Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya ‘Ask Indus Global’ imezinduwa huduma zake nchini Tanzania ikiwa ni ofisi itakayo waunganisha wananchi nchini Tanzania juu ya huduma mbalimbali wanazohitaji nchini India wakiwa Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ofisi za Ask Indus Tanzania Limited, Mkurugenzi Mtendaji wa Ask Indus Global, Abhilash Puljal alisema ofisi hiyo ya Dar es Salaam itakuwa kiungo kwa wananchi wanaoitaji huduma za afya, elimu na masuala ya biashara nchini India ambapo kwa sasa wataunganishwa bila usumbufu.
Alisema fursa hiyo pia itakuwa ni daraja zuri kwa wafanyabiashara wadogo nchini Tanzania ambao wanahitaji kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nchini India ambapo wataunganishwa na kupata mahitaji yao kwa gharama nafuu na kuepuka mlolongo na gharama za juu.
Alisema kampuni hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wanaotegemea huduma za afya kutoka nchini India kwani itakuwa na vifaa vya kisasa vya mawasiliano ambapo mgonjwa anaweza kupata huduma kupitia Ask Indus Tanzania na aweza kupata huduma za awali kuanzia mawasiliano na hospitali, daktari na hata uchaguzi wa hospitali ya kutibiwa kabla ya kuingia gharama za kwenda nchini India tena kwa gharama nafuu.
Alisema ofisi hiyo ambayo pia ipo nchini Kenya itakuwa kiungo kikubwa na kuchochea maendeleo kuanzia kwa wafanyabiashara, wananchi wahitaji wa huduma za elimu nchini India kutokea Tanzania na wahitaji wa huduma za afya ambao awali ilichukua muda na gharama kubwa.
Akizindua Ofisi hiyo, Balozi wa India nchini Tanzania, Debnath Shaw alisema hiyo ni fursa pekee kwa wananchi Tanzania kuunganishwa kwa huduma mbalimbali kuanzia zile za afya, biashara hasa kwa wafanyabiashara wadogo na wakati pamoja na wahitaji wa huduma za elimu.
Alisema kufunguliwa kwa ofisi hiyo mbali na kuchochea maendeleo ya nchi pia ni daraja la kuwaunganisha wananchi wa pande zote juu ya mahusiano ya kiuchumi, kijamii na shughuli nyingine muhimu. Aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo ipasavyo ili kuokoa gharama huku wakijipatia mahitaji yao thabiti.
No comments:
Post a Comment