Picha hizo hapo juu zinanikumbusha mbali saana wakati huo nikiwa katika mazingira haya yanayonikumbusha saaana Bob Kinyesi, Nyangala, Quarter Master, Coy, Smart area, na mengineyo mengi.
Nakumbuka mwaka 1993 nilichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora (Tabora Boys High School). Shule hii yenye historia ya kipekee kwa nchi yetu imetoa mchango mkubwa sana wa kusomesha viongozi wa nchi yetu.
Wakati huo nilipokuwa nikijiunga na shule hiyo ilikuwa na mchepuo wa kijeshi. Mchepuo huo wa kijeshi sio tu ulitupatia wanafunzi ukakamavu na nidhamu ya hali ya juu bali pia ulitujaza uzalendo kwa nchi yetu kwa kiwango kikubwa. Huku tukiwa na sare zetu za ‘kijeshi’ (zilikuwa kombati za khaki kama za jeshi la mgambo), maafande wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliokuwa wakiendesha mafunzo shuleni hapo walitupatia mwamko wa hali ya juu kuhusu kuitumikia na kuilinda nchi yetu.
Heko zao maafande Chacha, Peter Majasho, Warioba, Binde na walimu Madafu, Magesse, Nyanda, Katendele huyu alikuwa Headmaster wetu kabla hajakabidhi ofisi kwa Mkuu wa Shule Ngosha Wajimila.
Kabla ya kuanza masomo tulipewa kile kilichoitwa introduction to the camp iliyojumuisha kwata za kijeshi na hatua nyingine wanazopitia ‘makuruta’ wanapoingia kambini kwa mara ya kwanza. Ilipofika mwisho wa mwaka, wanafunzi wa kidato cha tatu na cha tano tulipelekwa msituni kwa mafunzo ya vita kwa vitendo, ambako huko tuliweza kufunzwa ujanja wa porini, sindicate na zoezi maarufu la range.
No comments:
Post a Comment