Mbunge wa jimbo la Isimani Bw Wiliam Lukuvi ambae ni waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi (kulia) akimpa maelekezo mwenyekiti wa kijiji cha Mapogolo baada ya kumkabidhi fedha kiasi cha Tsh milioni 2 za kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi watakaohamishiwa makazi mapya kutoka kitongoji cha Kitanewa Idodi ambao nyumba zao zilisombwa na mafuriko
Mbunge wa jimbo la Isimani Bw Wiliam Lukuvi ambae ni waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi (kulia) akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukabidhi fedha hizo, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh. Richard Kasesela.
……………………………………………………………………………………………………..
Na MatukiodaimaBlog
MBUNGE wa jimbo la Isimani Bw Wiliam Lukuvi amewapa pole
waathirika wa mafuriko wa kata ya Mapogolo tarafa ya Idodi wilaya ya
Iringa mkoani Iringa kwa kuwakabidhi msaada wa pesa zaidi ya Tsh
milioni 9 kwa ajili ya kusaidia mahitaji mbali mbali ikiwa ni pamoja
na kurejesha miundo mbinu ya maji safi iliyoharibiwa na mafuriko.
Bw Lukuvi ambae pia ni waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi alikabidhi msaada huo jana baada ya kutembelea waathirika hao waliopo kambi ya Kitanewa pamoja na kutembelea eneo la barabara ya
kutoka Iringa kuelekea hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo kwa sasa
imekarabatiwa baada ya awali barabara hiyo kukatika kutokana na
mafuriko hayo , alisema kuwa lengo lake kama mbunge wa jimbo
hilo la Isimani na serikali ni kuona wananchi waliokumbwa na
mafuriko wanaendelea kusaidiwa .
Alisema kuwa awali aliomba msaada wa mahindi tani 100 kutoka serikali kwa
ajili ya waathirika hao wa mafuriko Idodi na Pawaga ikiwa ni
pamoja na kuwasaidia msaada wa fedha kiasi cha zaidi ya Tsh
milioni 3 kwa ajili ya kuwawezesha waathirika hao wa mafuriko
kupata mahitaji mengine kama mboga na pesa ya kusagia mahindi hayo .
Bw Lukuvi alisema kuwa kwa ajili ya kurejesha huduma ya maji kijijini
hapo amewasaidia kiasi cha Tsh miliobni 4 ambazo wameomba kwa ajili
ya kuboresha miundo mbinu hiyo ,pia kiasi cha Tsh milioni 2 kwa ajili
ya kukiwezesha kijiji kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi waliotoa
ardhi yao kwa ajili ya wakazi wa kitongoji cha Kitanewa ambao
wanapaswa kuhamishwa eneo hilo la mafuriko la kupewa makazi mapya .
” Waambieni watu wenye mashamba ambayo yatachukuliwa kwa ajili ya
viwanja mwaka huu wavune mazao yao na baada ya hapo kila mmoja
muweze kumlipa fidia ya Tsh 200,000 na baada ya hapo waitini
wataalamu wa ardhi ili waweze kupima viwanja na mpanfgilio mzuri
zaidi kwa ajili ya makazi mapya …….pia nataka hata mashamba ya
kawaida ya wananchi kupimwa ili kupata hati za ardhi
zitakazowawezesha kutumia kupata mikopo ….ila nitawaletea mashine
za kufyatulia tofari ambazo unaweza kuzijengea bila kuchoma “
Alisema kuwa kwa ajili ya kuhamasisha ujenzi wa nyumba bora mwananchi
atakayekuwa wa kwanza kupandisha jengo atamchangia bati japo kwa
sasa amekwisha toa bati zaidi ya 300 kwa mkuu wa wilaya ya Iringa
kwa ajili ya waathirika hao.
Bw Lukuvi pia amewapongeza wadau mbali mbali zikiwemo taasisi za dini ,watu binafsi
,taasisi ya kifedha pamoja na mifuko ya hifadhi za jamii kwa
kujitolea misaada mbali mbali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko na
wagonjwa wa Kipindupindu Pawaga .
Pamoja na kuwashukuru wadau hao Lukuvi alimpongeza waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kuwatembelea waathirika hao wa Mafuriko na wale wa Kipindupindu Pawaga .
Hata hivyo Lukuvi alimpongeza mkuu wa wilaya ya Iringa Bw Richard
Kasesela na viongozi wote akiwemo mkuu wa mkoa Amina Masenza kwa
kusimamia shughuli mbali mbali ikiwemo ya urejeshaji wa miundo mbinu
ya barabara iliyokuwa imekatika katika barabara ya Iringa – Ruaha .
Katika hatua nyingine Bw Lukuvi aliagiza serikali ya kijiji cha Mapogolo
kutowabagua wananchi katika kugawa chakula hicho cha msaada na
kutaka hata ambao si waathirika wa mafuriko ambao wana njaa wapewe
chakula hicho cha msaada kwa waathirika wa mafuriko.
Wakati huo huo Waziri Lukuvi alisema kuwa serikali inakusudia kuijenga
barabara ya Iringa- kuelekea hifadhi ya Ruaha kwa kiwango cha lami
kama mbavyo Rais Dr John Magufuli alivyoahidi wakati wa kampeni
kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM.
Pia kwa ajili ya kuwafanya wananchi kunufaika watalii wanaotembelea
hifadhi hiyo ya Ruaha Iringa alisema tayari jitihada za kujenga
viwanja vidogo vya ndege nje ya hifadhi ya Ruaha zimeanza na
kuwa lengo la serikali ni kuwahamisha wafanyakazi wanaoishi ndani
ya hifadhi hiyo na kujumuika na wananchi nje ya hifadhi ili
waweze kupata mahitaji kama wananchi wengine.
No comments:
Post a Comment