Saturday, October 04, 2025

TANZANIA NA ZIMBABWE ZASAINI MAKUBALIANO KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA




Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na Chemba ya  Biashara ya Taifa la Zimbabwe (ZNCC) wamesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Zimbabwe. Hafla ya utiaji saini imefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika mjini Victoria Falls, Zimbabwe tarehe 2 na 3 oktoba,2025.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, na Naibu Rais wa ZNCC, Bi. Josephine Takundwa, yakilenga kuhamasisha, kukuza na kuwezesha ushirikiano wa kiuchumi kati ya sekta binafsi za nchi hizo mbili. Tukio hilo limeshuhudiwa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan S. Kaganda, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa ya Zimbabwe, Balozi Albert Chimbindi.

Kupitia makubaliano hayo, pande zote zimekubaliana kuandaa misafara ya kibiashara, maonesho, warsha na mikutano ya kibiashara kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji. Pia, zitabadilishana taarifa muhimu za kiuchumi na takwimu zitakazowezesha wanachama kufanya biashara kwa ufanisi na kuongeza tija.

Makubaliano hayo yanalenga pia kushughulikia changamoto za kibiashara, hususan vikwazo visivyo vya kiforodha, pamoja na kujenga mitandao ya kibiashara itakayowaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji kuanzisha miradi ya pamoja yenye manufaa kwa pande zote.

Hati hii ya makubaliano itadumu kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Oktoba 2025, ikiwa na uwezekano wa kuongezwa kwa makubaliano ya maandishi kati ya pande mbili. Hatua hii inalenga kuhakikisha uendelevu wa ushirikiano wa kibiashara na manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wa Tanzania na Zimbabwe.

Kupitia ushirikiano huu, nchi hizo mbili zinatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza ajira, na kuimarisha nafasi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi wa kikanda. Hatua hii pia inaonesha dhamira ya dhati ya Tanzania na Zimbabwe kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukuza maendeleo endelevu barani Afrika.

No comments:

TANZANIA NA ZIMBABWE ZASAINI MAKUBALIANO KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA

Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na Chemba ya  Biashara ya Taifa la Zimbabwe (ZNCC) wamesaini hati ya makubaliano (MoU...