Tuesday, October 08, 2013

Wizara ya Kazi na Ajira imewaasa waajiri katika Sekta binafsi kuzingatia Sera na sheria za kazi mahali pa kazi ili kuleta tija na nidhamu kazini



 Msemaji toka Wizara ya Kazi na Ajira Bw.Ridhiwan Wema(Kulia) akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Bodi  za Mishahara Kisekta kwa mujibu wa sheria Na. 7 ya Mwaka 2004 ya Taasisi za Kazi katika Sekta Binafsi, wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mchumi Mwandamizi wa Wizara hiyo Bw. Jofrey Mashafi.
 Afisa Kazi Mwandamizi toka Wizara ya Kazi na Ajira(kulia) akieleza kwa waandishi wa habari(Hawapo pichani) jinsi ukuaji wa sekta unavyochangia kuanzishwa kwa bodi ya Mshahara kwa Sekta husika wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Leo jijini Dar es Salaam. Msemaji Wizara hiyo  Bw.Ridhiwan Wema.
Mchumi Mwandamizi toka Wizara ya Kazi na Ajira Bw. Jofrey Mashafi (kulia) akieleza mipango ya serikali ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa Ajira Nchini ikiwa ni pamoja kuanzisha programu ya miaka 3 inayoratibiwa na Wizara ya Kazi na Ajira kwa kushirikiana Chuo cha Sokoine na  Bank ya CRDB ya kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu, inayotarajiwa kuzalisha ajira 30,000, wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Georgina Misama. Picha na Frank Mvungi
---
 Na Frank Mvungi

WIZARA ya Kazi na Ajira imewaasa waajiri katika Sekta binafsi kuzingatia Sera na sheria za kazi mahali pa kazi ili kuleta tija na nidhamu kazini.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara hiyo Ridhiwani Wema wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, akieleza kuhusu utaratibu wa uanzishwaji wa Bodi za mishahara kisekta ili kusaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Wema amevishauri vyama vya wafanyakazi kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi kupitia majadiliano ya pamoja sehemu za kazi  kwa kuwa sheria na kanuni zinatoa na kuhimiza haki hizo.
Alizitaja bodi za mishahara zilizoanzishwa kuwa ni kilimo, Afya, Biashara na Viwanda, Mawasiliano, Madini, Uvuvi na huduma za majini, hoteli na huduma za majumbani, na ulinzi binafsi.
Wema alifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2011 hadi sasa ziliundwa bodi 4 za mishahara kufanya jumla ya bodi za kisekta kuwa 12 hadi mwaka 2013.
“Moja ya majukumu ya bodi ni kufanya uchunguzi kuhusu kima cha chini cha mishahara na hali ya ajira katika sekta husika ambapo  pia humshauri Mhe. Waziri kuhusu kima cha chini cha mishahara pamoja na masharti ya ajira katika sekta husika”, alisema Wema.
Alibainisha kuwa Bodi za ajira zimetembelea mikoa ya Daressalaam, Mororogoro, Pwani, Dodoma, Arusha, Mwanza, Tanga, Manyara, Iringa, Mbeya na Kilimanjaro ili kijionea mazingira ya kazi na kupata maoni ya wadau kuhusu kima cha chini cha mishahara katika Sekta husika.
Msemaji huyo aliongeza kuwa vyama vya wafanyakazi vina nafasi kubwa kusaidia katika kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi kupitia majadiliano ya pamoja sehemu za kazi kwa kwa kuwa sheria na kanuni zinatoa na kuhimiza haki hiyo.
Naye Afisa Kazi Mwandamizi Idara ya Ajira, Ayubu Musa alisema kuwa wizara hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa taratibu, sheria na kanuni za kazi zinazingatiwa ambapo wamekuwa wakifanya ukaguzi mara kwa mara ili kuhakisha kuwa kuna mazingira bora na maslahi ya wafanyakazi katika sekta binafsi.
Bodi za mishahara kisekta zinaundwa kwa mujibu wa sheria ya Taasisi za kazi namba 7 ya mwaka 2004 ambapo kila bodi inaundwa na wajumbwe 8 akiwemo mwenyekiti na wajumbe wanaowakilisha maslahi ya Serikali wajumbe 2,waajiri wajumbe2 na wafanyakazi 2 katika mfumo wa utatu.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...