Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akikagua magari matano yaliyotolewa kwaajili ya kupambana na ujangili katika kanda ya Kaskazini kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro(KIA) yakiwa na thamani ya Sh 750 milioni.
Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akijaribu moja ya bunduki 50 aina ya AK 47 zilizotolewa kwaajili ya kupambana na ujangili katika kanda ya Kaskazini kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro(KIA)
……………………………………….
Kikosi cha kupambana na ujangili nchini kimepata vitendea kazi kutoka kwa wadau wa sekta ya utalii vitakavyowezesha kukabiliana na matukio ya ujangili yaliyoshika kasi nchini na kuhatarisha kutoweka baadhi ya wanyama.
Miongoni mwa misaada iliyotolewa ni magari matano aina ya Land Cruser yenye thamani ya Sh 750 milioni,bunduki za kivita 50 aina ya Ak 47 na risasi 10,000 na Magazini 20 ambazo thamani haikutajwa kwa kwasababu za kiusalama.
Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu baada ya kukagua vitendea kazi hivyo kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) amesema vitasaidia kuongeza nguvu za kufanya doria na kupambana na ujangili kwenye mapori ya akiba nchini na kudhibiti utoroshwaji wa nyara za serikali.
Nyalandu amekiri kuwapo kwa changamoto ya mwingiliano wa maeneo yaliyohifadhiwa na makazi ya wananchi ambayo inatatuliwa kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)lengo likiwa kuwa na uhifadhi endelevu ambao unaleta maendeleo endelevu kwa wananchi.
Naye Naibu Mkuu wa Kikosi cha kupambana Ujangili Kanda ya Kaskazini,Michael Msuka amesema vitendea kazi hivyo vitaongeza hari ya watumishi katika kulinda wanyamapori katika mikoa ya Arusha,Kilimanjaro,Manyara na Tanga.
Alisema vita ya kupambana na ujangili ni kubwa kwani katika kipindi cha mwezi Septemba hadi Disemba mwaka 2014 jumla ya majangili 203 walikamatwa kwenye maeneo mbalimbali nchini na kuwa wamefikishwa mahakamani na baadhi yao kutozwa faini.
No comments:
Post a Comment