Monday, March 30, 2015

KITUO CHA JIMOLOJIA KUWEZESHA UONGEZAJI THAMANI MADINI NCHINI

001
Mkandarasi wa kampuni ya Kiure Engineering iliyofanya Ukarabati Mkubwa katika kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) cha Jijini Arusha, Oswald Modu ( wa tatu kulia) akimkabithi funguo za vyumba mbalimbali vya kituo hicho, Mkurugenzi wa Manunuzi Wizara ya Nishati na Madini Amon Makachayo (wa tatu kushoto). Wengine wanaoshuhudia ni baadhi ya watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini na Wafanyakazi wa kampuni ya Kiure Engineering.
002
Mratibu wa Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) Mussa Shanyangi (wa pili kulia), akiwaonesha Mkurugenzi wa Manunuzi Wizara ya Nishati na Madini Amon Makachayo (wa pili kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Habari na Teknolojia Francis Fungameza namna mashine ya kukata mawe inavyofanya kazi.
003
Baadhi ya Wanafunzi katika kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) waki polish mawe wakati wa mafunzo. Wanafunzi hao wako katika mafunzo ya ukataji na unga’rishaji madini katika kituo hicho.
004
Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) Idrisa Yahya (kushoto) akimweleza jambo Mkandarasi wa Kampuni ya Kiure Engineering Oswald Modu(wa tatu kulia) wakati wa ukaguzi wa jingo la kituo hicho kabla ya makabidhiano rasmi kufanywa.
005
Baadhi ya wanafunzi wa kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) kilichopo Jijini Arusha. Wakiwa katika mafunzo ya kunga’risha madini. Kituo hicho kitawezesha shughuli za Uongezaji Thamani kufanyika chuoni hapo.
006
Sehemu ya Jengo la kituo cha Jimolojia Tanzania TGC, inavyoonekana pichani baada ya Ukarabati Mkubwa kufanywa na Kampuni ya Kiure Engineering. Jengo hilo limekabidhiwa rasmi kwa kituo hicho mwishoni mwa wiki.
007
Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) Idrisa Yahya (katikati) na ujumbe wa Wizara na Mkandarasi wa Kampuni ya Kiure Engineering wakikagua mfumo wa CCT katika kituo cha Jimolojia Tanzania. (TGC).
008
Baadhi ya Vinyango vilivyochongwa kwa madini yam awe katika kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC).
………………………………………………………………………………
Na Asteria Muhozya, Arusha
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) cha Jijini Arusha ni mafanikio makubwa kwa Wizara ya Nishati na Madini hususan katika tasnia ya Uongezaji Thamani Madini nchini kwani kitawezesha shughuli hizo kufanyika nchini.
Hayo yamebainishwa na Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) Idrisa Yahya mwishoni mwa wiki wakati wa makabidhiano ya kituo hicho baada ya kukamilika kwa ukarabati mkubwa uliofanywa na kampuni ya Kiure Engineering .
“Mkandarasi amejitahidi kufanya kazi katika muda tuliokubaliana na kazi imefanyika kama ilivyotakiwa. Hivi sasa tutautaja kama mradi uliokamilika”, alieleza Idrisa.
Aliongeza kuwa, mradi wa SMMRP utaendelea kukisaidia kituo hicho ili kiweze kutimiza malengo yake na kuhakikisha kinatoa taaluma katika masuala ya uongezaji thamani madini na hivyo kuwezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika pato la taifa. 
Alisema kuwa, SMMRP imelenga katika kukiwezesha kituo hicho kuwa bora katika mafunzo ya uongezaji thamani madini nchini kutokana na umuhimu wa shughuli hizo kufanyika nchini badala ya madini hayo kusafirishwa nje ya nchi yakiwa ghafi. 
“Tumelenga katika kukiunganisha kituo hiki na vyuo vingine duniani vinavyotoa taaluma katika masuala haya ili kupata uzoefu na kubadilishana taaluma. Tunataka kituo hiki kifanye kazi iliyokusudiwa na kisimame peke yake hivyo lazima kiweke mipango mizuri. Kwa upande wa wizara ina budi kutenga bajeti ya kituo hiki kiendelee ili kutimiza malengo tunayoyatarajia”, alisisitiza Idrisa.
Kwa upande wake Mratibu wa kituo hicho Musa Shanyangi alisema kuwa, kituo hicho kinatarajia kuanza muhula mpya wa masomo ifikapo mwezi Juni mwaka huu katika fani za ukataji madini, masuala ya jimolojia, mafunzo ya usanifu na utengenezaji wa mapambo ya vito.
“Hivi sasa tunao wanafunzi 15 wanawake wanaosoma fani ya kukata na kung’arisha madini. Wanafunzi hawa walianza mafunzo tangu Novemba 2014 na wanasoma kwa ufadhili wa Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA)” alisema Shanyangi.
Aidha, Shanyangi aliishukuru Serikali kwa kutambua shughuli za uongezaji thamani madini nchini kwani zitaongeza wigo wa ajira, kipato cha mtu mmoja mmoja, kuwezesha ukuaji wa shughuli za kiuchumi kupitia sekta hiyo ikiwemo pia kuchangia katika pato la taifa.
Shughuli za uimarishaji na uendelezaji wa kituo hicho zinafanyika chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP). Kituo kitakuwa na maabara ya utambuzi wa madini ya vito, maktaba ya jimolojia na makumbusho ya madini ya vito.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...