Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee ( wa pili kutoka kulia) akielezea mikakati ya kampuni hiyo katika uwekezaji wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ( kulia) akimweleza Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee (kushoto) fursa za uwekezaji nchini kwenye sekta ya umeme.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo katika kikao hicho
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee akifafanua jambo katika kikao hicho.
……………………………………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka taasisi zinazosimamia miradi ya umeme nchini kuongeza kasi ya utendaji kazi ili Tanzania iweze kupata umeme wa uhakika.
Profesa Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake kilichokutanisha Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema kuwa ili nchi iweze kuwa na umeme wa uhakika unaozalishwa kwa wakati ni lazima taasisi zilizopo chini ya Wizara zikahakikisha zinaongeza kasi katika uwekezaji kwenye uzalishaji wa umeme kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye vigezo ili uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ambayo ni kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika kundi la nchi masikini duniani na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Alisisitiza kuwa ili kufikia lengo hilo ni lazima taasisi zikaongeza kasi katika miradi yake ya umeme, kwa kushirikiana na wawekezaji mbalimbali na kuwataka kuondoa urasimu kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji wa umeme nchini.
Aliongeza kuwa nishati ni roho ya uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua bila kuwa na nishati ya umeme ya uhakika.
“ Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inakua kwa kasi na kutoa ajira hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo nishati ya umeme inahitajika sana; bila nishati ya uhakika uchumi hauwezi kukua kwa kasi inayotakiwa,’ alisisitiza Profesa Muhongo.
Waziri Muhongo aliendelea kusema kuwa nishati ya umeme ya uhakika itachangia ukuaji wa sekta za viwanda vidogo hasa maeneo ya vijijini, kilimo kukua kwa kasi na hivyo kunufaisha wananchi na pato la taifa kukua kwa kasi.
Aidha Profesa Muhongo alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kushirikiana kwa pamoja katika hatua zote za uwekezaji nchini ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kujitokeza kati ya serikali na wawekezaji.
“TANESCO na EWURA naomba mshirikiane katika kila hatua, kwa kukaa meza moja na wawekezaji na kufikia mwafaka kabla hawajaanza kuwekeza”, alisema Profesa Muhongo
Awali Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee akizungumza katika kikao hicho, alisema kuwa kampuni ya Kibo Mining ina mpango wa kuwekeza katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe ambapo itaanza na ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Megawati 900 kwa awamu tofauti.
Alisema awamu ya kwanza ambayo ni ujenzi wa mtambo wa kuzalisha Megawati 300 utakaogharimu Dola za Marekani milioni 800 utakamilika ifikapo mwaka 2019.
Akielezea hatua iliyofikia ya maandalizi ya uwekezaji wa kampuni ya Kibo Mining Coetzee alisema kuwa kampuni hiyo iliyoanza maandalizi yake mwaka 2008 inakamilisha upembuzi yakinifu (feasibility study) katika mradi wake na kuongeza kuwa wana mpango wa kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza mwaka 2017 baada ya taratibu zote kukamilika.
Alisema mara baada ya ujenzi wa mtambo wa kwanza kukamilika mwaka 2019, umeme utakaozalishwa mbali na kutumika viwandani utaongezwa kwenye gridi ya taifa na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa umeme nchini.
No comments:
Post a Comment