiks, amewasilisha salamu za Mfalme wa Uholanzi Mtukufu Willem-Alexander ambaye amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizoonesha katika mwanzo wa utawala wake, katika kusimamia Uadilifu serikalini na katika biashara na pia kuisaidia Mahakama. Amesema Uholanzi inaamini kuwa maeneo hayo ndio yamekuwa yakileta vikwazo vya maendeleo, biashara na uwekezaji.
Balozi Jaap Frederiks amemhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ilivyofanya katika miaka 45 iliyopita, huku akitaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano kuwa ni Kilimo na Nishati.
Balozi wa India hapa nchini Mheshimiwa Sandeep Arya, amewasilisha salamu za Waziri Mkuu wa India Mheshimiwa Narendra Modi, ambaye pamoja na kuitaja Tanzania kuwa lango muhimu katika mpango wake wa ushirikiano na Afrika, amemhakikishia kuwa India itaendeleza uhusiano wake na Tanzania hususani katika biashara na uwekezaji ikiwemo kuunga mkono mpango wa ujenzi wa viwanda Tanzania.
Nae Balozi wa Zambia hapa nchini Mheshimiwa Judith Kangoma Kapijimpanga ameelezea matumaini makubwa ya kuendelezwa kwa ushirikiano na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Zambia na amemuomba Rais Magufuli aimarishe maeneo kadhaa ya kiushirikiano yakiwemo Reli ya TAZARA, Bomba la Mafuta la TAZAMA na taratibu za usafirishaji wa Mizigo katika bandari ya Dar es salaam na Mpaka wa Tanzania na Zambia.
Kwa upande wake Rais Magufuli amewahakikishia mabalozi hawa kuwa serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na nchi hizo na kwamba atafurahi kuona mahusiano na ushirikiano huo unaleta manufaa kwa wananchi.
Baadhi ya maeneo ambayo amezialika nchi hizo kuongeza ushirikiano na Tanzania ni katika ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge" kuwekeza katika viwanda vya kusindika mazao na kuzalisha bidhaa mbalimbali, Elimu na Afya.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Jaji Mkuu wa Mahakama hapa nchini, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Imetolewa;
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
23 Februari, 2016
No comments:
Post a Comment