Thursday, October 17, 2013

KESI YA MAUAJI YA BILIONEA WA TANZANITE ERASTO MSUYA YAENDELEA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI MJINI MOSHI

Watuhumiwa wakiondolewa Mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa Polisi
---
Na Fadhili Athumani, Moshi
MTUHUMIWA “Muhimu” katika kesi ya mauaji ya Bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43), Ally Mussa “Majeshi” (42) amepandishwa mahakamani katika Mahakama ya hakimu mkazi Moshi, mkoani Kilimanjaro. 

Mtuhumiwa huyo aliyekamatwa Oktoba 8, mwaka huu, alinaswa mkoani Kigoma akijaribu kutorokea nchini Burundi baada ya kufanikiwa kukimbia mitego ya polisi katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Mwanza na kurudishwa mkoani kilimanjaro ambapo jana aliunganishwa katika kesi ya Mauaji ya Msuya. 

Akisoma Mashtaka yanayomkabili Mtuhumiwa huyo mbele ya Mahakama ya Hakimu Munga Sabuni, Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Janet Sekule alisema Mshtakiwa huyo pamoja na wenzake Saba, wanashtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia kinyume cha kinyume cha kanuni namba 16, 
kifungu cha 196 ya sheria za makosa ya jinai.

“Kinyume cha sheria ya makosa ya jinai, kanuni ya 16, kifungu cha 196, Ally Mussa au kwa jina lingine Majeshi, walimuua Erasto Msuya katika maeneo ya Mjohoroni, njia panda ya Arusha na KIA kwa kumpiga risasi,” alisema Sekule.

Aidha baada ya kusoma maelezo ya shtaka hilo, upande wa Jamhuri, ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Janet Sekule iliiomba Mahakama ya Hakimu Sabuni kuipa muda kuweza kukamilisha upelelezi ambapo kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 28, mwaka huu, itakapo tajwa tena.

Ally Mussa “Majeshi”, anayedaiwa kuwahi kulitumikia Jeshi la kujenga  Taifa (JKT), kabla ya kufukuzwa anaungana na Sharif Mohamed Athuman (31) mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), mkazi wa Songambele Wilaya ya Simanjiro.

Wengine ni Joseph Damas Mwakipesile maarufu kama Chusa (36), mfanyabiashara wa madini na mkazi wa Arusha, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir ‘Msudani’ au ‘Mnubi’(32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata wilayani Hai na Karim Kihundwa (33) mkazi wa Kijiji cha Lawate Wilaya ya Siha na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha. 

 Hata hivyo Mwandishi wa Habari hizi alishuhudia kesi hiyo ikisomwa  katika hali ya utulivu tofauti na ilivyozoeleka kwani katika mara zote kesi hiyo ilipofikishwa Mahakamani hapo kulikuwa na umati mkubwa wa watu wakiwemo ndugu za Marehemu Erasto Msuya. 

Mfanyabiashara Erasto Msuya, aliuawa Agosti 7, mwaka huu majira ya  6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha– Moshi katika eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...