Friday, February 26, 2016

TANZANIA KUNUFAIKA NA DOLA BILIONI 60 ZA CHINA SEKTA YA NISHATI

SO1
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akiongea jambo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (wa pili kushoto)  wakati alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni  Afisa Ubalozi wa China.
SO2
Balozi wa wa Jamhuri ya Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (katikati) akimweleza jambo Afisa Ubalozi wa China nchini, wakati wa kikao chake na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia).
SO3
Afisa Ubalozi wa China nchini (wa kwanza kushoto) akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo wakati wa kikao chake na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dkt. Lu Youqing (katikati).
SO4
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dkt. Lu Youqing (wa tatu kushoto), akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Utumishi Wizara ya Nishati na Madini, Lusias Mwenda. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Balozi wa China.
………………………………………………………………………………………………………………
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam,
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeitaja nchi ya Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na fedha kiasi cha Dola Bilioni 60  kupitia  uwekezaji sekta ya nishati, fedha zilizoahidiwa kutolewa na nchi hiyo wakati wa Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika, uliofanyika nchini Afrika Kusini mwezi  Desemba,2015.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing na ujumbe wake alipokutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, China ina imani kubwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia masuala mbalimbali nchini, pia Profesa Sospeter Muhongo kutokana na  namna anavyoisimamia sekta ya Nishati  na Madini.
Miongoni mwa Sekta zinazopewa kipaumbele katika fedha hizo ni pamoja na pamoja na  miundombinu, afya, biashara, uwekezaji na kupunguza umaskini, barani Afrika.
Kutokana na mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo kwa miongo kadhaa baina ya nchi hizo mbili, Balozi Youqing amemwakikishia Waziri Muhongo kuwa, China itaendeleza ushirikiano huo kwa kuhakikisha inazishawishi kampuni kubwa na zilizobobea kitaalamu na kiteknolojia za China, ili ziweze kushirikiana na Tanzania katika sekta ya nishati, na zaidi katika uzalishaji umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe kutokana na namna ambavyo Wizara inavyokipa kipaumbele chanzo hicho kuzalisha umeme nchini.
Wakati huo huo, China imesema itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi Watanzania kusoma masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali nchini humo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo na kwamba, China inapenda Tanzania ifanikiwe katika kuzalisha wataalam wa kutosha katika fani hizo na kuongeza kuwa, anatambua juhudi zinazofanywa na Waziri Muhongo kuhakikisha wanafunzi wengi wa kitanzania wanapata fursa ya kusoma masuala ya mafuta na gesi maeneo mbalimbali Duniani, ikiwemo China.
Aidha, leo tarehe 26 Februari, 2016, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za Masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kuomba kusoma katika Vyuo vya China katika fani za Mafuta na Kazi katika ngazi za Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (Phd). Maelezo zaidi ya kuomba nafasi hizo yanapatikana kupitia tovuti ya wizara www.mem.go.tz

No comments: