Monday, September 08, 2014

SARAFU YA SH.500 KUANZA KUTUMIKA RASMI KUANZIA MWEZI OKTOBA MWAKA HUU

39-640x400
Kipimo Abdallah
KATIKA kile kinachodaiwa ni uchakavu wa haraka wa noti ya shilingi mia tano Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeibadilisha noti hiyo na kuwa ya sarafu ambayo itaanza kutumika rasmi kuanzia mwezi ujao wa Oktoba mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BOT Emmanuel Boaz wakati akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Kibenki BOT alisema takwimu zinaonyesha kuwa shilingi mia tano ya noti inahusika zaidi kwenye  manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti zingine, hivyo noti hiyo kupita kwenye  mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi hivyo kuchakaa haraka.
Alisema sababu nyingine ni kuwa noti ya shilingi mia tano inakaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo wake.
“Kimsingi tumeangalia kwa umakini mpaka tumefikia uamuzi huu ila kiukweli ni kuwa noti ya mia tano inatumika sana katika mzunguko wa kila siku katika manunuzi hivyo sulihisho ni mia tano ya sarafu ambayo inaweza kudumu kwa muda mrefu”, alisema.
Boaz alisema sarafu hiyo itatambulika kwa alama mbalimbali ambazo ni umbo la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5, uzito wa gramu 9.5, rangi yake ni ya fedha na imetengenezwa kwa madini ya chuma na nickel.
Aidha kwa upande wa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume, kwa upande wa nyuma  inataswira ya mnyama nyati akiwa mbugani na ina alama maalumu ya usalama iitwayo “latent image” iliyo upande wa nyuma ambayo ni kivuli kilichojificha ambacho huonyesha thamani ya sarafu ya shilingi mia tano au neno BOT inapogeuzwa geuzwa.
Mkurugenzi huyo alisema sarafu hiyo itaendelea kutumia sambamba na noti ya shilingi mia tano hadi hapo itakapo isha na wananchi wasiwe na wasiwasi ambapo aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia vipindi mbalimbali ambavyo vitakua vikielezea  jinsi sarafu hiyo ilivyo na namna ya kutunza noti na sarafu kwa njia salama.
Aidha Boaz alisema sarafu hiyo itakuwa ya 12 tangu kuanzishwa kwa BOT ambapo sarafu ya kwanza ilikuwa senti tano, kumi, ishirini, hamsini, shilingi moja, kumi, ishirini na zingine nyingi hadi kufikia hii ya sasa ya shilingi mia tano, ambapo kwa sarafu za kumbukumbu hadi sasa zimetolewa hadi kufikia 23.
Akijibu juu ni kwa nini wamekuwa wakitumia sura za viongozi waasisi wa Taifa hili pekee katika fedha alisema suala hilo ni maamuzi ya BOT ila kwa hii sarafu ya mia tano msingi wake ni kuendeleza muonekano ambao ulikuwa katika mia tano ya noti.
Kwa upande wake Hassan Jarufu ambaye ni Mshauri wa Fedha wa BOT akijibu swali la kuwepo kwa watu ambao wanajihusisha na uuzaji wa fedha hasa katika vituo vya daladala alisema BOT haihusiki na biashara hiyo kwa kile alichodai kuwa hakuna sheria inayokataza au kuruhusu biashara hiyo.
Alisema BOT imewaelekeza watumia huduma za kifedha zote waende katika mabenki ambayo wamefungua akaunti zao kubadili fedha iwapo wanahitaji ambapo wakitoa shilingi elfu kumi ya noti watapatiwa elfu kumi ya sarafu iliyochenchiwa.
Jarufu aliwataka watanzania kuacha tabia ya kurahisisha mambo na baadae kuilamu BOT kwani utaratibu upo wazi kwa kila mteja wa benki kuomba huduma yoyote katika benki aliyofungua akaunti.
Naye Meneja Msaidizi wa Habari na Itifaki Victoria Msina alitoa wito kwa wananchi kutumia BOT makao makuu na katika matawi yao mbalimbali yaliyopo Zanzibar, Arusha, Mbeya na kwa sasa wapo katika mchakato wa kufungua tawi linguine Dodoma kwa kupata ufumbuzi wa jambo lolote linalowakera.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...