Mbunge wa jimbo la Kalenga Godfrey Mgimwa kulia akisalimiana na mdau mkubwa wa maendeleo kata ya Nzihi Kidamali George Filiakosi |
Mkuu wa shule ya sekondari Kidamali Sixtus Kanyama akieleza mahitaji ya ujenzi wa maabara hiyo kwa wageni waalikwa na wananchi |
Mbunge wa jimbo la Kalenga Godfrey Mgimwa akieleza furaha yake baada ya kuona ujenzi wa maabara ya sayansi shule ya sekondari Kidamali |
Na matukiodaima.co.tz
KATIKA kile kinachoonyesha ni kuunga mkono maagizo ya Rais Dr Jakaya Kikwete katika uanzishaji ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari nchini ,mbunge wa jimbo la Kalenga Godfrey Mgimwa ameahidi kuchangia kushirikiana na shule ya sekondari Kidamali na shule nyingine jimboni humo ambazo zitaanzisha ujenzi wa maabara.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa maabara katika shule ya Sekondari Kidamali ,mbunge Mgimwa alisema kuwa mbali ya kuupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuja na wazo la kujenga maabara kwa upande wake kama mbunge atakuwa bega kwa bega na wananchi wake katika ujenzi wa maabara katika shule za sekondari kama ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dr Kikwete .
” Kazi mnayoifanya ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono na kila mdau wa maendeleo katika jimbo la Kalenga kwani kati ya maagizo ya Rais mheshimiwa Dr Jakaya mrisho Kikwete ni Halmashauri za wilaya na mikoa kuanzisha ujenzi wa maabara za sayansi katika shule zake za sekondari …..hivyo mimi kama mbunge wenu nimefurahishwa sana na jitihada hizi” alisema mbunge Mgimwa
Kuwa iwapo shule zote za sekondari katika jimbo la Kalenga zikaanza mkakati wa ujenzi wa maabara za sayansi ari ya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi itakuwa juu zaidi na kuwa kazi yake kama mbunge ni kuona anaendelea kuunga mkono shule zote zitakazoanzisha ujenzi wa maabara hizo.
Alisema kuwa mbali ya kuwa elimu katika jimbo lake la Kalenga inaendelea vema ila bado kuna haja ya shule zote za sekondari katika jimbo hilo kuwa na maabara ya masomo ya Sayansi .
” Maendeleo ambayo mmeanzisha ni makubwa sana na mimi kama mbunge najivunia kuona shule inaanzisha mpango huu na zaidi nampongeza sana mkuu wa shule ambaye amekuja na wazo hilo na mdau mkubwa wa maendeleo kata ya Nzihi mkulima George Filiakosi aliyejitolea kuandaa chakula ili watu wafike kuchangia ujenzi huo …..mimi kama mbunge nitawachangia milioni 1 pamoja na kujitolea bati zote za kuezekea jengo hilo pindi litakapo malizika “
Mbali ya mbunge huyo kujitolea kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Sixtus Kanyama aliwapongeza wadau mbali mbali hasa George Filiakosi kwa kuendelea kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo huku akiwaomba wadau wengine waliopo nje ya jimbo la Kalenga kuunga mkono jitihada za mbunge wao kwa kujitokeza kuchangia ujenzi huo .
Mkuu huyo wa shule alisema kuwa ili kukamilisha ujenzi wa maabara hiyo ya kisasa jumla ya zaidi ya Tsh milioni 200 zinahitajika na kuwa kwa wale ambao watakuwa tayari kuunga mkono ujenzi huo wanaweza kuchangia kwa kupitia akaundi ya shule Kidamali sec School namba 6051100149 benki ya NMB ama kwa jina ya M- Pesa kwa namba ya mkuu wa shule 0752 507519
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na diwani wa kata ya Nzihi Stephen Mhapa alisema kuwa wapo baadhi ya wananchi wa kata hiyo ambao mbali ya kualikwa kufika kuchangia ujenzi huo ila hawakuweza kufika jambo ambalo alisema halipaswi kuendelea kwani kufanya hizo ni kurudisha nyuma maendeleo ya ujenzi huo na maendeleo mengine kwa ujumla wake.
|
No comments:
Post a Comment