Mhe. Said Ali Mbarouk akiwa na mwenyeji wake Waziri wa Habari nchini Oman Sheikh Dk. abdulla wakati alipofanya mazungumzo katika ofisi yake tarehe 29 Septemba 2014 akiwa katika ziara rasmi ya siku nne kutembelea sekta mbali mbali za Utalii, Utamaduni na Michezo.
MUSCAT, OMAN 30/09/2014
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk ameuelezea ushirikiano baina ya Oman na Zanzibar kuwa daima utakuwepo na utaendelea kukua kutokana na kutanuka kwa maeneo mapya ya ushirikiano katika Nyanja mbali mbali za maendeleo.
Amesema ni jambo la faraja kuona kuwa hivi sasa Zanzibar na Oman zinatambua umuhimu wa kutanua maeneo hayo ya ushirikiano katika sekta za uchumi, utalii na michezo kwa lengo la kuwanufaisha watu wa pande zote mbili.
Mhe. Saidi Ali Mbarouk ameyaeleza hayo katika nyakati tofauti wakati alipokuwa na mazungumzo na Mawaziri wa sekta za Habari, Michezo, Utamaduni na Utalii mjini Muscat Oman leo, akiwa katika ziara yake ya siku nne ya kukutana na viongozi mbali mbali wa nchi hiyo kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mapema akizungumza na Waziri wa Habari wa Oman, Sheikh Dk. Abdulla Monaim Bin Mansoor Al Husani, alitoa shukrani zake kwa Serikali ya Oman kwa misaada yake kwa Zanzibar na kusifu nidhamu ya vyombo vya habari vya nchi hiyo katika kuwaunganisha watu na kuwawezesha kujenga uchumi imara.
Alisema hatua hii ya mfano wa kuigwa inatokana na usimamizi madhubuti kwa vyombo vya habari na kujali kuwajibika kwa jamii kwa vile vinatoa nafasi ya kuwapatia taarifa za kutosha juu ya harakati za kujiendeleza na kujenga ustawi na maendeleo yao.
Ameshauri haja ya kuwepo na utaratibu wa kubadilishana wataalamu na vipindi ili kila nchi iweze kujifunza kutoka upande mwengine kwa kutambua maendeleo yanayofikiwa na kila upande na hivyo kutoa fursa za kuwawezesha vijana na vyombo vya habari kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao kwa pamoja hasa kwa vile ni tegemeo kubwa la taifa katika kujenga uchumi.
Katika ziara yake hiyo ya siku nne, Mheshimiwa Saidi Ali Mbarouk pia alipata fursa ya kubadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Utamaduni na Mambo ya Kale, Sheikh Hamad Hilal Al Maamari na Waziri wa Michezo, Sheikh Shallal Saad Moh’d Al Saad na kutuwama zaidi katika masuala ya kubadilishana wataalamu wa michezo na kuyahuisha majengo ya kihistoria yenye mnasaba na Oman.
Wakati huo huo, Mhe. Said Ali Mbarouk ameitaka Oman kufungua fursa nyengine kwa kuisaidia Zanzibar katika kuanzisha Hoteli za kitalii za Halal utaratibu ambao Oman tayari imeuanzisha na kupata mafanikio yake.
Amefahamisha kuwa utaratibu wa hoteli kama hizo za Halal ni muafaka katika visiwa vya Zanzibar kwa vile zitaongeza soko la idadi ya watalii wanaohitaji kupumzika katika maeneo yenye utulivu wa maadili ya kidini na kiutamaduni.
Katika ziara yake hiyo Waziri huyo wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo alipata fursa ya kushiriki katika karamu rasmi iliyoandaliwa kwa ajili yake na ujumbe wa watu watatu aliyofuatana na Mwenyeji wake Waziri wa Habari wa Oman Sheikh Dk. Abdulla Monaim iliyofanyika katika jumba la serikali la Opera mjini Muscat.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI HABARI AMELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment