Friday, February 26, 2016

MAWAZIRI WAPEWA MWISHO LEO KUJAZA TAMKO LA MALI NA MADENI, HATI YA UADILIFU

 Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majliwa Majaliwa (kulia) akitoa taarifa mbele ya Waandishi wa Habari kuhusiana na misingi ya Fomu za Maadili ya Utumishi wa Umma kwa Viongozi wa Umma pamoja na kujaza fomu za tamko za rasilimali walizo nazo na za madeni waliyonayo sambamba na kutaja majina ya baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri ambao bado mpaka sasa hawajarudisha fomu hizo kwa Kamishna. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki.
 
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusiana na misingi ya Fomu za Maadili ya Utumishi wa Umma kwa Viongozi wa Umma pamoja na kujaza fomu za tamko za rasilimali walizo nazo na za madeni waliyonayo sambamba na kutaja majina ya baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri ambao bado mpaka sasa hawajarudisha fomu hizo kwa Kamishna.(PICHA ZOTE NA EBENEDICT LIWENGA-MAELEZO)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni (Ijumaa, Februari 26, 2016).

Agizo hilo la Rais limetolewa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Rais ameelekeza mawaziri ambao hawajajaza tamko la rasilmali au hati ya ahadi ya uadilifu wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema wakati akifungua mafunzo ya Mawaziri na Naibu Waziri kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu jana (Alhamisi, Februari 25, 2016) alikabidhiwa majina ya Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao hawajawasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.

Amewataja mawaziri wanaotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Bw. January Makamba. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga ambaye anatakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako ambaye anatakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira), Bw. Luhaga Mpina anatakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilmali na madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma

No comments: